Mtumiaji wa Twita Nchini Saudi Arabia Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 10 na Viboko 2,000 kwa Kosa la “Kukufuru Dini”

Blogging is bad for your back .. in Saudi Arabia. Image used as part of an Amnesty International campaign to draw attention to the plight of Saudi blogger Raif Badawi, sentenced to 10 years in prison and 1,000 lashes in Saudi Arabia in 2014 for setting up a "liberal" website

Kublogu kunahatarisha migongo na makalio ya watu …nchini Saudi Arabia. Picha imetumiwa kama sehemu ya kampeni ya Shirika la Amnesty International kutangaza uonevu aliokumbana nao mwanablogu wa ki-Saudia Raif Badawi, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela sambamba na viboko 2,000 nchini Saudi Arabia mwaka 2014 kwa kosa la kutengeneza tovuti ya ‘mambo ya kijinga’

Saudi Arabia imemhukumu mtumiaji wa mtandao wa Twita kifungo cha miaka 10 jela pamoja na viboko 2,000 kwa kuandika twiti 600 “zinazoeneza imani ya kutokutambua uwepo wa Mungu” mtandaoni.

Kwa mujibu jarida la kila siku nchini humo liitwalo Al Watan mtumiaji huyo wa mtandao wa Twita, ambaye jina lake limehifadhiwa, alihukumiwa na mahakama moja mjini Medina iliyompata na hatia ya kukana uwepo wa Mungu na kuidhihaki Kurani Tukufu, kumtuhumu mtume kwa kudanganya watu. Kadhalika, amepigwa faini ya Rayali 20,000 (sawa na Dola za Marekani 5,300). Mtu huyo alikamatwa baada ya kazi ya kufuatilia anayoyaandika kwenye mtandao wa twita kufanywa na Kitengo cha Kuzuia Makosa ya Habari kinachoundwa na Kamati ya Kukuza Maadili na Kuzuia Maovu au Polisi wa Kidini nchini Saudi Arabia.

Gazeti hilo linasema kwamba mtu huyo, mwenye umri wa miaka 28, alitangaza hadharani imani yake ya kukana uwepo wa Mungu mahakamani na kukataa kata kata jaribio la kumshawishi atubu madhambi yake, kwa kutumia kisingizio cha uhuru wake wa kujieleza. Aliongeza kwamba awali aliwahi kuwa Mwislamu na kwa sasa ameachana na dini zote baada ya kufanya mawasiliano na tovuti zinazoeneza imani ya kukana uwepo wa Mungu kupitia mtandao wa Intaneti.

Mahakama, linaoneza gazeti, ilithibitisha mashitaka hayo dhahiri dhidi ya mtu huyo kwa kutumia ushahidi wa aliyoyakiri mahakamani pamoja na ushahidi wa watu wanne waliosema walikutana na akaunti ya Twita kwenye simu yake, na kwamba ilithibitika kuwa yaliyokuwa yakifanyika kwa kutumia simu hiyo yalifanyika kwa jina lake.

Hukumu hiyo haikupata mwitikio mkubwa mtandaoni, isipokuwa baadhi ya watumiaji kubadilishana viungo vya habari zinazohusiana na tukio hilo bila kutolea maoni yoyote.

Abdulrahman, anayeishi Misri, anawaonya watumiaji wa Twita wanaoishi Saudi Arabia:

Hii ndiyo Saudi Arabia. Kijana wa miaka 28 wa ki-Saudi amehukumiwa miaka 10 jela, viboko 2,000 na kuamuriwa kulipa faini ya Riyali 20,000 kwa kosa la kutokuamini uwepo wa Mungu kwenye mtandao wa Twita.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Saudi Arabia lazima muwe waangalifu. Mnafuatiliwa, mtaadhibiwa na kutishwa. Twiti moja nyepesi inaweza kutishia maisha yako. Da. Jamii iliyojaa ujinga na ujima kiasi gani!

Kwa mujibu wa Sheria ya Saudi ya 2001, “chochote kile kinachopingana na kanuni ya msingi au sheria, au kisichoonesha adabu kwa imani ya Uislamu na Shaaria, au kinachokwenda kinyume na maadili yanayokubalika” kitaadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Mwaka 2014, ufalme wa nchi hiyo, uliidhinisha sheria ambazo, kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch, zinatafsiri “kitendo chochote cha kutoa maoni yoyote huru kuwa ni ugaidi” na kutoa adhabu kali. Ibara ya 1 ya sheria hiyo inatoa tafsiri sahihi ya maana ya ugaidi:

“Kutangaza kwa namna yoyote ile mawazo yenye kukana uwepo wa Mungu, au kuhoji hadharani misingi ya dini ya ki-Islam ambayo ndiyo nguzo ya nchi hii.”

Mwezi Mei 2014, mahakama ya jinai mjini Jeddah ilimhukumu mwanablogu Raif Badawi kifungo cha miaka 10 jela na viboko 1,000 kwa ‘kukashifu Uislamu”. Badawi alihukumiwa kwa kujaribu kujenga jamii wa “Wasaudi Arabia Wanaoshabikia Mabadiliko”, jukwaa la mtandaoni lililoanzishwa mwaka 2008 kuendesha mijadala ya nafasi ya dini nchini humo.
Badawi akiwa na umri wa miaka 32 wakati huo aliamuriwa kulipa faini ya Riyali milioni moja (takribani dola za kimarekani 266,600). Pamoja na kampeni ya kimataifa inayodai kuachiwa huru kwake, Badawi bado anasota jela hadi leo. Mwezi Januari 2015, alichapwa viboko 50 kati ya 1,000 alivyohukumiwa. Awamu ya pili ya zoezi la kumchapa imeahirishwa kwa muda ufuatia kuzorota kwa afya ya Badawi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.