Wakati mamia ya waandamanaji wakiingia mitaani mwishoni mwa juma huko Oromia na Amhara, ambayo ni mikoa miwili mikubwa ya kiutawala nchini Ethiopia, vikosi vya ulinzi vilimimina risasi za moto kwa waandamanaji. Kwa mujibu wa taarifa za tovuti na mitandao ya kijamii, waandamanaji wapatao 100 waliuawa.
Maandamano ndani ya Oromia na Amhara yalianza kwa nyakati tofauti na kwa sababu tofauti, lakini iliyo kubwa ni madai ya kisiasa. Ndani ya mikoa yote miwili, waandamanaji wanapinga utawala wa wasomi kutoka kabila moja -waTigrai- katika siasa za Ethiopia. Mgawanyo wa mali na madaraka kati ya wa-Ethiopia wapatao milioni 100 unafanywa kwa upendeleo wa kikabila. Wa-Tigrai ni asilimia 6 ya raia wa Ethiopia lakini ndio wanaoshikilia nafasi za juu katika jeshi na serikali. Kwa 34%, Wa-Oromo ambao ni asilimia 34 ya watu wote nchini humo, ndilo kabila kubwa nchini Ethiopia, lakini hata hivyo wana uwakilishi wa jina tu katika serikali. Na Wa-Amhara wanawakilisha asilimia 27 nyingine ya watu nchini.
Undani wa idadi halisi ya vifo ilikuwa ngumu kupatikana kabla ya Jumatatu kwa sababu serikaliilifunga huduma ya intaneti pamoja na huduma ya simu katika mkoa wa Oromia na baadhi ya sehemu za mkoa wa Amhara. Mazishi ya waliouawa yalifanyika siku za Jumatatu na Jumanne katika mji wa Bahir Dar na vitongoji kadhaa vyaOromia.
Licha ya serikali kuwa na nia ya kutumia nguvu za kijeshi, wito wa maandamano zaidi katika mikoa ya Oromia na Amhara ulishachukua nafasi katika mtandao waFacebook. Wanaharakati wa ndani ya Ethiopia na nje ya nchi, wanadai kuwa maandamano hayatapungua labda serikali ifungue mlango wa siasa za umoja huko Oromia na Amhara.
Mwisho wa wiki wa mauaji katika Amhara na Oromia
Katika Makao makuu ya mkoa wa Amhara, Bahir Dar, yameshuhudiwa maandamano makubwa ambayo hayajaonekana kwa miongo mingi hapo Jumamosi baada ya wakazi wa mji huo kuingia mitaani kuandamana, wakipinga mamlaka iliyoua waandamanaji karibu 20 karibia na mji wa kihistoria wa Gonder wiki mbili kablaKulingana na taarifa za shirika la Kutetea Haki za Binadamu (Amnesty International), watu wapatao 30 waliuawa kwa siku moja huko Bahir Dar.
Vile vile, huko Oromia watu wapatao 50 waliuawa na mamia wengine walikamatwa. Katika mji mkuu Addis Ababa, mamia ya waandamanaji walijaribu kujikusanya katika viwanja vya Meskel, lakini walitawanywa kwa haraka na kwa nguvu kubwa na vyombo vya usalama. Siku ya Jumanne adhuhuri saa saba na dakika arobaini video ya pili iliwekwa katika tovuti ya EthioTube ikionesha vyombo vya usalama vikiwapiga waandamanaji kikatili. [Bofya hapo chini uweze kuangalia]
Waandamanaji wa Amhara
Maandamano ya Amhara yalianza Julai 12, 2016 wakati vyombo vya usalama vilipojaribu kumkamata kiongozi wa Kundi la Wolqait Linalodai Kutambuliwa, Kanali Demeka Zewdu, kwa tuhuma za ugaidi. Waandamanaji wa Amhara na viongozi wao wanadai kurejeshwa kwa jimbo la Welkait-Tegede katika mkoa wa Amhara kutoka kwa mamlaka ya mkoa wa karibu wa Tigrai.
Taarifa za habari na taarifa za mitandao ya kijamii zinaonesha kero za wanajamii ya Welkait-Tegede zimejengeka kwa muda sasa hasa kuhusu kile wanaharakati walichosema katika uhalalishaji wa ardhi yao na kuingiza utambulisho wao kwa nguvu katika jimbo la Tigrai. Inashangaza, siasa, uchumi na nguvu za kijeshi zisizowiana, zimeachwa kwa kundi la wasomi wachache wanoibukia kutoka mkoa wa Tigrai.
Hata hivyo watoa maoni wa upande wa serikali walipuuzia nguvu ya wasomi wa Ki-Tigrari na badala yake walilaumu makundi pinzani kwa kulipigia debe swala la jamii ya watu wa Welkait-Tegede bila kuzingatia uwiano.
Waandamanaji wa Oromia
Maandamano ndani ya Oromia ni muendelezo wa maandamano ambayo yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku tangu Novemba 2015.
Awali, maandamano yalianzia Oromia pale wanafunzi walipoidai serikali kuacha mpango wake wa kuupanua mji mkuu wa Addis Ababa kuelekea katika sehemu za mashamba ya Oromia. Wanafunzi walisema kuwa mpango huo tata wa kuupanua mji wa Addis Ababa kuelekea Oromia kutasababisha kufukuzwa kwa wakulima wengi hasa wenye asili ya Ki-Oromo.
