Mbeki Rais wa Mstaafu wa Afrika Kusini Bado Anaamini ‘Mambo ya Ajabu’ Kuhusu UKIMWI/VVU

Former South Africa's president Thabo Mbeki. Image released under Creative Commons by Antônio Milena/ABr.

Rais mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki anasema kirusi hawezi kusababisha UKIMWI. Picha imetolewa kwa leseni ya Creative Commons na Antônio Milena/ABr.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki imewasha upya mjadala wenye utata unaolenga kuukana UKIMWI baada ya kuandika makala yenye kichwa cha habari “Maoni Mafupi kwenye Swali la VVU/UKIMWI.

Akiwa madarakani, Mbeki na waziri wake wa zamani wa Afya Manto Tshabalala-Msimang, aliyepachikwa jina la utani “Dk. Magimbi,” walituhumiwa kwa kupinga kwamba Virusi Vya UKIMWI (VVU) vinasababisha UKIMWI, pamoja na kuwepo ushahidi wa kisayansi unaothibitisha suala hilo. Manto Tshabalala-Msimang alitangaza matumizi ya malimao, magimbi, vitunguu saumu na mafuta ya mzeituni kuwa ndiyo tiba sahihi ya UKIMWI.

Wakati wa urais wake kati ya mwaka 1999 na 2008, Mbeki aliwatuhumu wanasayansi wanaohusisha VVU na UKIMWI kwa ubaguzi wa rangi. Alidai kwamba kukubaliana na porojo za Kimagharibi kuhusu UKIMWI ni upuuzi na ni dalili za uelewa finyu. Alipinga matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV), akisema zilikuwa ‘sumu’ na ni bidhaa zilizokubaliwa na makampuni ya madawa kwenye nchi za Magharibi.

Aliunda Jopo la Kumshauri Rais kuhusu VVU/UKIMWI mwaka 2000, lililokuwa na wanasayansi kama Peter Duesberg na Harvey Bialy, ambao nao wanadai kwamba VVU havisababishi UKIMWI.

Kwenye makala yake ya Machi 7, 2016, Mbeki alipinga madai kwamba aliwahi kusema VVU havisababishi UKIMWI. Anachoamini, anasema, ni kwamba virusi hivyo haviwezi kusababisha dalili za upungufu wa kinga:

Ni lazima niseme kwamba sijawahi kusema “VVU havisababishi UKIMWI”. Hizi ni shutma zilizotolewa na watu wanaonufaika na kampeni ya vibwagizo vya “VVU vinasababisha UKIMWI” utafikiri ni mafundisho ya kidini. Nilichosema ni kwamba “virusi haviwezi kusababisha upungufu wa kinga”.

Kama unavyofahamu, UKIMWI ni kifupisho cha maneno “Upungufu wa Kinga Mwilini” – na hivyo UKIMWI ni upungufu wa kinga, yaani, mkusanyiko wa magonjwa yanayofahamika, yenye visababishi vinavyofahamika. Magonjwa hayo, kwa pamoja, hayasabishwi na kirusi kimoja! Nilisema kwamba UKIMWI unaweza kuwa sababu moja wapo ya upungufu wa kinga -yaani UKI kwenye neno UKIMWI!

'Red Ribbon' symbol of solidarity of people living with HIV/AIDS. Image by Flickr user Andy McCarthy UK (CC BY-NC 2.0).

“Utepe Mwekendu’ alama ya mshikamano wa watu wanaishi na VVU/UKIMWI. Picha na mtumiaji wa Flickr Andy McCarthy UK (CC BY-NC 2.0).

Inakadiriwa kwamba maoni ya Mbeki na upinzani wake dhidi ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi (ARV) wakati wa urais wake vimesababisha takribani vifo 365,000 vya wagonjwa wa UKIMWI.

