- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Magazeti Nchini Iran Yabaini Udhalilishaji na Unyanyasaji wa Wanafunzi wa Afghanistan

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Iran, Haki za Binadamu, Uandishi wa Habari za Kiraia, Vyombo na Uandishi wa Habari, Wakimbizi
Afghan school children in Iran have been the subject of abuse and mistreatment. Photo from ICHRI and used with permission. [1]

Watoto wa Afghanistan wanaosoma nchini Iran wanakabiliwa na udhalilishwaji na unyanyaswaji. Picha kutoka ICHRI na imetumiwa kwa ruhusa.

Mnamo Januari 5, 2016 gazeti la Shargh [2] lilitaarifu kuwa, mkuu wa shule huko Damavand aliwapiga wanafunzi wadogo raia wa Afghanistan kwa kutumia mpira wa kupitishia vitu kama maji na kuacha alama kwenye nyuso na miili yao, huku akiwaambia, “Ninyi raia wa Afghanistani, mnatakiwa kuondoka. Mpo wengi sana” Wanafunzi wa Afghanistan wanakabiliana na udhalilishaji kimwili pamoja na kunyanyapaliwa katika shule nyingi za nchini Iran, hii ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran na kwamba serikali imekuwa ikijaribu kuficha matukio haya.
“Kwa ujumla, habari kuhusu kuonewa kwa wanafunzi, na hususani wanafunzi raia wa Afghanistan, huwa zinaonekana kwa bahati sana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa mamlaka za ufuatiliaji na Wizara ya Elimu imejaribu kufifisha matukio haya,” Shirzad Abdollahi, ambaye ni mtaalam wa masuala ya elimu nchini Iran aliiambia asasi ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Binadamu ya nchini Iran.

Nchini Iran kuna kambi ya wakimbizi inayoaminika kuwa ni moja ya kambi zenye idadi kubwa ya wakimbizi ambapo raia 950, 000 wa Afghanistan walijiandikisha kwa mwaka 2015, hii ni kwa mujibu wa Kamishana wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia wakimbizi [3] (UNHCR).

Uonevu dhidi ya watoto wa Afghanistan mashuleni, bila kujali kama ni wa kudhuru mwili, maneno ya uonevu au udhalilishaji, kwa mujibu wa Abdollahi, mambo haya yamezoeleka nchini Iran, hata hivyo, hali ni mbaya sana kwa raia wa afghanistan ambao wana watu wachache wa kuwatetea. Wakati wa Kampeni ya kutetea haki za binadamu, Abdollahi aliweka bayana kuwa mamlaka za elimu zinajaribu kufuatilia matukio haya bila ya kuwawajibisha wahusika, na pia wanajaribu kuficha matukio haya yasiandikwe au kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Watoto wengi wa Afghanistan wasiofahamika pia wanakabiliwa na vikwazo vya kiukiritimba vinavyowakosesha fursa ya kupata elimu, jambo ambalo ni kinyume na haki ya Kimataifa ya kuhakikisha kila mtu anapata elimu.

Mwanafunzi wa Afghanistan kutoka katika jiji la Pakdasht alipigwa na kufukuzwa shule kwa kushindwa kulipa ada ya masomo, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa mapema tarehe 16 Januari 2016 kwenye gazeti la Vaghaye Ettefaghieh [4].

Wazazi walikuwa na uwezo wa kutoa fedha za Iran, riali milioni moja (sawa na dola za Marekani 33) kati ya riali milioni 2.3 (sawa na dola za Marekani 76) zilizopaswa kulipwa shuleni hapo. Mwanafunzi huyu aliambiwa asirudi shuleni hadi hapo kiasi chote cha fedha kitakapolipwa.

Kufuatia tukio la Damavand la mwezi Januari, mmoja wa wazazi alizungumza na gazeti la Sharg na kusema,

Tulipeleka malalamiko yetu kwa uongozi wa elimu hali iliyopelekea kutumwa kwa mtu wa kuchunguza shule iliyohusika. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi, mkuu wa shule alitueleza kuwa haikuwa vyema kuchukua hatua za juu namna ile… Alisema kuwa, watoto wetu walikuwa wakipiga kelele kiasi cha kumfanya mkuu wa shule kujawa na hasira.

