Mlipuko na Milio ya Risasi Katika Kasri la Dolmabahçe huko Instanbul

The peaceful exterior of the Dolmabahçe Palace. Photo by Jack Hennessy.

Muonekano wa nje wa kuvutia wa Kasri la Dolmabahçe. Picha na Jack Hennessy.

Hii ni makala ya ushirika iliyoandikwa na Jack Hennessy na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na Global Student Square. Imechapishwa tena kwa ruhusa. 

Washukiwa wawili waliokuwa na bunduki wameshakamatwa mara baada ya kutokea kwa mlipuko ulioambatana na kurushiana risasi kwenye Kasri la Dolmabahçe,jijini Instanbul ambalo ni kivutio kikuu cha watalii na palipo na makazi ya Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

Watu walipatwa na taharuki huku wakikimbia na kuruka mageti na kisha kuingia mitaani pale wavamizi wawili walipotupa bomu la mkono pamoja na kuvurumisha mizunguko kadhaa ya risasi, shambulizi linalodhaniwa kuwa liliwalenga maafisa wa polisi waliokuwa wameweka doria katika eneo la Ottoman-era. Hata hivyo, polisi walifanikiwa kukabiliana mapema na wavamizi hao.

Associated Press lilitaarifu kuwa, polisi mmoja alijeruhiwa kidogo katika tukio hilo.

Pamoja na kuwa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika katika tukio hilo, kwa mujibu wa Associated Press Anadolu, moja ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali lilitaarifu kuwa, washambuliaji hao walikuwa ni wanachama wa chama cha Kijeshi cha Wanaharakati wa Ukombozi wa Kimapinduzi, au DHKP-C. The Guardian pia lilitaarifu kuwa vyombo vya habari vya Uturuki viliwakariri maofisa wa polisi walioelezea kuwa DHKP-C ndio waliohusika kwenye shambulio hilo.

Dolmabahçe linabaki kuwa moja ya Makasri muhimu sana yaliyosalia ya Ngome ya Ottoman jijini Istanbul. Mbunifu wa Uturuki ya kisasa, Mustafa Kemal Atatürk, alifariki akiwa kwenye Kasri hili mwaka 1938. Kasri hili ni eneo muhimu kwa ajili ya watalii, pamoja na kuwa maeneo mengine yanatumiwa na taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na makazi ya Waziri Mkuu wa Uturuki.

Tukio hili linakuja kipindi ambacho kumekuwa na mvutano mkali nchini Uturuki, kwani Rais aliyepo madarakani, Reccip Tayyip Erdogani pamoja na Chama cha Utafutaji Haki (AKP) wakiwa wameonesha kwa mara nyingine chuki dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi waliopo huko kaskazini mwa Iraki pamoja na wanamgambo wa Dola ya Kiislam nchini Syria.

Image: Google maps

Image: Google maps

Pia, siku ya Jumatano, wanajeshi watano waliuawa kufuatia mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa pembezoni mwa barabara huko Siirt, eneo la Kusini mwa Uturuki linalopakana na nchi za Siria na Iraki.   Kwa mujibu wa BBC, shambulio hilo linadhaniwa kuwa lilitekelezwa na wanamgambo wa PKK.

“Uturuki ipo katika hali kuu ya tahadhari,” alisema, Eyup Kabogan, aliye na umri wa miaka 27, mfanyakazi katika hoteli ya Pierre Loti iliyopo Sultanahmet, katikati mwa Jiji la Istanbul takribani kilometa 5 Kusini mwa Kasri hili. “Kwa sasa, ninapaswa kuchukua tahadhari kila mtaa ninaopita.”

“Hata hivyo, mimi ni Mkurdi,” anasema Kabogan, anaongeza, “lakini ninajua kuna namna nyingine ya kubadili hali ya mambo (kisiasa).”

Kabogan alionya kuwa, watalii wanapaswa kuwa mbali na mikusanyiko mikubwa ya watu pamoja na kutokuwepo karibu na vituo vya polisi, pamoja na kuwa alitanabaisha kuwa, makundi ya waasi “hayawalengi watalii, bali maafisa wa usalama.”

Hali ya siasa za Uturuki ipo katika misukosuko kufuatia kushindikana kwa jaribio la Davutoglu la wiki jana la kuunda serikali ya mseto. Siku ya Jumanne, alitoa mamlaka kwa Rais Erdogan ya kuunda serikali mpya kabla ya chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwezi November.

“Sijui hata niseme nini (kufuatia shambulizi la leo),” alisema Berk Çoker, aliye na umri wa miaka 21, ambaye ni mturuki na kinda aliyepo Chuo Kikuu cha Stanford.

Coker, ambaye ni mtaalamu wa Sayansi ya Kompyuta, alikuwa na mipango ya kurejea nchini mwake mara baada ya kumaliza mafunzo yake ya ujasiriamali wa uhandisi wa vitumizi vya kompyuta, uliokuwa unafanyikia eneo la San Francisco Bay katika kipindi cha majira haya ya joto.

“Kama inavyodhihirishwa kwa mashambulizi pamoja na kutofikia makubaliano ya serikali ya mseto, hali ya kisiasa bado ni tete sana, kiasi cha kuifanya nchi hii isiwe salama kuizuru,” Coker alisema.

Kufuatia machafuko yanazozidi kushamiri, kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph, serikali ya Erdogan imeshawatia nguvuni zaidi ya washukiwa 2,500 wa makundi ya IS, PKK na DHKP-C.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.