Kuibuka kwa mitandao ya kijamii kumeleta mapinduzi makubwa katika namna vyombo vya habari vinavyopeleka habari zake kwa hadhira yao barani Afrika, hususani nchini Ghana. Mashirika ya habari hivi sasa yanategemea majukwaa ya mitandao ya kijamii kama njia muhimu ya kueneza habari zao.
Katika kutathmini matumizi halisi ya mitandao ya kijamii katika mashirika ya habari nchini Ghana, Penplusbytes, shirika lisilo la kibiahsra linalofanya kazi ya kukuza ufanisi wa kiutawala kwa kutumia teknolojia barani Afrika, limetoa Ripoti ya Kiwango vya Mitandao ya Kijamii (SMI) kwa vyombo vya habari vya magazeti, radio na televisheni.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Penplusbytes, utafiti wa ufanisi wa vyombo vya habari ulitathmini shughuli za vyombo vya habari kwenye mitandao ya kijamii kufikia Februari 8, 2016, na kwa namna gani vyombo hivyo vilitumia majukwaa ya mitandao ya kijamii, hususani Twita na Facebook, kuwasiliana na hadhira wanayoilenga. Utafiti huo ulijumuisha magazeti 37 yaliyo hai na/au yanayoonekana zaidi kwenye meza za mauzo mitaani. Utafiti huo pia ulichunguza vituo 16 vya televisheni kati ya 22 na vituo 309 vya radio kati ya 390 vinavyorusha matangazo yake.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kiwango cha chini cha matumizi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya magazeti. Magazeti mengi nchini Ghana hayapatikani kwenye mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwa radio na televisheni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya magezeti 37, 20 pekee yana kurasa hai kwenye mtandao wa Facebook, na sita pekee yalikuwa na anuani ya Twita.
Radio
Vituo vya radio nchini Ghana, kwa mujibu wa ripoti hiyo, vinatumia mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa katika kuwasiliana na wasikilizaji wake kuliko magazeti. Citi FM, moja wapo ya vituo maarufu vya radio nchini Ghana, kilibainishwa kuwa mbele zaidi katika matumizi ya mitandao ya kijamii nchini Ghana. Citi FM ina zaidi ya wafuatiliaji 600,000 kwenye mtandao wa Facebook na akaunti yake ya Twita iliyohakikiwa (kimsingi chombo cha kwanza cha habari nchini Ghana chenye akaunti ya Twita iliyohakikiwa) ina wafuatiliaji zaidi ya 265,000.
Joy FM, kituo kingine maarufu cha radio, kinaongoza kwenye mtandao wa Twita kwa kuwa na wafuatiliaji 330,000.
Television
Viasat 1, kituo binafsi cha televisheni, kiliripotiwa kuwa na matumizi ya kiwango cha juu ya mtandao wa Facebook — kikiwa na wafuatiliaji zaidi ya 680,000 – wakati kituo cha televisheni cha taifa Ghana Television News kilikuwa na zaidi ya wafuatiliaji zaidi ya 191,000 kwenye mtandao wa Facebook.
Magazeti
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Daily Graphic, gazeti linalosomwa zaidi nchini Ghana, lilikuwa na wafuatiliaji wengi zaidi kwenye mtandao wa Facebook likiwa na wafuatiliaji 621,000. Daily Guide, gazeti binafsi nchini humo, liliongoza kwa kuwa na wafuatiliaji wengi kwenye mtandao wa Twita – zaidi ya 12,000.
Baada ya Penplusbytes kuisambaza taarifa kwenye Facebook, Fundraising Africa, tovuti ya mtandaoni kwa ajili ya harambee za kukusanya fedha, ilikuwa na maoni yafuatayo:
Wananchi wa Ghana zaidi na zaidi wanafuatilia kwenye mitandao ya kijamii kupata taarifa hadi zinazotokea kila dakika, kwa hiyo ni mihimu kwa vyombo vya habari kukidhi kiu hii vinginevyo wananchi wanaweza kuishia kupenda vyombo vya kigeni vyenye vinavyotumia mitandao ya kijamii.
Unaweza kupakua taarifa hiyo kamili hapa.