Muda Gani Umebaki kwa ‘Marais wa Maisha’ Barani Afrika?

Burundian president Pierre Nkuruzinza. Photo released under Creative Commons by the World Economic Forum.

Rais wa Burundi Pierre Nkuruzinza. Picha imetolewa chini ya leseni ya Creative Commons na World Economic Forum.

Utafiti mpya uliofanywa na Afrobarometer, mradi unaopima mitazamo ya wananchi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, unaonesha kwamba wa-Afrika wengi wanaunga mkono ukomo wa vipindi viwili tu kwa marais wao.

Taarifa hiyo, inayojumuisha tafiti katika nchi 34 za Afrika, inasema:

[Matokeo] haya yameonekana hata kwenye nchi zile ambazo hazijawahi kuwa na ukomo wa vipindi vya urais na hata kwenye nchi zile zilizoondoa ukomo huo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Juhudi zinazoendelea za kuondoa ukomo wa madaraka zinaonesha tofauti kubwa kati ya matakwa ya watawala wa Afrika dhidi ya matakwa ya wananchi wanaowongoza, hali inayoonesha kuendelea kuwepo kwa hulka ya udikteta barani humo na hivyo kuonesha dalili mbaya kwa demokrasia ya Afrika.

Taarifa inajadili dhana ya kuongeza ukomo wa mihula ya utawala katika siasa za Afrika:

Mwishoni mwa karne ya 20 , nchi nyingi za Afrika ziliweka ukomo wa mihula ya urais kama sehemu ya sheria pana za kikatiba zilizoenda sambamba na mabadiliko kutoka kwenye utawala binafsi na wa kiimla kwenda kwenye mfumo wa utawala unaoheshimu matakwa ya walio wengi. Wakati takwa la ukomo wa mihula ya urais lilipokelewa vizuri na wananchi wengi wa Afrika, bado sheria hizi katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikishambuliwa na marais walioko madarakani wanaotafuta kuendelea kutawala [wananchi hao hao wanaotaka ukomo]. Katika miezi sita ya kwanza ya 2015 pekee, marais wa Burundi, Benin, Congo (DRC), na Rwanda wamejaribu ama wao wenyewe au kwa kuwatumia wafuasi wao, kuonesha nia ya kuondoa ukomo wa mihula ya utawala ili kuwawezesha kupata muhula mwingine madarakani.

Majaribio haya mara nyingi hufanyika kwa lugha inaonesha kuwa nia ya watawala hawa kuendelea kubaki madarakani ni kuitikia mwito wa wananchi. Mfano wa karibu ni ule wa jaribio la mwaka 2014 la Blaise Compaoré kutafuta muhula wa tatu nchini Burkina Faso, ambalo lilisitishwa na maandamano makubwa nchini humo kumlazimisha rais si tu kuachana na wazo hilo, lakini kuihama nchi. Lakini wapo watawala wengine ambao jitihada zao za kukwepa kuondoka madarakani zilifanikiwa.

David Shinn, balozi wa zamani wa Marekani nchini Burkina Faso na Ethiopia, anasema rekodi ya ukomo wa mihula ya urais katika siasa za Afrika ina mkanganyiko:

Rekodi ya Afrika kwenye suala la ukomo wa urais ina mkanganyiko. Mapema mwaka 2008, nchi thelathini na tatu kati ya arobaini na nane zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zilikuwa na katiba zenye ukomo wa vipindi vya urais. Baadhi ya watawala wa Afrika kwa hiari yao wamekubaliana na matakwa haya ya katiba. Hawa ni pamoja na watawala wa zamani wa Botswana, Benin, Cape Verde, Mali, Mozambique, Säo Tomé e Principe na Tanzania. Nelson Mandela wa Afrika Kusini aling'atuka baada ya muhula mmoja tu wa urais. Jerry Rawlings wa Ghana na Daniel arap Moi wa Kenya walikubaliana na matakwa ya katiba zao zilizoweka ukomo wa urais.

Watawala wengine wa Afrika walijaribu kubadili masharti yaliyoweka ukomo wa madaraka kwenye katiba ili waendelee kutawala na wakashindwa. Kuna Frederick Chiluba wa Zambia, Bakili Muluzi wa Malawi na Olusegun Obasanjo wa Naijeria ambao hatimaye ilibidi kukubaliana na matakwa ya mfumo wa kisiasa yanayodai kuwepo kwa ukomo wa madaraka.