Mwaka uliopita, mwalimu mmoja wa shule moja iliyopo Pakdasht aliwaadhibu watoto wanne raia wa Afghanistan waliokuwa wakisoma shule ya msingi kwa kuwalazimisha kushika uchafu chooni, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Februari 10, 2015 ya gazeti la Tabnak [5].

Kwenye kampeni ya kutetea haki za binadamu, Abdollahi alisema, “Udhalilishaji wa wanafunzi raia wa Afghanistan siyo wa mfumo mzima wa elimu, bali umekithiri mashuleni kulingana na mtazamo binafsi wa wakuu wa shule na walimu”.

Abdollahi aliongeza kuwa, walimu na viongozi hawana mafunzo ya kutosha kuhusiana na haki za watoto.

Kwa sasa, kunahitajika ufuatiliaji wa karibu wa wakuu wa shule na walimu na pia, ukiukwaji wowote wa haki za watoto ushughulikiwe barabara. Walimu waungwana ambao ni wachache sana wasiwavumilie walimu wanaoendekeza unyanyasaji. Vyombo vya habari pia havina budi kuimarisha uelewa wa watu kuhusu haki za watoto na pia kuifanya jamii kuwa na uelewa zaidi kuhusu uonevu dhidi ya wanafunzi.

“Hakuna matamko rasmi ya serikali yanayokemea uonevu dhidi ya wanafunzi wa Afghanistan. Tatizo ni mtazamo walionao wanajamii,” Abdollahi aliweka bayana wakati wa kampeni.

“Miaka michache iliyopita, kundi la familia kadhaa katika halmashauri ya Kan, Tehran, waliandamana mbele ya shule iliyopo jirani na makazi yao wakishinikiza wanafunzi wa Afghanistan wasijiunge na shule hiyo” Abdollahi alisema.

Mbali na uonevu wa kimwili na udhalilishaji, wanafunzi raia wa Afghanistan wanakabiliwa pia na hatari ya kukosa mahitaji ya msingi kwani wazazi wao, wengi wao wakiwa ni wakimbizi, kwa kawaida hupata ujira mdogo kuliko raia wa kawaida wa Iran.

“Tangu mwaka jana, suala la ada ya shule kwa kiasi fulani lilitatuliwa kwani shule haziwatozi tena ada wanafunzi raia wa Afghanistan,” alisema Abdollahi. “Wanaweza kuombwa kuchangia michango ya hiari kwa ajili ya matumizi fulani ya shule, lakini hata hivyo, haijawekwa wazi ni michango gani ni ya lazima na ipi isiyo ya lazima.”

“Hata hivyo, kanuni zinasema kuwa Wanafunzi raia wa Afghanistan wana haki sawa na wanafunzi wenzao wa Iran na hakuna yeyote aliye na mamlaka ya kuwadhalilisha,” alisema Abdollahi.

Mwaka 2011, Naibu Waziri wa elimu, Masuala ya Kimataifa, alitangaza [6] kuwa, wanafunzi wa kigeni wamezuiwa kujiunga na shule za vipaji maalum, pamoja na shule za serikali za kupigiwa mfano na shule za ufundi, hali ambayo ni ukiukwaji wa haki ya kimataifa ya kupata elimu ya juu.

“Sera za elimu hazipaswi kubadilishwa mara kwa mara kwa kuzingatia matakwa ya mtu binafsi au uongozi ulipo madarakani. Elimu ni haki ya mtoto inayotambuliwa bila kujali uraia, ukabila, sehemu unayoishi au uwezo wa kifedha,” Abdollahi alitanabaisha wakati wa kampeni.

“Haki hii haina budi kuheshimiwa kwa dhati kabisa bila ya kikwazo chochote kutokana na kubadilishwa kwa serikali au sera,” alisema Abdollahi.