- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Shughuli Husimama kwa Muda Waziri Mkuu wa Pakistan Anapotembelea Jiji la Quetta

Mada za Habari: Asia ya Kusini, Pakistan, Safari, Uandishi wa Habari za Kiraia, Utawala
Courtesy: Demotix.com [1]

Foleni ya magari kwenye barabara ya Zarghoon jijini Quetta, Pakistan. Picha ya PPIimages tarehe 1 August 2011. Copyright Demotix.

Makala haya yaliandikwa na Adnan Aamir kwa tovuti ya The Balochistan Point [2]. Imechapishwa kwa mara nyingine Global Voices kwa makubaliano ya kushirikiana maudhui. 

Maisha na shughuli za kawaida zilisimamishwa kwa raia wengi, wanafunzi, wagonjwa na wasafiri wa jiji la Quetta city, pale Waziri Mkuu wa Pakistani na ujumbe wake walipozuru kwenye makao makuu ya jimbo la Balochistan juma lililopita.

Kwa mujibu wa makadirio, mamia ya maelefu ya raia wanaathirika moja kwa moja au kwa namna moja au nyingine kila barabara zinapofungwa kwa sababu za usalama wa watu maarufu wanapozuru Quetta, jiji lenye wakazi milioni 1 [3]. Hii ni mara ya tano maafisa wa usalama wanafunga njia kwa ajili ya kuwapisha watu maalumu kwenye jiji hilo ndani ya mwaka huu.

Waziri Mkuu Nawaz Sharif aliwasili Quetta asubuhi kushiriki mkutano wa vyama vya siasa uitwao “Mkutano wa Vyama Vyote vya Siasa [4]“. Mkutano huu uliitishwa baada ya tukio la mauaji ya kwenye basi la Mastung jijini Balochistan, [5] ambapo wanamgambo waliwaua abiria 22 wa Pashtun kwenye shambulio linalosemekana kusukumwa na chuki za kikabila.

Barabara zote za Quetta zilizo karibu na Makazi ya Gavana, mahali ambapo mkutano huo ulifanyika, zilzifungwa kwa sababu za kiusalama. Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, imekuwa kawaida kila  mwanasiasa au mtu maarufu alipotembelea Quetta [6], barabara zote kufungwa na usafiri wa kawaida kuzuiliwa.

Wasafiri kutoka nje ya jiji waliokuwa wanaingia mjini walilazimika kutembea umbali wa kilometa mbili hadi tatu ili kufika walikokuwa wakienda kwa sababu barabara zote zilikuwa zimefungwa. Usafiri wa umma haukuruhusiwa kuingia katikati ya jiji na wasafiri walishushwa karibu na vizuizi.

Wagonjwa na watu waliokuwa wakielekea kwenye hospitali kubwa ya jiji hilo iitwayo Sandmen iliwabidi kuvumilia mateso ya kusubiri masaa kadhaa kabla ya kuingia hospitalini, iliyopo karibu kabisa na Makazi ya Gavana.

“Nilisafiri kutoka kijijini kwangu wilayani Kalat kuja Quetta nikimleta mtu kwa dharura lakini kwa sababu ya kufungwa kwa barabara sitaweza kufika ninakokwenda kwa wakati,” Murtaza Baloch, aliuambia mtandao wa The Balochistan Point. Aliongeza, “sasa itanibidi kurudi Quetta siku nyingine na huu ni usumbufu mkubwa kwangu.”

Shule tatu kubwa jijini hapo Mt. Francis, Mt. Joseph na Sacred Heart zote zilitangazwa kufungwa na mamlaka za jiji. Shule hizo ziko kwenye barabara inayotumiwa na waziri mkuu.

“Kila Waziri Mkuu akitembea mji huu, binti yangu hupoteza siku moja ya shule kwa sababu shule yao hufungwa kwa siku hiyo,” alisema Saleem Haider, mkazi wa Quetta.

Siku hiyo ya ziara ya waziri mkuu, Muhammad Siddique, mmliki wa gari lililokuwa kwenye foleni alisema mikutano muhimu na safari za watu maarufu zibaki kuwa kwenye maeneo ya kijeshi la jiji hilo. “Kama waziri mkuu na serikali ya Balochistan wanawajali kidogo tu wakazi wa Quetta,” Siddique alisema, “basi wafanye mikutano yao kwenye maeneo ya kijeshi ya Quetta na kutuepusha na matatizo yasiyo ya lazima.”