Imeanza Kuwa Jinai Kuibua Vitendo vya Kifisadi Nchini Botswana?

Journalist Sonny Serite. Photo from

Mwandishi Sonny Serite. Picha kutoka kwenye ukurasa wake wa Twita @kivuki.

Mwandishi mwenye msimamo mkali nchini Botswana Sonny Serite alikamatwa na kushitakiwa  mnamo Machi 17 kwa kosa la kupokea mali ya wizi kinyume na Sheria ya Makosa ya Jiani nchini humo.

Serite, anayejiita “Uandishi wa ki-Bruce Lee”, anadaiwa kukamatwa na maafisa wa Ikulu ya nchini hiyo wakati akipokea karabrasha za siri kumwezesha kukamilisha habari ya ufisadi aliyokuwa akiishughulikia.

Watetezi wa Serite wanasema alipokea karabrasha hilo, ambalo haijulikani bado lilikuwa na maudhui gani, bila kujua au kuwa na sababu ya kuamini lilikuwa limepatikana kinyume cha sheria au kuibwa kutoka Ikulu.

Inaaminika karabrasha hilo linaweza kuwa na uhusiano na habari iliyochapishwa na Jarida la Botswana Gazette mnamo Machi 10 likibainisha  vitendo vya kifisadi kwenye mradi wa ununuzi wa behewa la abiria kwa ajili ya Shirika la Reli nchini humo.

Mwandishi huyo amenyimwa dhamana pamoja na kuzuiwa kukutana na mwanasheria.

Chama cha Waandishi wa Habari Botswana (BOMAWU) kimelaani kukamatwa kwake na vitendo alivyofanyiwa tangu alipokamatwa.

Wanaharakati wanaopingana na ufisadi na kupigania uhuru wa kujieleza wanaendesha kampeni kwenye mtandao wa Twita ya kudai kuachiwa kwake kwa kutumia alama habari #FreeSonnySerite [MwachieniSonnySerite].

Kuandika habari za ufisadi nao ni ufisadi nchini Botswana?

Baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Twita wametetea mwandishi huyo:

Kuufahamu ukweli unaikuhusu serikali imekuwa hatari. Kuandika masuala ya kijinai imekuwa jinai nchini Botswana na bado eti tunahubiri Kupambana na ufisadi

Unawezaje kumkamata mwandishi kwa kuibua vitendo vya ufisadi?

Unaweza kabisa kuamini hawa jamaa walioko madarakani wanaweza kuachia tu hizo nyaraka? Haiwezekani. Mfumo huu unawafanya waandishi wasiwe na chaguo jingine lolote

Ni ujinga kumshitaki mwandishi kwa kupokea taarifa, ziwe zimeibwa ama la. Unadhani tunaweza kuzipata wapi taarifa hizo, wajinga nyie!

Chochote kilichotokea fahamuni “mjumbe hauwawi”

Nini kimezikumba harakati za kupambana na ufisadi nchini Botswana?

Botswana inafahamika kama nchi yenye kiwango cha chini cha ufisadi barani Afrika kwa mujibu wa mashirika kama Transparency International. Shirika la ushauri elekezi liitwalo Cushman & Wakefield lilitoa ripoti mwaka 2015 inayofahamika kama & Masoko Makubwa Yanayoibuka iliyoonesha kwamba kwa hakika Botswana ni nchini yenye uchumi unaokua kwa kasi na yenye uwazi kuliko zote barani Afrika.

Lakini kukamatwa kwa Serite kumewafanya baadhi kusaili upya sifa hiyo:

Serikali ya Botswana inakamata mwandishi anayechunguza vitendo vya ufisadi. Uwazi tunaoambiwa upo umekwenda wapi?

Inajalisha mwandishi amepata taarifa zake ili kuibua ufisadi?

Kwenye mtandao wa Facebook, Radifalana Turpelo Bobo Ronald alikuwa na maoni kwamba waandishi lazima waweze kupata taarifa kwa namna yoyote:

[…] Bado ninasema penye ufisadi, lazima utangazwe. Hatua zilizochukuliwa dhidi ya Serite ni ushahidi wa wazi kwamba ni kweli vitendo vya ufisadi vilifanyika. Namna alivyopata taarifa haitusumbui, tunawahitaji waandishi kama yeye wanaofanya kazi bila kuchoka kuchimbua taarifa zinazohusiana na masuala yanayoiathiri Botswana.

Lakini wengine, kama Yusrah T Gareegope walisema Serite lazima ajibu mashitaka yake mbele ya sheria kama mtu mwingine yeyote:

mshikilieni Sonny Serite mpaka mtakapopata taarifa zozote zile mnazozihitaji kutoka kwake, yeye si wa kwanza wala wa mwisho kukamatwa na wala hana utofauti wowote na raia wengine wa Botswana ambao hukamatwa kila siku!

Sethamiso Moritshane alibainisha:

Yeye ni kama raia mwingine yeyote wa Botswana anayeweza kufanya makosa ya jinai, sasa kuna kipi cha pekee alichonacho?

Na Tlhagisang Duncan Sakie Masake aliandika:

Idara ya Usalama inafanya kazi nzuri. Kadri inavyowezekana tunapaswa kujifunza kuheshimu sheria na kuandika habari zenye ubora sio habari nyingi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.