Mitaa ya Paris Inavyonikumbusha Mitaa ya Beirut

Meme widely shared in solidarity with the victims of the Paris attacks.

Picha zinazozunguka mitandaoni kuwafariji wahanga wa shambulio la Paris.

Ninatoka katika jamii iliyoendelea kidogo pale Lebanon. Kwa kuwa lugha yetu ni Kifaransa, nimejikuta nikiiona nchi ya Ufaransa kama nyumbani kwetu. Mitaa ya Ufaransa ninaifahamu sana kama ninavyoifahamu Beirut. Nilikuwa Paris siku chache tu zilizopita.

Siku mbili hizi zimekuwa za kutisha sana. Siku ya kwanza ilishuhudia vifo vya watu zaidi ya 40 mjini Beirut; usiku wa siku ya pili maisha ya zaidi ya watu 120 jijini Paris yalikatishwa.

Kwangu, inaonekana wazi kwamba kwa dunia yetu, vifo vya watu mjini Beirut havijagusa hisia za watu kama ilivyotokea kwa vifo vilivyotokea jijini Paris.

Hatujapata kile kitufe cha ‘salama’ kwenye mtandao wa Facebook. Hatujapata salamu za pole zilizotolewa usiku wa manane kutoka kwa watu maarufu zaidi duniani pamoja na mamilioni ya watumiaji wa mtandao.

Hatukubadilisha sera zitakazoathiri maisha ya wakimbizi wasio na hatia ambao idadi yao haifahamiki.

Hali hii haieleweki kabisa.

Ninayasema haya bila chuki wala hasira yoyote, isipokuwa huzuni.

Ni vigumu kuelewa kwamba kwa yote yaliyosemwa, kwa maneno matupu tuliyoweza kuyatamka kwa jina la ‘mshikamano na wahanga’, wengi wetu tulio binadamu kama wengine tunatengwa na kelele hizi hewa za mshikamano wa kile kinachoitwa ‘dunia’.

Natambua kwa kutumia neno ‘dunia’, mimi mwenyewe ninabagua sehemu kubwa sana ya dunia. Kwa sababu huo ndio muundo wa wenye nguvu unavyofanya kazi.

Sina thamani.

‘Mwili’ wangu hauna thamani kwa ‘dunia’.

Nikifa, hakuna anayejali.

Narudia, siyasemi haya kwa chuki na hasira.

Sentensi hii ni ukweli uliodhahiri. Ni ukweli wa kisiasa, uhalisia, lakini ndio ukweli wenyewe.

Labda nijikaze niwe na hisia fulani ndani yangu, lakini nimechoka. Ni jambo zito sana kulitambua.

Ninafahamu kwamba nina bahati sana kwamba nikifa, nitakumbukwa na marafiki na wapendwa wangu. Huenda blogu yangu na ninayoyaandika mitandaoni yanaweza kuwafanya baadhi ya watu wakatafakari maneno yangu. Huo ndio uzuri wa mtandao wa intaneti. Lakini mtandao unatumika na wachache sana. Wengi ‘duniani’ hawaufahamu.

Sikuwahi kuelewa vizuri Ta-Nehisi Coates alimaanisha nini alipoandika kuhusu Mwili Mweusi nchini Marekani [Black Body in America]. Nadhani tunaweza kupanua simulizi hiyo na kuwa Mwili wa Kiarabu pia. Mwili wa Mmarekani Mzawa. Mwili wa Mhindi Mwekundu. Mwili wa Mwamerika Kusini. Mwili wa Mhindi. Mwili wa Mkurdi. Mwili wa Mpakistani. Mwili wa Mchina. Na miili mingine mingi.

Mwili wa Binadamu unatofautiana. Kwa hakika inaonekana hivyo kwa sasa. Labda kufanana kwa miili ni ndoto. Lakini huenda ni ndoto inayohitaji kutunzwa kwa sababu bila hata hisia hizi hewa za mshikamano kwa sehemu ya viungo vya mwili, sina hakika ni dunia ya aina gani tungekuwa tunaishi sasa hivi.

Miili mingine ni ya kidunia, lakini miili mingine inayahusu maeneo husika, nchi husika, na baadhi ya makabila pekee.

Ninasikitika sana pamoja na wahanga wa mashambulio ya kinyama ya leo na jana, na ninasikitika na wale wote wanaathirika na ubaguzi mbaya sana unaotokana na matendo ya wauaji wa halaiki na kushindwa kwa sisi wanadamu kujiona kwa utambulisho mmoja.

Tumaini langu pekee ni kwamba tunaweza kuwa imara kiasi cha kutoa majibu yaliyo kinyume na yale yaliyotarajiwa na wahalifu wa mashambulizi haya. Nina matumaini mengi kiasi cha kusema kwamba tunaelekea huko, bila kujali ‘huko’ ni wapi.

Tunahitaji kuzungumzia masuala haya. Tunahitaji kuzungumzia kuhusu rangi za watu. Tunalazimika.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.