Serikali iliyakataa mashitaka hayo, ikidai kuwa upanuzi huo ulilenga tu kuwezesha maendeleo ya miundo mbinu kama vile barabara, maboresho mengine pamoja na sehemu za burudani.
Ingawa serikali ilifuta mpango wa upanuzi wa Addis Ababa, hatua hiyo inaonekana kukwamishwa na madai ya waandamanaji yanayojumuisha suala kubwa la utawala huru, uhuru na utambulisho. Kwa mfano, wanafunzi wanadai kuwa ki-Oromo kiwe lugha ya taifa. Ki-Oromo, lugha ya watu wa Oromo ndio lugha inayozungumzwa zaidi nchini Ethiopia na lugha ya nne kwa ukubwa barani Afrika. Pamoja na hayo, hiyo sio lugha rasmi kwa serikali ya shirikisho.
Hapo Mei 2014, serikali ilifuta mpango wa upanuzi wa mji mkuu ili kupunguza maandamano ya wanafunzi yaliyopelekea wanafunzi 12 kuuwawa na mamia wenye asili ya ki-Oromo kufungwa jela. Lakini Novemba 2015, serikali iliamua kuufufua mpango wa upanuzi wa mji mkuu. Kwa sasa hatuna uhakika kama serikali itaufufua mpango huo tena.
Madai ya utawala huru katika mikoa mingine
Kukamatwa kwa viongozi maarufu kadhaa wa upinzani kama vile Bekele Gerba na Yonatan Tesfaye, ukandamizwaji wa waandishi wa habari na wanablogu na utawanywaji wa kikatili kwa waandamanaji kunakofanywa na vyombo vya usalama, watu wapatao 500 wameshakufa na taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch kumechochea maandamano mapya huko Oromia.
Msemaji wa serikali ya Ethiopia Getachew Reda mara kwa maraanasema kuwa hakuna suluhu ya kisiasa kwa kuwa serikali ilishinda uchaguzi wa bunge uliofanyika karibuni hapo Mei 2015 kwa asilimia 100.
Waangalizi wanasema kuwa hii ni changamoto kubwa sana ambayo serikali ya Ethiopia inakumbana nayo tangu iwepo madarakani mwaka 1991. Ya karibuni ilikuwa ni mwaka 2005 wakati Ethiopia ilipofanya uchaguzi pekee wenye ushindani wa kweli.
Lakini baadayemaswali kuhusu kujitawala na utambulisho vimekuwa moja ya vyanzo vya misuguano ya kisiasa. Hapo Aprili kulikuwa na mifano ya maandamano ya vurugu waandamanaji wakidai utawala huru katika ukanda wa Kusini mwa nchi, hasa katika eneo la Konso. Pia kulikuwa na mgogoro wa kufanana na huo katika ukanda wa Kusini Magharibi mwa jimbo la Gambela hapo Januari 2016.
Mtumiaji wa mtandao wa Twita, Awol alitoa maoni yanayofanana na hayo akisema, hii ni hatua muhimu sana ya kisiasa baada ya wananchi wengi kuchukua hatua tangu kifo cha Waziri Mkuu Meles Zenawi:
#MaandamanoyaOromoMbio zinazoendelea nchi nzima ni muhimu sana kwa maendeleo ya kisiasa kwa Ethiopia tangu kifo cha Meles Zenawi
— Awol Allo (@awol_allo) Agosti 6, 2016
Mbio zinazoendelea nchi nzima ni muhimu sana kwa maendeleo ya kisiasa kwa Ethiopia tangu kifo cha Meles Zenawi
Kufuatia uchaguzi wa mwaka 2005 serikali iliwapiga risasi waandamanaji wapatao mia tatu baada ya Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Meles Zenawi, kutangaza hali ya hatari wakati watu waliokuwa wanawaunga mkono wapinzani kuamua kuingia mtaani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Kuonesha kiwango cha kupinga serikali kilichooneshwa na waandamanaji, vyombo vya habari vya Ethiopia vilisambaza picha hiyo hapo chini:
#MaandamanoyaOromo: Tukio lingine la kuonesha mapigano ya nguvu . Wazee wakipigana na vyombo vya usalama huko Oromia #Ethiopia pic.twitter.com/zVdEZMtPWJ
— Vyombo vya habari vya Ethiopia (@abenezer_a) Agosti 10, 2016
Tukio lingine la kuonesha mapigano ya nguvu. Wazee wakipigana na vyombo vya usalama huko Oromia
Katika kurasa za Facebook, Balcha Mitiku aliwashauri waandamanaji wasifanye vurugu:
Tafadhali endelezeni ustaarabu mliouonesha kwa kipindi chote, msiguse raia wala mali zao.
Mtumiaji wa Facebook mwenye jina la ‘Fair Man’ yaani Mtu wa Haki alinukuliwa akisema: :
Kwa kasi hii ya kuondoa utawala na kushughulikia Ethiopia huru na ya haki iko karibu. Nawaomba wanaharakati kusimamia na kusaidia kujenga mapambano yenye kusudi la kutengeneza Ethiopia huru na ya haki ambayo tutakuwa nayo hivi karibuni.
Sanyiikoo Oromoo alijaribu kuonesha utulivu wa waandamanaji:
Watu wa Oromo ni wapenda amani. Sisi sio wachokozi. Watu walitembea wakiwa wamebeba vitabu vya dini na matawi mabichi ya miti kuonesha kuwa maandano yao hayakuandaliwa kwa ajili ya mapambano. Lakini bado walishambuliwa kinyama.