- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Kampeni ya ‘Alaa Aachiwe’ Yashika Kasi Mwaka Mmoja Baada ya Kufungwa Kwake

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Misri, Habari za Hivi Punde, Haki za Binadamu, Harakati za Mtandaoni, Maandamano, Sheria, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, GV Utetezi
Friends and supporters changed their avatars on social media to this Free Alaa poster today to protest the first anniversary of his unfair imprisonment

Katika kuadhimisha mwaka mmoja baada ya kufungwa kiuonevu kwa Alaa, marafiki na watetezi wake walibadili picha zao za wasifu kwenye mitandao ya kijamii na kuweka mabango ya ‘Alaa aachiwe huru’

Mwaka mmoja umepita tangu mwanablogu wa ki-Misri Alaa Abdel Fattah, mtu muhimu katika mapinduzi yaliyoendelea nchini Misri, ahukumiwe kifungo kwa sababu tu ya uanaharakati wake. Alaa alihukumiwa kifungo cha miaka mitano [1] kwa kudaiwa kushiriki maandamano na “kumtukana polisi na kumwibia redio ya upepo”. Alitozwa faini ya paundi za Misri 100,000 (sawa na dola 13,000 za Marekani). Katika kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufungwa kwake, katika majukwaa ya kijamii, watumiaji wa mtandao duniani kote walibadili picha zao za wasifu na kutumia picha ya Abd El Fattah ili kuongeza uelewa wa watu kuhusu masaibu ya Alaa pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa nchini Misri.

Abd El Fattah ni mmoja wapo wa washitakiwa 25 katika kile kilichokuja kujulikana kama kesi ya Baraza la Shura. Alikuwa wa kwanza kukamatwa mnamo Novemba 28, 2013. Mwezi Juni mwaka jana, alihukumiwa miaka 15 jela bila kuwepo mahakamani na aliamuriwa kulipa faini ya paundi 100,000 za Misri baada ya kushitakiwa [2] kwa kosa la kumshambulia ofisa wa polisi na kukiuka sheria ya kuandamana ya 2013 [3] inayozuia maandamano yasiyoruhusiwa. Kwa mujibu wa tovuti ya Mada Masr, iliyonukuu kutoka kwenye tovuti inayomilikiwa na Ahram Gate, watuhumiwa hao wanadaiwa [4]: “kuandaa maandamano haramu nje ya jengo la Baraza la Shura jijini Cairo, kumshambulia afisa wa polisi, kuiba radio ya upepo, uhuni, ghadhabu dhidi ya maafisa wa polisi, kufunga barabara, kujaza watu kwenye maeneo ya umma na kuharibu mali ya umma.”

Baada ya rufaa iliyokatwa na wanasheria wake, kesi ya Abd El Fattah ilisikilizwa upya mnamo Agosti 2014. Ilipofika Septemba 15, 2014, jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alimhukumu tena [5] baada ya tukio la juma lililotangulia kesi hiyo, ambako mwendesha mashitaka alionesha video ikimwonesha Manal Hassan, mke wa Abd El Fattah, akicheza dansi. Video hiyo iliyokuwa imechukuliwa kutoka kwenye kompyuta ya Hassan, iliyokuwa imechukuliwa na polisi mara baada ya Abd El Fattah kuwekwa chini ya ulinzi na kuondolewa kwenye familia yake mwezi Novemba 2013, video hiyo haioneshi uhusiano na shughuli zozote za kisiasa.

Sekeseke hilo lilimalizika Februari 23, 2015, ambako jaji mpya alimhukumu kifungo cha miaka mitano Abd El Fattah na mwenzake aitwaye Ahmed Abdel Rahman, aliyekuwa anapita wakati wa maandamano, na aliwekwa chini ya ulinzi sambamba na Abdel Fattah, na alikuwa anawasaidia wasichana kadhaa waliokuwa wakibughudhiwa na polisi. Abdel Rahman aliamriwa kulipa kiwango kile kile cha faini. Washitakiwa wengine kumi na nane walihukumiwa miaka mitatu jela na miaka mitatu mingine ya uangalizi, mbali na kiwango kile kile cha faini.

Zaidi ya kubadili picha zao mtandaoni kwa ajili ya siku hiyo, watumiaji wa mtandao wanaomwunga mkono walitumiana nukuu na twiti za Abd El Fattah. Shangazai yake, mwandishi maarufu wa riwaya Ahdaf Soueif alitafsiri baadhi ya nukuu na twiti hizo hapa:

Mimi ni Alaa. Ninajivunia kufanya kile ninachoweza kukifanya ; wakati mwingine ninashangaa kwa kile ninachoweza kufanya…

Kesho tutatengeneza suluhisho bila kufungana jela. Kesho ni mali yetu

Mwanablogu wa ki-Lebanoni Abir Ghattas, ambaye ni mwandishi wa Global Voices, anayo nukuu nyingine:

Siwezi kamwe kuwa msaliti

Nukuu nyingine inayoelezea msimamo wa Abd El Fattah kuhusu kufungwa kwake:

Kila ninapofungwa, sehemu yangu inamomonyoka

Kampeni hiyo ilipata mwitikio kutoka duniani kote, kwa sababu Abd El Fattah alikuwa mwanablogu, mwanaharakati na mtengeneza programu anayeheshimika duniani kote.