Akijibu wakosoaji wake kuwa kauli zake tata kuhusu VVU na UKIMWI zimesababisha vifo vingi nchini mwake, Mbeki alitoa takwimu kutoka Shirika la Takwimu la Nchi hiyo (Statssa) zinazonesha vyanzo vikuu kumi vya vifo nchini humo kwa mwaka 2006 ambapo UKIMWI ulikuwa nambari tisa na akaelekeza maswali kadhaa kwa wakosoaji wake:

Kama unavyoona hapo juu [tazama makala yake kamili kwa takwimu anazozirejea], Shirika la Takwimu lilionesha kwamba vifo vinavyotokana na “Ugonjwa wa UKIMWI” vinashika nafasi ya tisa kwenye orodha ya sababu za vifo nchini Afrika Kusini mwaka 2006, kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.

Ninashawishika kuwa ili suala hili lieeleweke vizuri Mwafrika wa kawaida anayefikiri vizuri angeuliza maswali yafuatayo:

Ilikuwaje tukasikia kelele nyingi kutoka kwenye nchi za Kimagharibi kuhusu sababu ya tisa ya vifo nchini mwetu, wakati hatusikii chochote dhidi ya kifua kikuu kinachoongoza kwa kusababisha vifo?

Kwa nini Serikali ya Afrika Kusini, inayofahamu hali ya afya ya watu wake vizuri, itarajiwe kuhangaika na ugonjwa ambao ni sababu ya tisa ya vifo na isiweke nguvu yoyote ya dharura kwa sababu nane (8) nyingine za vifo?

Je, hii inahusiana na ukweli kuwa Afrika Kusini inaweza kuwa soko muhimu la mauzo ya dawa za kupunguza makali ya vurisi (ARV), kama ilivyo sasa?

‘Jaribio la Kujenga Upya Sura ya Urais Wake’

Akijibu makala ya Mbeki, Katherine Furman, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PHD) katika filosofia kwenye Shule Kuu ya London ya Uchumi na Sayansi ya Siasa, alifikiri kile kinachomfanya Mbeki achukue hatua alizochukua akiwa rais:

Jumuiya ya kimataifa ya sayansi imekuwa wazi kwa kutokukubaliana naye kupitia Azimio la Durban , tamko lililotiliwa saini na zaidi ya wanasayansi 5000 waliounga mkono maoni ya kisayansi kuhusu VVU na UKIMWI.

Ni wazi kuwa Mbeki lazima aupe uzito upinzani anaoupata kutoka kwa wanasayansi, kwa kuzingatia kwamba wao ni wataalam. Lakini sehemu ya kile kilichokosewa kwenye suala la Mbeki ni kwamba haonekani kuelewa wataalam hasa ni akina nani. Anaamini kwamba wanasayansi wapinzani anaowaunga mkono walikuwa kundi la wachache waliotengwa ambao hawajawa wakitendewa ilivyo haki na jumuiya ya wanasayansi wenzao – akiamini kwamba alikuwa anafahamu vilivyo kuwa hayo yote ni sehemu ya mapambano dhidi ya ukaburu.

Tunaweza kukubaliana, hata hivyo, kwamba labda kuchanganyikiwa kwa Mbeki kunaweza kueleweka katika mazingira hayo. Lakini hata alipoletewa Azimio la Durban, Mbeki hakurudi nyuma na kutafakari upya msimamo wake. Hali hii inashangaza.

Kufuatia kuchapishwa kwa makala ya Mbeki, Kerry Cullinan, mhariri mtendaji wa tovuti ya habari za afya Health-e.org, alisema Mbeki ameonesha kwamba hajisikii kusutwa na dhamira kwa sera zake:

Mara nyingine nimefikiri huenda rais mstaafu Thabo Mbeki amejutia msimamo wake kuhusu VVU na UKIMWI, kufuatia kuongezeka kwa umri wa kuishi tangu ang'olewe madarakani.

Lakini leo, sifikiri tena hayo kwa sababu Mbeki ameendelea kusimamia imani zake hizo za kushangaza kuhusu UKIMWI kwenye tovuti yake na kwenye mfululizo wa barua anazoziandika kujaribu kujenga upya kipindi cha urais wake.

