- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Filamu ya Difret Inayosimulia Mila ya ‘Kumteka’ Mwanamke Kulazimisha Ndoa Nchini Ethiopia

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ethiopia, Sanaa na Utamaduni, Sheria, Uandishi wa Habari za Kiraia, Wanawake na Jinsia
Tizita Hagere (right) plays the role of 14-year-old Hirut Assefa in 'Difret.' Credit: Truth Aid Media.

Tizita Hagere (kulia) akicheza nafasi ya Hirut Assefa mwenye umri wa miaka 14 kwenye filamu ya ‘Difret.’ Haki Miliki: Truth Aid Media.

Makala haya pamoja na taarifa ya redioni yameandaliwa na Joyce Hackel [1] akishirikiana na Julia Barton [2] kwa ajili ya kipindi cha The World [3] kilichosikika awali kwenye tovuti ya PRI.org [4] mnamo Oktoba 22, 2015, na imechapishwa tena hapa kama sehemu ya makubaliano ya kushirikiana maudhui.

Neno “Difret” lina maana nyingi katika lugha ya ki-Amariki inazungumzwa nchini Ethiopia: linaweza kumaanisha ‘kuthubutu’ na ‘kuwa na ujasiri,’ lakini vile vile laweza kuwa na maana ya ‘kufanyiwa ukatili.’

Kama lilivyo jina lake, filamu ya “Difret [5]” inawakilisha masuala mengi: ni kazi ya sanaa inayosimulia mkasa wa kweli unaohusu ujasiri na mabadiliko yanayoongozwa na msichana; ni filamu pekee iliyoandaliwa nchini Ethiopia kwa picha ya milimeta 35l na tayari imepata heshima kubwa kwa kuandaliwa na mtayarishaji maarufu wa filamu, Angelina Jolie Pitt. Lakini zaidi ya yote, filamu hiyo inasimulia mila za ndoa za asili nchini Ethiopia kwa kutumia mkasa wa kweli uliompata msichana mmoja nchini humo.

Filamu ya “Difret” inajenga masimulizi yake kwenye tukio la Aberash Bekele — anayetumia jina la Hirut kwenye filamu — msichana aliyekamatwa na wanaume na kutoroshwa kijijini kwa kutumia farasi ili akaolewe. Wakati anatekwa na wanaume hao, msichana huyo alikuwa ndio kwanza ameingia darasa la tano shuleni kwake. Mwanaume aliyemteka -aliyeshindwa kupata ruhusa ya baba wa binti huyo ili aweze kumwoa -anatumia utekaji kama njia ya kulazimisha ndoa na msichana huyo kwa mujibu wa mila inayofahamika kama telefa nchini Ethiopia. Hata hivyo, msichana huyo anapambana, na kwa bahati mbaya anafanikiwa kumwua mwanaume huyo. Matokeo yake, msichana huyo anajikuta akikabiliwa na hukumu ya kifo mpaka pale mwanasheria Meaza Ashenafi anapoingilia kati kumsaidia. Kurindima kwa kesi hiyo mahakamani kulivuta hisia za watu wengi nchini humo mwaka 1996, wakati mkasa huo ulipotokea.

“Kwa mara nyingine, watu walianza kuzungumzia mila hiyo ya kumteka mwanamke,” Meaza Ashenafi anakumbuka. “kumteka mwanamke lilikuwa suala lnalokubalika, hususani kusini mwa nchi hiyo, wanawake walikuwa wakitekwa kwa miaka mingi. Hapakuwa na yeyote aliyethubutu kuhoji mila hiyo. Lakini kesi hii ilifungua mjadala mkali dhidi ya mila hii potofu.”

Ashenafi alikuwa ndio kwanza ameanzisha Umoja wa Wanasheria Wanawake miaka miwili iliyopita kwa lengo la kupigania haki za wanawake kwa mujibu wa katiba mpya ya Ethiopia.

A scene from "Difret" depicts the horseback kidnapping of the main character. Credit: Truth Aid Media

Sehemu ya filamu hiyo ikionesha tukio la kutekwa kwa mwanamke kwa njia ya farasi. Haki Miliki: Truth Aid Media

Filamu ya “Difret” imeoneshwa kwenye kumbi za filamu mjini Addis Ababa kwa majuma sita. Watengeneza filamu walipotaka kuipeleka nje ya nchi, walimtumia Jolie, wakili [6] maarufu wa haki za wanawake barani Afrika.

“Filamu hiyo ya kigeni kutoka barani Afrika ina kazi ngumu mbeleni kwa maana ya kupata watazamaji,” mtayarishaji wa filamu Mehret Mandefro anakiri. “Kwa hiyo kupata ushirikiano wake kumetusaidia sana…kukutana na watu ambao hatukudhani kama tungeweza kuwapata.”

Pamoja na kupata msaada wa watu maarufu na mafanikio ya filamu ya “Difret,” Ashenafi na Mandrefo wanasema kazi yao bado haijakamilika: wanakadiria kwamba si chini ya asilimia 20 ya ndoa kusini mwa Athiopia zinatokana na mila inayofanana na telefa.

“Mila hii lazima itokomezwe,” Ashenafi anasema. “Mila hii haivumiliki kwa vyovyote.”

Kuhusu malengo makuu ya filamu yenyewe, Madrefo anasema amekuwa na maisha magumu baada ya kesi yake, hakuruhusiwa kurudi kijijini kwake wala kuungana na familia. Alijiunga na shule ya bweni, na baadae akaamua kubadili jina lake na kuhama nchi. Hata hivyo, hivi karibuni alirudi nyumbani na kuendeleza harakati za kupambana na mila hiyo ya telefa, alitumaini kuwakinga wasichana na mikasa kama aliyokumbana nayo.