Hata hivyo, wapo watawala wa Afrika waliofanikiwa kubadili katiba zao ili kupata angalau muhula mwingine wa kugombea. Watawala wa sasa au wa hivi karibuni nchini Burkina Faso, Chad, Gabon, Guinea, Namibia, Togo, Uganda na Aljeria ni miongoni mwa wale walifanikiwa kuondoa ukomo wa madaraka ili kuwawezesha kuendelea kuwa madarakani. Mwaka 2008, bunge la Cameroon liliondoa ukomo wa madaraka (ambao ni miaka saba kwa muhula) kwa ajili ya Paul Biya. Nilifanya kazi kwneye ubalozi wa Marekani jijini Yaounde wakati ambao Biya aliingia madarakani mwaka 1982. Ataweza kugombea tena mwaka 2011 baada ya kutawala kwa miaka ishirini na nane akiwa rais. Rais wa Naija hivi sasa anaendelea na jitihada zake za kubadili katiba ili aweze kugombea tena kwa muhula wa tatu.

Kwa ujumla, nchi 18 za Afrika hazina masharti ya ukomo wa urais. Sudani ni mfano tofauti kidogo; ingawa Rais Bashir amekuwa madarakani tangu mwaka 1989, kuchaguliwa kwake tena mapema mwaka huu -huku akipata asilimia 94 ya kura – ndio muhula wake wa pili pekee unaoweza kusema amekuwa madarakani, kufuatia kujitenga kwa Sudani Kusini mwaka 2011 baada ya kura ya maoni.

Wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) mwezi uliopita jijini Accra, Ghana, watawala wa Afrika Magharibi walikubaliana kuachana na wazo kuheshimu ukomo wa mihula miwili tu ya urais katika eneo hilo, baada ya Gambia na Togo, nchi wanachama pekee zisizo na ukomo wa madaraka, kupinga hatua hiyo. Watuamiaji wa intaneti katika eneo la Afrika Magharibi walipinga vikali uamuzi huo.

Mgogoro wa Burundi unaendelea leo, umechochewa na Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kutaka kugombea tena kwa muhula wa tatu. Ghasia zimeenea nchini kote kwa maandamano. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kimoon amemwomba Rais wa Uganda Museveni kuingilia kati suala hilo. Kwenye mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jenerali wa zamani wa jeshi Godefroid Niyombare (ambaye alikuwa amesimamishwa miezi kadhaa iliyopita) aliongoza jaribio la mapinduzi kutaka kumng'oa Nkurunziza. Hata hivyo hakufanikiwa.

Matukio nchini Burundi na nchi nyingine kama Kongo (DRC), Burkina Faso, na Rwanda zimeendeleza mijadala inayoendelea miongoni mwa wa-Afrika kuhusu ukomo wa madaraka.

Kwa mfano, nchini Uganda ambapo rais anaonekana kutafuta kuchanguliwa tena kwa muhula saba, watumiaji wa mtandao walisherehekea mapinduzi nchini Burundi:

Wa-Ganda wanasherehekea mapinduzi katika nchi ndogo ya Burundi wakati Rais wao anatamani kugombea kwa muhula wake wa saba

Sasa ninaweza kuelewa kile walichokimaanisha wa-Rundi walipomwambia Nkurunziza kwenda Uganda kama alitaka kuwa rais wa maisha

Utani mwingi umefanywa kuhusiana na mapinduzi ya Burundi. Allan Senyonga, mwandishi wa habari anayefanya kazi Rwanda, alisema:

Mtawala wa zamani wa Burundi: Pierre N-coup-runziza. (P ya kwenye coup inayomaanisha mapinduzi haitamkwi)

Nkurunziza: Mungu ameniambia kugombea ‘muhula wa pili’.
Mungu: Usilitaje bure jina langu kama huwezi hata kuhesabu vizuri

Simon Kaheru alifanya utafiti mdogo kwa wasomaji wake kuhusu alama habari zinazotumika zaidi kumkejeli Nkurunziza:

Inaonekana ni utani mbaya, lakini wacha niulize: Hivi kuna alama habari ambazo watu wanazitumia kumkejeli Nkurunziza?

Mchora katuni wa gazeti la Daily Monitor alikuwa na mchoro ufuatao:

Wakati dunia ikingoja kusikia kutoka kwa Nkurunziza, hebu usipitwe na katuni ifuatayo

Rais wa kwanza wa Uganda, Dk. Milton Obote, aling'olewa kwa namna inayofanana na ile iliyotumiwa na Niyombare, wakati akitoa hotuba kwenye mkutano wa Commonwealth nchini Singapore mwaka 1971.

Milton Obote atakuwa anamcheka Nkurunziza kaburini kwa kushindwa kusoma historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Benjamin Rukwenge alionesha kutokuwa na imani na marais wa Afrika Mashariki:

Kama taarifa kutoka Burundi ni kweli, ningependa kuamini hawa jamaa hawakula njama na kumwita Dar, wakijua atapinduliwa

Denis Juuko aliwalaani wale waliokuwa wakifurahia mapinduzi:

Kama unashangilia kuona mapinduzi ya Burundi, basi wewe ni adui wademokrasia

Nchini Zimbabwe, ambapo rais Robert Mugabe amekuwa madarakani tangu 1980, mtu mmoja anayetumia jina la Hungwe alitania kwenye habari ya tovuti ya New Zimbabwe, akitania:

Minimum of 4 terms of course! One term to fill up personal pockets. Another term for the family. Another one for relatives and friends, and probably another one to look at national issues and avenues to stay in power.