Mtaalam wa usalama wa mtandao Jacob Appelbaum alitwiti:

Kila siku, ninamfikiria Alaa Abdel fattah na wengine waliofungwa isivyo haki nchini Misri

Muasisi wa Global Voices Online Ethan Zuckerman alikuwa na maoni yafuatayo:

Mwaka mmoja akiwa gerezani kwa kuandaa maandamano ni mwaka mrefu sana

Na Ahmed Abdel Rahman ahakusahaulika. Wengi wali-twiti namna maisha ya mpita njia yalivyoharibiwa kwenye tukio hili. Hend Nafea anaeleza:

Ahmed Abdel-Rahman amekuwa kizuizini kwa mwaka mmoja leo kwa sababu tu alisaidia kuwalinda wanawake dhidi ya udhalilishaji wa polisi

Omar Robert Hamilton anatukumbusha kwa nini kampeni hii ina umuhimu mkubwa:

Twiti moja haina nguvu. Lakini mamilioni ya twiti yanaweza kutikisa dunia. Alaa anaamini katika nguvu ya mawasiliano na kwa hivyo, leo, ni lazima tufanye hivyo.

Anaeleza:

Tangu Novemba 2013 Alaa ametumia siku 575 gerezani. Bado ana miaka minne ya kifungo. Kosa lake: Kuandamana

Na Rasha Abdulla, mwanaharakati wa uhuru wa kujieleza nchini Misri, anaongeza:

Alaa si gereza pekee la dhamira. Tunataka uhuru wake na kwa wote.

Mapema leo, familia ya Abd El Fattah ilifanya maandamano mitaani, ambapo walisimama mbele ya Makazi ya Rais pale Ittihadeya kupinga kufungwa kwa wanaharakati –na wafungwa wengine wa kisiasa kwenye kesi hiyo:

Picha nyingine kutoka kwenye Makazi ya Rais ambapo familia ya Alaa ilipinga kufungwa kwake.

Mama yake Alaa, Leila Soueif, anaonekana, kulia, akibeba bango lenye majina ya wafungwa wanne wanaotumikia vifungo vyao kwa sababu ya kesi ya Shura. Zaidi ya Alaa na Ahmed Abdelrahman, Abdelrahman ElSayed na Abdelrahman Tarek nao pia wamefungwa. Pamoja na msamaha wa rais wa kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa, wafungwa hawa hawakuachiliwa huru.

Katika video ifuatayo, Soueif, ambaye ni mwanaharakati, anasema wamekuwa wakisimama kwa saa moja wakiwakumbusha watu kuhusu Alaa na Ahmed Abdelrahman, ambao wamekuwa jela baada ya kuhukumiwa kifungo katika kesi ya Shura.

Anaeleza:

Ni kweli, mashitaka hayo yalikuwa kichekesho na yalisahalika kwenye msamaha wa rais. Kwa hiyo tuna vijana wanne kwenye kesi ya Shura ambao hawajaufaika na msamaha wa rais. Tunao maelfu wa mahabusu lakini leo tunamwongelea Alaa na Ahmed Abdelrahman ambao wametumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Na hapa, dada yake Mona Seif, ambaye ni mwanaharakati, anabeba bango linalosomeka: “Bado kuna wafungwa wengi walioonewa. Uhuru kwa wafungwa”:

Bado kuna wafungwa wengi walioonewa. Uhuru kwa wafungwa

Jijini Cairo, mabango yanayotoa wito wa wafungwa wengine wanne wa kisiasa waliobaki katika kesi ya Baraza la Shura ambao hawapewa msamaha. Dada yake Abd El Fattah, Sanaa Seif, ambaye pia ni mwanaharakati ambaye alifungwa kwa kushiriki maandamano, anaweka picha za baadhi ya mabango kwenye ukurasa wake wa Facebook [30]:

Posters calling for the release of the remaining four remaining political detainees from the Shura Council case who were not included in a presidential pardon popped up across Cairo today. Photo credit: Sanaa Seif (Facebook) [30]

Mabango yakitoa wito wa kuachiliwa kwa wafungwa wanne wa kisiasa waliobaki katika kesi ya Baraza la Shura ambao hawakupata msamaha warais uliotangazwa jijini Cairo leo. Picha imepigwa na Sanaa Seif [30] (Facebook)

Kwa maoni zaidi, pitia mkusanyika huu wa Storify [31], ulioandaliwa na APC.

Chombo Huru cha Habari Mada Masr pia kina habari za Kiingereza zilizotafsiriwa kutoka kwenye makala za hivi karibuni za Alaa hapa [32].