Wakati kila mwaka katika kipindi cha urais wa Mbeki wastani wa umri wa kuishi ulikuwa ukipungua kila mwaka, baada ya kung'olewa na serikali mpya kuweka mikakati imara ya kupambana na VVU/UKIMWI ikiwa ni pamoja na kusambaza madawa ya kupunguza makali ya virusi (ARV), wastani wa umri wa kuishi umeongezeka mwaka hadi mwaka.

Sanele Sano Ngcobo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pretoria, alimpa changamoto Mbeki kuhusiana na suala la ARV:

Makala yako inapinga kwa namna isiyo ya moja kwa moja ukweli uliothibitika kisayansi kwamba madawa ya kupunguza makali ya VVU (ARV) yameokoa maisha ya raia wengi wa Afrika Kusini.

Ningependa nikushirikishe habari chache za mafanikio ya matumizi ya ARV:

Mwaka 2005, wastani wa umri wa kuishi nchini Afrika Kusini ulikuwa miaka 51 na leo hii ni miaka 61. Nchini Zimbabwe wastani wa umri wa kuishi ulikuwa miaka 44 mwaka 2000 na leo ni miaka 60. Nchi hizi mbili ziliamua kutekeleza kwa nguvu mipango ya kusambaza dawa za ARV.

Kwa sababu ya matumizi ya ARV, vifo vinavyotokana na VVU vimepungua kwa:

  • asimilia 58 nchini Afrika Kusini
  • asilimia 71 nchini Ethiopia
  • asilimia 64 nchini Thailand, na
  • asilimia 87 nchini Senegal.

Nchi zote hizi zilianza kutekeleza kwa bidii mipango ya matumizi ya ARV. Tunahitaji ushahidi upi zaidi kwamba ARV zinaokoa maisha ya watu wetu?

Umejenga hoja kwamba makampuni ya madawa nchini Marekani yanataka kunufaika na usambazaji wa ARV, hata hivyo mnamo Aprili 19 2001 serikali yako iliamua kutunga sheria inayoruhusu kuzalishwa kwa madawa ya bei nafuu -ikiwa ni pamoja na ARV -kinyume na kesi iliyokuwa imefunguliwa na makampuni makubwa ya kimataifa ya madawa.

Kwa nini hamkuwekeza kwenye makampuni ya ndani ili kuzalisha madawa ya ARV?

‘Tamko Jepesi la Kuomba Radhi…Lingetosha ‘

Akitoa maoni yake kuhusu suala hilo kwenye mtandao wa Twita, Africa is a Country alisema:

Tutajifanya hatukumwona rais mstaafu wa Afrika Kusuni Thabo Mbeki akieneza imani zake za ajabu dhidi ya VVU/UKIMWI

Wakati huo huo Muzi Maseko alimshauri rais mstaafu kuomba radhi:

Tamko jepesi la kuomba radhi kutoka kwa Rais mstaafu Mbeki, kuhusu imani zake za kudai VVU haisababishi UKIMWI na kusababisha vifo 300,000 lingetosha.

Hata hivyo, Mbeki ana watu wanaomwuunga mkono pia. Nande N alijaribu kueleza msimamo wa Mbeki kwa wakosoaji wake:

Msimamo wa Mbeki wala haukusudii kukanusha uwepo wa UKIMWI isipokuwa kuunganisha kwa kisababishi kati ya VVU na UKIMWI

Msizi James alitaka majadiliano kuhusu rais huyo wa zamani yawe kwenye siha njema za uongozi wake:

Tuzungumzie namna alivyokuwa imara. Ukiacha imani zake kwamba UKIMWI haukuwa tatizo kuu

Mtumiaji mwingine wa mtandao anaonekana kupendekeza kwamba ni vigumu kwa wataalam wa UKIMWI kupingana na madai ya Mbeki:

Hawa ‘wataalam’ wote wa VVU/UKIMWI anaopiga kelele za “Mbeki anajifanya hauoni UKIMWI” watakuwa na wakati mgumu kukanusha kile anachokidai Mbeki

Watafiti wawili huru wa UKIMWI, Anthony Brink na Chris Rawiins, wanaokataa kile kinachosemwa na sayansi kuhusu uhusiano kati ya VVU na UKIMWI, wameunga mkono kile alichokiandika Mbeki.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.