- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Nguvu ya Mitandao ya Kijamii Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Uganda, 2016

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Uganda, Siasa, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi

 

Michael Niyigeteka

Michael Niyitegeka, mtaalam wa mitandao ya kijamii nchini Uganda. Picha kutoka kwenye ukurasa wake wa Twitter. @niyimic

Tarehe 18 Februari mwaka huu, nchi ya Uganda itafanya chaguzi. Kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kisiasa na majibizano nchini Uganda. Kwa mfano, mitandao ya kijamii ilibeba jukumu muhimu sana wakati wa mdahalo wa aina yake kuwahi kutokea wa mapema Januari 15. Kiungo habari #UGDecides16 [1] kilishika kasi wakati wote wa [2] mdahalo [3].

Watu wa Uganda, wanatumia sana mitandao ya kijamii pengine kuliko wakati mwingine wowote kama sehemu ya ushiriki wao kwenye mambo yanayohusu chaguzi. Kwa mujibu [4] wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda, hadi mwezi Machi 2015, Uganda ilikuwa na zaidi ya watumiaji wa intaneti milioni 11 na pia hadi mwezi Novemba 2015 kulikuwa na watumiaji wa mtandao wa Facebook zaidi ya milioni 37, huku watumiaji wa simu za mkononi walikadiriwa kufikia milioni 19 [3].

Nilikutana na Michael Niyitegeka, [5] ambaye ni mshauri mhakiki na mtaalam wa mitandao ya kijamii nchini Uganda ili kujadili mchango wa mitandao hii katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Prudence Nyamishana (PN): Mitandao ya kijamii imekuwa na mchango gani kwenye chaguzi za mwaka huu nchini Uganda?

Michael Niyitegeka (MN): Mitandao ya kijamii imefanya kazi kubwa sana ambayo hakuna yeyote ambaye alitegemea. Bila kutarajiwa, kumekuwa na hamasa kubwa kutoka kwa wanasiasa na wafuatiliaji wa siasa. Ni kama vile wamegundua kuhusu ukweli kwamba mitandao ya kijamii ni kitu ambacho hakiwezi kuchukuliwa kirahisi. Na kwa hiyo, kumekuwa na uwekezaji mkubwa, idadi kubwa ya watu wameajiriwa ili kusimamia kampeni kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kurasa za wagombea. Kwa hiyo, umuhimu wa mitandao ya kijamii nchini Uganda umeongezeka kwa kiasi kikubwa kabisa. Hata hivyo, kumekuwepo na kile ninachoweza kukiita kufanya kazi bila weledi kwa kuwa watu waliopewa jukumu la kuendesha kampeni za mtandaoni hawakuwa na mikakati madhubuti katika hatua za mwanzo za kampeni. Matokeo yake, baadhi yao walianza wakiwa imara sana, na mara wakapotea, wengine walizidi kushika kasi kadiri kampeni zilivyokuwa zikiendelea, , lakini kama wangekuwa wamejipanga vizuri mapema, wafuasi wao wangalinufaika zaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uganda wamechipukia na idadi yao imeongezeka. Kwa mfano, idadi ya watumiaji wa Twittter waliojisajili hivi karibuni wakati wa kipindi cha uchaguzi ni wengi mno. Mitandao ya Kijamii imejiweka mahali ambapo hapo awali haikuwepo-imekuwa yenye umuhimu mkubwa na inayohitajika. Watu wanatuma mitandaoni picha halisi ambazo zinapelekea baadhi ya makundi “kughushi picha” za mikusanyiko ya watu ili kuwaonesha wapiga kura kuwa wanaungwa mkono na wengi. Mitandao ya kijamii imewapa nafasi wanasiasa wengi pamoja na matukio anuai ya kisiasa kama ilivyokuwa kwa mdahalo wa Urais ambao ulifuatiliwa kwa ukaribu na kujadiliwa kwa mapana sana na watu wa Uganda kupitia mitandao ya kijamii.

PN: Unafikiri watu wa Uganda wamefanikiwa kukutana na kuchangamana na wagombea wa kiti cha Urais kupitia mitandao ya kijamii?

MN: Nionavyo mimi, kati ya mwanasiasa mmoja au wawili ndio wanaoweka taarifa kupitia Twitter wao wenyewe, wengine wote wameajiri watu wa kuwapigia kampeni kupitia mitandao ya kijamii. Wagombea walitafuta watu wa kupiga kampeni kupitia mitandao ya kijamii, na watu hao ndio wakabuni kurasa za Twitter na Facebook. Kimsingi, wanaendesha kampeni kwa niaba ya wagombea. Ni vigumu kupata ladha ya mgombea halisi, ni utaratibu wa mgombea halisi kupitia Twitter, yaani ni kama roboti linalotwiti yale ayafanyayo mgombea.

Tumefanikiwa kuzikutanisha kambi za kisiasa kwa mtazamo wa taratibu za kivyama? Chama tawala, National Resistance Movement, kimejaribu kuwa na utaratibu wa kupiga soga kupitia Twitter, hata hivyo utaratibu huu haujakuwa wa kudumu na umepelekea watu kukosa hamasa kwa sababu ya kukosekana kwa ushirikiano. Kwa mfano, kipindi ambacho chama kilimualika Mh. Rebecca Kadaga, ambaye ni spika wa kwanza Mwanamke nchini Uganda, watu walikuwa wakituma jumbe kupitia Twitter kuhusu kile alichokuwa akikijadili Kadaga, hata hivyo, ingekuwa na maana sana kama Kadaga mwenyewe angekuwa anapiga soga na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Nina uhakika kuwa utaratibu huu ungeleta utofauti mkubwa sana. Kwa hiyo, matumizi ya mitandao ya kijamii ni jambo ambalo kambi za kisiasa zimelikurupukia tu, sifikiri kuwa ni jambo ambao waliliwekea mikakati ya kutosha.

