GV Face: Kuhusu Beirut na Paris, Kwa nini Majanga Mengine Yanatangazwa Zaidi Kuliko Mengine?


‘Kwa nini maiti nyingine ni mali ya dunia nzima, wakati maiti nyingine ni za maeneo husika pekee?’

Katika toleo hili la mazungumzo ya GV, mfululizo wa soga za Global Voices, Joey Ayoub, mwanablogu wa ki-Lebanoni na mwandishi wa Global Voices, Lova Rakotomalala, mhariri wa lugha ya Kifaransa anayeishi Paris na Laura Vidal, kiongozi wa jumuiya ya Amerika Kusini anayeishi Paris watazungumzia rangi, siasa za vifo na miitikio isiyo na usawa yanapotokea majanga duniani kote.

Global Voices ni jamii isiyo na mipaka, kwa sehemu kubwa jumuiya ya watu wanaojitolea yenye waandishi, wachambuzi, wataalamu wa uandishi wa mtandaoni na wafasiri wapatao 1400. Tunaanzisha mijadala ya kihabari inayojenga madaraja, uelewa wa masuala ya kidunia na mahusiano ya kirafiki. Tunalenga kusimulia habari za jamii zinazopuuzwa na zinazopuuzwa. Timu ya wahariri na waandishi wenye weledi —watu kama Joey, Laura, na Lova — wanaandika kutoka katika nchi 167 duniani kote. Watafsiri wetu wanahakikisha kwamba habari hizo zinapatika katika lugha 35. Wengi wa wanachama wetu wanazungumza luga zaidi ya moja na wanaishi zaidi ya mji au nchi moja.

Baada ya mashambulio ya Paris mnamo Novemba 13, Joey ameandika makala yenye kichwa cha habari,  “Mitaa ya Paris Inavyonikumbusha Mitaa ya Beirut “, ambayo imesomwa sana mtandaoni:

Ninatoka katika jamii iliyoendelea kidogo pale Lebanon. Kwa kuwa lugha yetu ni Kifaransa, nimejikuta nikiiona nchi ya Ufaransa kama nyumbani kwetu. Mitaa ya Ufaransa ninaifahamu sana kama ninavyoifahamu Beirut. Nilikuwa Paris siku chache tu zilizopita.

Siku mbili hizi zimekuwa za kutisha sana. Siku ya kwanza ilishuhudia vifo vya watu zaidi ya 40 mjini Beirut; usiku wa siku ya pili maisha ya zaidi ya watu 120 jijini Paris yalikatishwa.

Kwangu, inaonekana wazi kwamba kwa dunia yetu, vifo vya watu mjini Beirut havijagusa hisia za watu kama ilivyotokea kwa vifo vilivyotokea jijini Paris.

Hatujapata kile kitufe cha ‘salama’ kwenye mtandao wa Facebook. Hatujapata salamu za pole zilizotolewa usiku wa manane kutoka kwa watu maarufu zaidi duniani pamoja na mamilioni ya watumiaji wa mtandao.

Hatukubadilisha sera zitakazoathiri maisha ya wakimbizi wasio na hatia ambao idadi yao haifahamiki.

Hali hii haieleweki kabisa.

Ninayasema haya bila chuki wala hasira yoyote, isipokuwa huzuni.

Laura Vidal alikuwa baa mtaa wa pili na eneo ambalo mashambulizi yalitokea. Laura alihamia Paris miaka saba iliyopita akitokea Venezueelza kama mwanafunzi. Kwenye makala ya, “Baada ya Mashambuzi la Paris: Ili Uwe Mshikamano Kweli, Haupaswi Kuwa Nusunusu “, anaandika:

Tangu nimefika Paris, nimefutilia mijadala mingi sana kuhusiana na masuala ya asili ya mtu, rangi ya ngozi, historia ya mtu na imani za kidini. Sehemu ya utafiti wangu imejikita kwenye -mada ya ajabu kabisa- uelewa wa tamaduni za wengine. Mazungumzo haya yamejaa hisia, kwa hiyo wakati mwingine yanafanya watu wajisikie vibaya. hata hivyo, mijadala hiyo ni ya muhimu. Na nayasema haya kwa sababu inavyoonekana kuigawa dunia kwa maneno kama “sisi” na “wao” hayatusaidii. Na haiwezi kuwa hivyo. Kwa hakika, tofauti hizi zinazotengenezwa ndizo zinazoharibu mambo. Na hivyo ndivyo tunavyojifunza kujiona kama “sisi” na “wengine”, na tunajifunza historia na kutazama taarifa za habari kwa jicho hili. “Sisi” na “wao”. “Hapa” na “mbali”. Sidhani kama tunaweza kuendeleza mtazamo kama huu kwa muda mrefu -labda tuliweza kabla- na kuendea kuukana ukweli wa mambo.

Andiko la Lova, “Kujenga Uandishi wa Kujali Wengine Moja Baada ya Nyingine“, iliyochapishwa baada ya shambuzi la Charlie Hebdo, aliyoiandika kwa kushirkiana na mwandishi wa Naijeria Nwachukwu Egbunike:

Wakati wa kufanya mijadala ya maana kidunia kuhusu mashambulizi ya kigaidi, uhuru wa kujieleza, kujali wengine na Hofu ya Uislamu sio pale majanga yanapotokea lakini kabla, tena yapaswa kuwa wakati vichwa vyetu vimetulia.

Hata hivyo, tupende tusipende, kiu ya umma kujaribu kuulewa ulimwengu ni kubwa pale matukio mabaya yanapotokea. Wakati muafaka unaweza usiwepo, lakini tunayo fursa, kama waandishi wa habari kutengeneza aina ya mijadala yenye tija kwa maelfu ya wasomaji wetu duniani kote, hasa pale wanapokuwa wanafuatilia kwa makini.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.