Sheria ya Makosa ya Mtandao Tanzania Inafanya Iwe Hatari ‘Kumtukana’ Rais Kwenye Mtandao wa Facebook

Image shared on Twitter by Tanzanian Member of Parliament Zitto Kabwe Ruyagwa. (@zittokabwe)

Picha imewekwa kwenye mtandao wa Twita na Mbunge wa Tanzania Zitto Kabwe Ruyagwa. (@zittokabwe)

Mtanzania anayetumia mtandao wa intaneti Isaac Habakuk Emily, anayeishi mkoani Arusha kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika, alisimamishwa kizimbani mnamo Aprili 15, 2016 kwa makosa ya “kumtukana” rais wa nchi hiyo, John Magufuli. Maneno ya Emily yanadaiwa kukiuka kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Tanzania Na. 14 ya 2015, kinachosema:

Mtu yeyote anayechapisha taarifa, takwimu au habari katika picha, maandishi, alama au kwa namna nyingine yoyote katika mfumo wa kompyuta ambapo taarifa hizo, takwimu au habari hizo ni za uongo, zenye udanganyifu, zenye kupotosha ukweli au zisizo sahihi atakuwa anatenda kosa, na akitiwa hatiani atatakiwa kulipa fidia ya si chini ya shilingi milioni tatu kifungo jela kisichopungua miezi sita jela au vyote viwili kwa pamoja

Emily anadaiwa kuchapisha ujumbe wenye utata kwenye mtandao wa Facebook kwa lugha ya Kiswahili mnamo Machi 17, 2015, hali akijua kwamba kumkosoa rais wa nchi ni kinyume cha sheria. Maoni yake hayo kwenye mtandao wa facebook yalihusu kitendo cha Rais Magufuli kupiga simu isiyotarajiwa kwenye kipindi kinachooneshwa na kituo cha televisheni cha Clouds TV kinachohusu habari zinazojiri kiitwacho 360. Rais alitumia kipindi hicho kuwashukuru watangazaji wa kipindi hicho na kuonesha alivyo shabiki wa kipindi hicho.

Pamoja na kwambaukurasa huo binafsi wa Facebook wa Emily, na hata ukurasa wa majadiliano anaodaiwa kuchapishia maoni hayo, hayaonekani kwa kutafutwa kwenye mtandao wa Facebook, lakini maoni yake hayo ya Facebook yanadaiwa kusomeka:

Hizi siasa za maigizo, halafu mnamfananisha huyu bwege and Nyerere wapi buana.

Kosa lake hilo limetokea wakati bunge la Tanzania limepitisha muswada wa makosa ya mtandao mnamo Aprili 1, 2015, kukabiliana na masuala yanayohusu makosa ya mtandao kama vile picha za ngono kwa watoto, kashfa za mtandaoni, matusi dhidi ya watu binafsi, utengenezaji wa maudhui yanayoleta hisia za ubaguzi wa rangi au kikabila, utumaji wa ujumbe bila ruhusa ya mpokeaji, kuingilia mawasiliano kinyume cha sheria na kutengeneza taarifa za uongo.

Pamoja upinzani mkubwa dhidi ya hatua hiyo kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanasiasa, wadau wa mitandao ya kijamii, wafadhili na wanaharakati wa haki za raia, muswada huo ulipitishwa bungeni baada ya mjadala mfupi. Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliutia saini uwe sheria mwezi Mei 2015.

Wanaopinga Sheria ya Makosa ya Mtandao wanasema kwamba sheria hiyo inawapa mamlaka makubwa — bila udhibiti wowote– polisi, ukiwapa uwezo wa kupekua nyumba za wanaotuhumiwa kuvunja sheria hiyo, kukamata vifaa vya kielektroniki, na kudai taarifa-pepe (data) kutoka kwenye makampuni yanayotoa huduma za mtandao wa intaneti. Wanaonya kwamba polisi au dola inaweza kutumia mamlaka hayo kuwabughudhi wanaharakati wa mtandnaoni au watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Mwezi Oktoba 2015, wa-Tanzania wawili walikuwa wahanga wa kwanza wa sheria hiyo mpya. Benedict Angelo Ngonyani, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 24 katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, alishitakiwa kwa kuchapisha maudhui ambayo “ni ya uongo au hayajathibitishwa na mamlaka zinazohusika.” Inadaiwa kwamba alichapisha bandiko la Facebook lililodai kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, alikuwa amelazwa kwa sababu alikuwa amekula chakula chenye sumu.

Mwezi huo huo, mtumiaji mwingine wa mtandao, Sospiter Jonas, alisimamishwa kizimbani kwenye mahakama ya mwanzo mkoani Dodoma kwa kosa la ‘kutumia vibaya mtandao’ baada ya kubandika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook akisema Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda “atakuwa mhubiri wa dini.”

Mwezi Novemba 2015, wa-Tanzania wengine wanne — Leila Sinare, Godfrey Soka, Deo Soka na Monica Gaspary Soka — walishitakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 kwa kuchapisha taarifa za uongo za kielektroniki kwenye mtandao wa kuandikiana ujumbe mfupi uitwao WhatsApp. Wanne haoa walisimamishwa mbele ya Hakimu Mkazi jijini Dar Es Salaam mnamo Novemba 6, 2015. Mwendesha mashtaka wa serikali alidai kwamba watuhumiwa hao walichapisha taarifa ya sauti kwenye kundi la WhatsApp linaloitwa “Soka Group”, ambayo ilikusudia kupotosha umma wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 nchini Tanzania , ambao uligubikwa na madai ya wizi wa kura.

Kwa tukio la hivi karibuni, Emily anatarajiwa kusimamishwa kizimbani tena mnamo Aprili 18, 2016 kwa ajili ya maamuzi ya ombi lake la dhamana.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.