Mihula minne iwe ni kiwango cha chini kabisa! Muhula wa kwanza unautumia kujaza mifuko yako. Muhula wa pili unawasaidia wanafamilia. Mwingine unautumia kwa ndugu na marafiki na muhula wa mwisho unautumia kuyatazama masuala ya kitaifa na namna ya kubaki madarakani.

Raia mwingine wa Zimbabwe, “William Doctor,” aliuliza:

kwa nini ukomo wa mihula miwili umekuwa na mafanikio Marekani? Na kwa nini hapa Afrika haiwezekani?

“Mchambuzi wa Siasa,” anayeonekana kukaa Zambia, alishauri:

Msikubali dikteta atake muhula wa tatu

Mwingine anayetumia jina la “Bants-a-nius Dante” alionya:

Hizi ni nyakati mbaya kwa Mugabe, Hayatou [Issa Hayatou ni rais washirikisho la Mpira wa mpira tangu mwaka 1988], Nkurunzizana wengine wanaong'ang'ania madaraka duniani kote…

Mtumiaji mwingine wa mtandao alidai kwmaba tatizo sio marais wa Afrika bali wagombea urais wa upinzani wanaogombea mara nyingi, kama ilivyo nchini Zambia:

Unategemea nini kutoka kwa mtu kama HH [Haikainde Hichilema] aliyegombea mara sita, Nawakwi mara sita, Nevers Mumba mara mbili, tafadhali waachieni nafasi wengine nyie mmeshashindwa mara nyingi na imetosha.

Hata hivyo, alitoa maoni kwenye habari kuhusu Rais wa Rwanda Paul Kagame, aliyesema kwamba yuko tayari kuachia madaraka, Abullah Omar aliandika:

Sielewi hizi porojo za ukomo wa madaraka. Kama watu wataamua uelendelee kwa nini uwakatalie wanachokitaka.

Profesa Nshuti Manasseh alikuwa na mtazamo ule ule:

Lakini Wanyarwanda wanamtaka aendelee kubaki ili ahakikishe utengamano na maendeleo yanakuwepo kwenye nchi hiyo tete iliyokuwa kwenye mauaji ya kimbari kwa miaka 21. Kwa hiyo kama Wanyarwanda wanaomba awaongeze kwa zaidi ya mihula miwili, hiyo sio demokrasia?

“Injinia.Murenzi Daniel” alidhani kwamba Rwanda na Burundi zina hali tofauti kidogo linapokuja suala la ukomo wa urais:

“Kiongozi” “Dikteta” Kagame AMELAZIMISHWA na watu kugombea muhula wa tatu na (kiongozi) Nkuruzinza ANALAZIMISHA watu agombee kwa muhula wa tatu. (Dikteta)

Raymond Maro, anayeishi Tanzania, alikuwa na matumaini:

Tanzania ni nchi ya kwanza katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara kuwa na ukomo wa kipindi cha Urais. Ifikapo mwaka 2017 nchi zote za Afrika ziige mfano huu

Mwanablogu wa Kenya Ken Opalo alibainisha kwamba taarifa zinaoonesa kwamba marais wanaojaribu kuongeza kipindi cha urais wana nafasi kubwa ya kufanikiwa:

Kile tunachokiona kwenye takwimu nikwamba wale wanaojaribu kuondoa ukomo kwa Wakuu wa Nchi za Afrika wana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuliko kinyume chake (tisa wamefanikiwa, sita wameshindwa). Hata hivyo, hali hii haituambii chochote kuhusu marais ambao hawakuonesha rasmi kutaka kujiongezea muhula madarakani. Kwa mfano, nchini Kenya (Moi) na Ghana (Rawlings) marais hawakuanzisha mjadala rasmi wa kujiongezea muhula wa urais lakini kulikuwa na tetesi nyingi kwamba walijaribu. Kwa hiyo huenda ni kweli kwamba marais wanaweza kufanikiwa kwa kuamua kuanzisa mjadala wa wazi wa suala la kujiongezea muhula wa kutawala, na hivyo kuweka uwiano. Na kama ukiingiza na nchi ambazo zimewahi kuwa na zaidi ya tukio moja la marais waliolazimishwa na katiba kuachia madaraka na wakafanya hivyo, hali inaonekana kuwa nzuri kwa kuwa na ukomo wa madaraka katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Anahitimisha kwa hoja yenye matumaini:

Siwezi kujua kwa hakika, lakini kuna uwezekano kuwa kwenye kipindi cha muongo ujao, Umoja wa afrika utakuwa na azimio (kama lile linalopinga mapinduzi) linalowawekea vikwazo Wakuu wa Nchi wasioheshimu ukomo wa kuwa madarakani.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.