- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Mwanafunzi wa Irani ‘Awekwa Ndani’ kwa Sababu ya Anayoyaandika Facebook

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Iran, Censorship, Haki za Binadamu, Maandamano, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, GV Utetezi
Amin Anvary's mother has been protesting for her son's release since October. Image from ICHRI.

Mama yake Amin Anvary Farah Bakhshi akidai kuachiwa huru kwa mwanae. Picha: ICHRI.

Mwanaharakati mwanafunzi Amin Anvari [1], 21, aliyesamehewa kifungo cha awali mapema mwaka huu kwa sababu ya maandishi yake kwenye mtandao wa Facebook yanayopigania uhuru wa kiraia, amekamatwa tena bila kushtakiwa kwenye gereza la Evin, kitendo kilichofanywa na Walinzi wa Mapinduzi ya Irani tangu Oktoba 4, 2015. Kwa mujibu nwa mwanafamilia, kijana huyo amekuwa akishinikizwa kukiri uongo.

“Wanatutisha na kutubughudhi kama mbinu ya kumshinikiza Amin huko jela. Nina uhakika na hilo. Wanataka akubali kukiri uongo,” mama wa Amin Anvari, Farah Bakhshi, aliuambia Mtandao wa Kimataifa wa Kutetea Haki za Binadamu nchini Irani.

Amin Anvari alimatwa kwa mara ya kwanza Desemba 30, 2014, kwa sababu ya kuandika masuala yanayohusu haki za msingi za raia kwenye mtandao wa Facebook. Aliachiliwa huru siku hiyo hiyo kwa dhamana ya riali milioni 300 (sawa na dola za Marekani 10,000). Mwezi Julai, 2015, alisomewa mashitaka kwenye Mahakama ya Kimapinduzi ya Kiislamu iliyokuwa inaongozwa na Jaji Ahmadzadeh na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa “kuendesha propaganda dhidi ya serikali,” “kumtukana Kiongozi Mkuu wa nchi,” na “Kumtukana Mohammad Taghi Mesbagh Yazdi”, ambaye ni mwanachama wa Baraza la Wataalam. Hata hivyo, hukumu hiyo iliahirishwa kwa miaka mitano.

Bi. Bakhshi anakumbuka kwamba kijana wake huyo Amin alikamatwa tena mnamo Oktoba 4 na watu wanne waliovamia nyumba yake bila kuonesha vitambulisho wala hati yoyote na kuchukua kompyuta za kijana huyo. Tangu wakati huo mama huyo ameweza kuongea na kijana wake mara nne tu kwa simu. Yeye, mume wake, na mtoto wao mdogo wamekuwa wakisumbuliwa na kuonywa wasithubutu kuongea na waandishi kuhusiana na kukamatwa kwa Amin.

“Chochote kitakachowakuta wanangu hawa wawili, mimi na mume wangu kitahusiana moja kwa moja na Walinzi wa Mapinduzi. Wanatutisha sana ili tusipinge jambo hilo wala kukubali kuhojiwa na waandishi. Lakini sina jinsi. Mnataka nisihojiwe? Nawaombeni kwa jina la Mwenyezi Mungu mwachieni mwanangu na nitakaa kimya,” alisema Bi. Bakhshi.

Bi. Bakhshi aliuambia mtandao huo namna afisa mmoja wa serikali kwenye gereza la Evin alivyojaribu kumwekea shinikizo la kutokuongea na vyombo vya habari:

Aliniambia ataniruhusu kumwona kijana wangu kama nitamhakikishia kuwa sitaongea na waandishi wala kuandamana. Nikamwambia ningekubali, kama angeniahidi kumwachia mwanangu. Alikataa, na nikamwambia, ‘kama ni hivyo, nitaendelea kufanya kile ninachokifanya.’

Mama wa Amin Anvari aliongeza kwamba amekuwa kimya kwa majuma mawili baada ya kukamatwa kwa kijana wake. Lakini ilipofika Oktoba 19, alishiriki maandamano yaliyoratibiwa na kikundi cha familia za wafungwa. “Siku hiyo hiyo Amin alitupigia simu nyumbani na kuongea na baba yake akamwambia alikuwa mzima na kusema, ‘Mwambie mama asiongee na waandishi kwa sababu itaniletea matatizo [kwenye kesi yake’.”

Bi. Bakhshi alisema wakati wa ziara ya kifamilia ya majira ya joto walioifanya nchini Uturuki waligundua kwamba baadhi ya marafiki wa Amin walikuwa wamekamatwa. Alimwambia asirudi Irani kama alihisi angepata matatizo. Lakini anasema hakufanya makosa yoyote na alitaka kurudi kuendelea na masomo yake ya Chuo Kikuu, Bi. Bakhshi aliongeza.

“Wito wangu kwa maafisa wa mahakama ni kwamba wasiwakamate vijana na kuwapa hukumu kubwa kila wanapokosoa. Kijana wangu alitakiwa awe darasani anasoma hivi sasa.”