- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Ni Zaidi ya Wanablogu wa Zone9: Wa-Ethiopia Wengine Watumiao Intaneti Wakabiliwa na Mashtaka ya Ugaidi

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ethiopia, Censorship, Haki za Binadamu, Harakati za Mtandaoni, Siasa, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Vijana, GV Utetezi

Zelalem, Yonatan, Bahiru and Abraham. Picha imetumiwa kwa ruhusa kutoka tovuti ya debirhan.com

Sambamba na kesi maarufu sasa ya wablogu wa Zone9 [1], kuna wanablogu, wanaharakati wa mtandaoni na wanasiasa wengine wengi wa ki-Ethiopia waliowekwa ndani ingawa majina yao bado hayajatajwa.

Mwaka uliopita mnamo Julai 8, 2014, Serikali ya Ethiopia iliwakamata [2] viongozi kadhaa wa upinzani, wanablogu, wanaharakati wa mtandaoni na raia kadhaa wanaoguswa na mwenendo wa mambo nchini humo. Baadhi yao waliachiwa baada ya miezi minne ya kuhojiwa. Hata hivyo, kumi kati yao walisomewa mashtaka yao [3] mnamo Oktoba 31, 2014 chini ya sheria ya Ethiopia ya Kupambana na Ugaidi  [4] kwa madai kuwa wana mitandao [4] ya makundi ya upinzani ya wa-Ethiopia wanaoishi nje ya nchi hiyo kama vile Ginbot 7 [5], kutuma maombi ya kuhudhuria mafunzo ya usalama wa kimtandao [6], pamoja nna kujihusisha na uanaharakati wa mtandaoni. Watatu kati ya washtakiwa 10 hawakuwa wanachama wa chama chochote cha siasa zaidi ya kuwa raia wa kawaida waliokamatwa kwa kuomba kupata mafunzo ya usalama wa mtandaoni. Hawa ni Zelalem Workagenegu, Yonatan Wolde and  Bahiru Degu.

Sheria hiyo tata ya Kupambana na Ugaidi [7] ilianza kufanya kazi mwezi Julai 2009. Maafisa wa Ethiopia wanaitetea sheria hiyo kwa kudai kwamba vipengele vyake vyenye utata vilinukuliwa kutoka kwenye sheria zinazofanya kazi katika nchi nyingine kama vile Uingereza. Ibara ya 6 ya sheria hiyo, ambayo ndiyo imetumika kufinya uhuru wa kujieleza, inatamka kwamba: 

Mtu yeyote atakayechapicha au kuwezesha kuchapishwa kwa tamko linaloweza kutafsiriwa na baadhi au watu wengine wote kama kuhamasisha moja kwa moja au kwa namna moja au nyingine ama kuwafanya watu kufanya au kujiandaa au kuchochea kitendo cha ugaidi [atastahili kifungo cha kati ya miaka 10 na 20 jela.]

Zelalem, mshitakiwa wa kwanza, ni mhadhiri na mwanaharakati wa haki za binadamu anayeblogu kwenye blogu ya DeBirhan [8]. Yonatan na Bahiru, wanaoweza kuelezewa vizuri kama wananchi wenye kuguswa na hali ya mambo nchini mwao, walituma maombi sambamba na Zelalem kushiriki mafunzo ya usalama wa intaneti na mitandao ya kijamii baada ya kuarifiwa uwapo wa mafunzo hayo na mwandishi mmoja wa ki-Ethiopia anayeishi Marekani. Kukutwa na barua pepe kutoka kwa mwandishi huyo aliyekuwa Marekani lilikuwa kosa kubwa na vijana hawa walikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kutuma maombi ya “kushiriki mafunzo ya ugaidi” wakati ukweli ni kuwa mafunzo hayo yalihusiana na usalama wa mtandao wa intaneti kwa watumiaji.

Mwezi uliopita, mahakama ya Ethiopia haikuwakuta na hatia [9] Abraham Solomon, aliyekuwa amekamatwa kwa kosa la kuwa na uhusiano na mshitakiwa wa kwanza Zelalem, sambamba na wanasiasa wengine wanne wa upinzani ambao ni Abraha Desta, afisa wa chama cha upinzani cha Arena Tigray Party na mwanaharakati wa mitandao ya kijamii, Yeshiwas Assefa, mwanachama wa baraza la chama cha siasa cha Semayawi, Daniel Shibeshi, afisa wa chama kisichosikika sana cha Unity for Democracy and Justice (UDJ) na Habtamu Ayalew, Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa chama hicho. Hata hivyo, mpaka leo hawajaachiliwa huru kwa sababu Mwendesha mashtaka anasekana kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Makala iliyoandikwa na asasi ya Electronic Frontier Foundation [10] inaonesha kuongezeka kwa juhudi za kuwanyamazisha wanaharakati wa mtandaoni pamoja na watumiaji wa jumla wa mitandao hiyo wanaoishi Ethiopia. Asasi hiyo ilitoa mwito kwa Ethiopia:

Tunadai kuachiwa huru waandishi wote walioko gerezani, ikiwa ni pamoja na wanablogu wa Zone 9 waliobaki, na kufutiwa mashtaka yote ya kutenda ‘jinai’ kwa sababu tu ya kuandika habari.
Acheni kutesa watu kwa [kosa la] kutafuta mafunzo ya usalama mtandaoni ama kutumia teknolojia za kuficha taarifa zao. Mwachieni huru Zelalem Workagegnehu, Yonatan Wolde, Abraham Solomon, na Bahiru Degu.

Komesheni na acheni kutumia teknolojia za kudukua mawasiliano ya watu kama vile FinFisher na mfumo wa kudhibiti mawasiliano ya wengine unaitwa Hacking Team kuwapeleleza waandishi wa habari wa Ethiopia, nje ya nchi, na makundi ya upinzani.

Wakati kesi ya Zone9 [1] inabaki kuwa ya aina yake nchini Ethiopia, habari kama za Zelalem zinaleta picha kwamba masuala yanayowakabili wanablogu hawa yanavuka mipaka ya makosa binafsi ya watu wachache. Zelalem, Yonathan na Bahiru wanatarajiwa kusomewa mashtaka yao kati ya Novemba 7-9, 2015.