Mnamo Mei 1, blogu ya Somali Faces iliandika habari kuhusu mama mmoja maskini wa ki-Somali anayeishi kama mkimbizi licha ya kuwa na watoto nane wadogo, ambao kati yao hakuna anayekwenda shule.
Alikuwa akikabiliana na vitendo vya ubaguzi kutoka kwa majirani zake kwa sababu ya kutoka kwenye ukoo mdogo wa kabila lisilofahamika sana ki-Somali na kwa sababu ya rangi yake nyeusi. Alijaribu kujinyonga.
Wakati mwingine ninatendewa kama mgeni ndani ya nchi yangu mwenyewe, kama vile si mwenyeji wa hapa. Mimi ni mama asiye na mume mwenye watoto nane na hakuna hata mtoto wangu mmoja anayekwenda shule. Ninasafisha nyumba nikiwa nimembeba mtoto huyu niliyembeba sasa hivi. Watoto wangu wengine waliobaki hutafuta vibarua vyovyote wanavyoweza kuvipata. Ninafahamu ni maisha magumu na si rahisi lakini kinachonifanya nione maisha yawe magumu na yasiyovumilika ni namna watu wanavyotendea mimi na watu wangu. Wakati mwingine najisikia kama niko kwenye bahari ya watu wenye mioyo ya mawe. Wengi wananibagua kwa sababu ya kuwa na ngozi nyeusi. Ninawaambia, hivi ndivyo Mungu alivyoniumba na sina uwezi wa kujibadilisha. Wananinyanyapaa ama kwa sababu ya kutoka uko mdogo au kwa sababu ya rangi yangu nyeusi. Wakati mwingine ninafikiri kifo ni unafuu kwetu kuliko kuishi maisha ya namna hii.
wasomaji waliguswa na habari hiyo, na kuanza kuchanga fedha kwa ajili ya kumsaidia. Jumla ya Dola za Marekani 4,000 zilichangwa ndani ya kipindi cha saa 21.
Baada ya michango hiyo, blogu ya Somali Faces ilitoa taarifa:
Michango yenu imebadili maisha ya familia ya mama yule. Kwa sababu yenu, sasa ataweza kumiliki duka lake mwenyewe, nyumba yake itakarabatiwa na alituambia wamba kwa fedha atakazokuwa akizipata kwa biashara ya duka, sasa ataweza kulipa ada za watoto wake wapate elimu. Uso wake umejaa tabasamu na furaha wakati huu; alikosa kabisa maneno sahihi. Hakuwa kufikiri kwamba siku moja angepokea kiasi kikubwa fedha kiasi hiki. Wiki moja lililopita, alikuwa akibaguliwa, alijiona hana matumaini na hakuwa hata na senti moja na sasa, ana chanzo endelevu cha mapato kumwezesha kutunza familia yake. Tunamshukuru kila mmoja wenu kwa ukarimu na jitihada za kubadili maisha ya mama huyu. Blogu ya Somali Faces ilihakikisha kwamba kila dola mliyoituma ilitumika kuboresha maisha ya familia hiyo na tulihusika kwa karibu kwa kila hatua katika kufuatilia matumizi ya kilichopatikana. Tunapenda kuishukuru Chama cha Jamii cha Tadamun (TAAS) kwa msaada wao wa kipekee. Tutakuwa tukifuatilia maendeleo na tutawapa video ya kinachoendelea katika kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi sita kuanzia sasa kuhusu namna yeye na watoto wake wazuri wanavyoendelea.
Somali Faces ni mradi wa mtandaoni unaoeneza habari za kila siku za maisha ya watu wa kawaida wa Somalia kutoka duniani kote. Wazo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ubunifu wa Donia Jamal Adam, mwanahabari, mtetezi na mpiganiaji wa haki za binadamu; na Mohammed Ibrahim Shire, mhariri na mpenzi wa historia.