Katika tangazo lililotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iran, serikali ya Iran itawaingiza wakimbizi wote walioandikishwa kwenye Mpango wake wa Bima ya Salamat. Mpango huu ni ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya ndani, inayoshughulika na masuala ya wahamiaji, Shirika la Bima ya Afya la Irani na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR). Mpango huu unawalenga wakimbizi wote raia wa Afrghastani na Iraq wanaoishi Irani.
Gazeti la kila siku la Kiingereza nchini Iran Tehran Times, ambalo ni sehemu Shirika la Habari la Mehr linalomilikiwa na Shirika la Kueneza Itikadi ya Kiislamu [IIDO], lilieleza shukrani za Sivanka Dhanapala, ambaye ni mwakilishi wa UNHCR nchini humo, kwa mradi huo:
Mwailishi wa UNHCR nchini Iran akiushukuru mchango wa serikali ya Irani, alionesha shukrani za UNHCR kwa serikali ya Jamhuri ya Kiislam ya Irani kwa huduma zote ilizozitoa kwa wakimbizi wanaoishi mijini nchini humo, ambao ni idadi kubwa zaidi duniani, katika kipindi cha miongo mitatu, na kuwaingiza wakimbizi kwenye Mpango wa Bima ya Afya, ambao ni mfano mzuri duniani, na kuongeza kwambahuduma kama hizo hazijatolewa kabla na ninaamini kwa dhati kwamba nchi nyingine zitafuata mfano huu.
Nusu ya gharama za mpango huo zitatoka kwa serikali ya Irani, wakati UNHCR itachangia dola za ki-Marekani milioni 8.3. Mpango huu utawanufaisha wakimbizi zote walioandikishwa, ambao watapata huduma za bima ya afya kwa ‘kulazwa na matibabu’, kama ilivyo kwa raia wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa tovuti ya UNHCR, Irani inahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Wakimbizi wenye asili ya Afghanistani inakaribia milioni 1, huku ikiaminika kwamba kuna wakimbizi wasioandikishwa wanaokadiriwa kuwa kati ya milioni 1.4 na 2 wanaoishi na kufanya kazi zao nchini humo.
Hatua ya serikali ya Irani kutoa huduma hizi kwa wakimbizi imekosolewa sana, hata hivyo, ripoti ya mwaka 2013 Shirika la Haki za Binadamu iliyoonesha kwamba wakimbizi wa Afghanistani walikuwa wakitendewa uonevu na wakati mwingine kunyanyaswa na wananchi wa Irani na serikali.
Kwa makadirio ya 2015, Shirika la UNHCR lilionesha matarajio yake kwa mpango huo mahsusi kwa wakimbizi wa Afghani, Iraq na Pakistani kama inavyooneshwa kwenye picha ifuatayo.
Irani imekuwa ikikosolewa kwa kutokuwapokea wakimbizi wa Syria wakati wote wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Haya yanatokea wakati ambao nchi hiyo inajihusisha mno na mgogoro wa Syria kama mshirika na mwuungaji mkono mkuu wa Rais wa Syria Rais Bashar Al-Assad.
Kwa hakika, maendeleo haya katika kuboresha huduma za afya kwa wakimbizi ni mafanikio makubwa kwa nchi ya Irani na eneo hilo zima. Irani inaweza, hata hivyo, kuboresha taswira yake katika kuchukua hatua za kushughulikia mgogoro wa wakimbizi wa nchi jirani ya Syria.