A screenshot of the official Twitter page for

Picha kutoka kwenye ukurasa rasmi wa Twitter wa Mdahalo wa Wagombea Urais wa Uganda. Tukio hili ni moja ya matukio ya uchaguzi yaliyowahi kusambazwa kwa kiasi kibubwa kabisa kupitia Twitter katika historia ya chaguzi nchini Uganda.


PN: Ni kwa kiasi gani mitandao ya kijamii imekuwa kama chombo cha kusambaza propaganda katika kipindi hiki cha uchaguzi?

MN: Uhuru wa kujieleza unaambatana na wajibu wake. Kuna wakati upotoshaji hutokea wakati wa kutoa taarifa na katika kuchangia maoni kupitia mitandao ya kijami. Wagombea wana wajibu wa kuonesha ukomavu na kuwajibika ipasavyo pale wanapotakiwa kuzungungumza, kwa kuwa, siyo tu wanaongea na mashabiki wao, bali pia ni kwa jamii nzima. Kwa hiyo, vyama vya siasa vinapaswa kuwa makini vinapotoa taarifa kwa umma. Kwa mfano, Katibu wa chama tawala alikaririwa akisema kuwa, kwa yeyote ambae angesababisha mitafaruku watoto wao wangeuawa [6], watu walirekodi ujumbe ule na kisha kuusambaza kwa kasi.

Sisi watumiaji wa mitandao pia tunawajibika na kudhibitisha taarifa kabla ya kuzisambaza kwa kuwa taarifa zisizo na udhibitisho zinaweza kuwa chanzo cha vurugu na machafuko ya kisiasa.

PN: Tupo kwenye nafasi gani kwenye suala la uhuru wa kujieleza mtandaoni?

MN: Ninaona kuwa, jamii ya watu wa Uganda bado wanafurahia kwa kisasi kikubwa uhuru wa kujieleza kupitia mtandao. Na pia, ninaamini kuwa hatuwezi kufikia kiwango walichofikia nchi kamaThailand [7] ambayo inakandamiza uhuru wa habari wa mtandaoni. Kwa kuzingatia haki na uhuru wanaoufurahia watu wa Uganda kwenye mitandao ya kijamii, kukandamiza uhuru huu itakuwa vigumu sana. Labda mtu mwenyewe aamue kuzima mtandao wa intaneti.

PN: Mitandao ya kijamii itakuwa na mchango gani kwenye uangalizi na ufuatiliaji siku ya uchaguzi?

MN: Ninafikiri kuwa kasi ya mtandao itapungua. Haya ni maoni yangu. Unajua nini, kama wewe ndiye msimamizi na unaona mambo yanaenda mrama, unaweza kuamua lolote. Lakini kwa jinsi mtandao wa intaneti ulivyosambaa, itakuwa vigumu sana kwa mtu kufanya jambo la kijinga kama hili. Kwa mfano, kuna gari la polisi huko Mbale, mjini ulio Mashariki mwa Uganda, lilionekana kusafirisha wafuasi wa chama tawala, sidhani kuwa kwa kuzingatia kiwango chao kikubwa cha kufikiri wangeweza kupiga picha na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii kama walivyofanya watumiaji wa mtandao wa intaneti. Kulikuwa pia na tukio jingine pale mtu mmoja kutoka chama tawala kupitia Twitter alidai kuwa chama cha upinzani, Forum for Democratic Change, kilikuwa kikisafirisha watu ili kuhudhuria mikutano yao, hata hivyo watu walijitokeza na kumpinga. Ili kubatilisha madai yake, watumiaji wa mitandao ya kijamii waliweka picha kadhaa za tukio hilo ambazo zilionesha katika magari hayo kulikuwa na ng’ombe. Kwa hiyo, yeyote anayehusika na uchaguzi huu, anapaswa kuwa makini.

PN: Unafikiri mitandao ya kijamii itakuwa na wajibu upi mara baada ya uchaguzi, kwa kuzingatia ushiriki wa jamii?

MN: Mitandao ya kijamii itazidi kuimarika; jukwaa hili litazidi kukua ukilinganisha na miaka mitano iliyopita. Tutashuhudia viongozi wakiwajibishwa kupitia uanaharakati wa mtandaoni, watu wengi zaidi watatilia maanani hisia na mahitaji ya wananchi wanayoyaweka bayana kupitia mtandao wa intaneti. Kwa hiyo, mitandao ya kijamii inaenda kuwa chombo cha kuwajibisha. Nikiona mtu anafanya jambo fulani, nitapiga piga na kuisambaza nikiwa na imani kuwa itaonwa na wengine wengi na watachukua hatua.

PN: Una lolote la kumalizia?

MN: Waganda kwenye mitandao ya kijamii, tunahitaji kuachana na kasumba ya kubweteka na wingi watu wanaokufuatilia, au utaratibu wa kuwa na watu wengi waliopendezwa na kile ulichokichapisha kwenye mtandao wa kijamii, tunatakiwa tufanye uchunguzi wa kina na kufanya mambo yenye tija na ambayo yatawafanya watu wasiishie tu kupendezwa au kuwa na wafuatiliaji wengi. Itakuwa vizuri kama tutakuwa tunachanganua, tunashirikiana na kuandaa vitu vyenye tija kwa ajili ya wale wanaotufuatilia. Tunafahamu kuwa kwa sasa, serikali, wafanyabiashara na kampuni mbalimbali zinatoa kipau mbele kikubwa sana kwenye mitandao ya kijamii.