Mwanablogu wa Ethiopia, Atnaf Berahane: Kijana Anayejiamini, Aliye Gerezani

Atnaf Berhane, member of the Zone 9 Bloggers was jailed for blogging about human right violations in Ethiopia. (Digital drawing by Melody Sundberg)

Atnaf Berhane, mmoja wa wanablogu wanaounda kundi la wanablogu wa Zone 9, amefungwa gerezani kwa sababu ya kublogu kuhusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Ethiopia. (Hisani ya picha: Mchoro wa kidigitali na Melody Sundberg. Picha imetumiwa kwa ruhusa yake)

Mnamo mwezi wa Aprili, wanablogu tisa pamoja na waandishi wa habari walikamatwa nchini Ethiopia. Baadhi ya wanaume na wanawake hawa walikuwa wakifanya kazi na Zone9, blogu ya ushirika  iliyokuwa inazungumzia masuala ya kijamii na ya kisiasa nchini Ethiopia ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uzingatiaji wa haki za binadamu na uwajibikaji wa serikali. Miongoni mwao, wanablogu wanne walikuwa ni waandishi wa Global Voices. Mwezi Julai, walihukumiwa chini ya tamko la wazi la nchi dhidi ya ugaidi. Tangu wakati huo, wameendelea kuwepo gerezani, huku shitaka lao likiwa linaahirishwa mara kwa mara.

Wiki iliyopita, tuliweka makala yetu ya kwanza kutoka kwenye mfululizo wa makala- “Wanayo Majina” – iliyo na tumaimi la kuwazungumzia wanablogu ambao hadi sasa wapo gerezani. Tunataka kutambua utu wao, tunataka kuelezea habari zao za kipekee na mahususi kabisa. Wiki hii, mwandishi kutoka Ghana, Kofi Yeboah, aandika kuhusu mwanablogu mdogo kabisa wa Zone9, Atnaf Berahane.  

Atnaf Berahane, aliye na umri wa miaka 26, ndiye mwanablogu wa Zone9 aliye mdogo kuliko wengine wote. Alitiwa kizuizini nchini Ethiopia mnamo tarehe 25 April, 2014 akiwa na wenzake Abel Wabela, Befeqadu Hailu, Mahlet Fantahun, Zelalem Kibret, na Natnael Feleke (wote wakiwa katika ushirika wa kublogu wa Zone 9) pamoja na waandishi wa habari, Asmamaw Hailegeorgis, Tesfalem Waldyes na Edom Kassaye.

Ethiopia ni nchi ambayo uhuru wa kujieleza unaminywa na serikali. Nchini Ethiopia, kuna sheria kali dhidi ya uanahabari, hususani pale linapokuja suala la kujadili kuhusu siasa na haki za binadamu. Hii inapelekea raia kutegemea kupata habari kupitia mtandao wa intaneti.

Hamasa ya Atnaf ya kujihusisha na uelimishaji wa jamii na kuvutiwa kwake kusambaza taarifa kwa raia ili kuwafahamisha kile katiba ya nchi inachokizungumzia kuhusiana ha haki na uhuru wao ilimfanya yeye kuwa mmoja wa waanzilishi wa blogu ya zone9: Hamasa yake ya kuwa mwanaharakati wa haki za binadamu ilichochea yeye kuwa mmoja wa waanzilishi wa asasi ya Zone9. Hata hivyo, hamasa yake ya kutetea haki za binadamu imempelekea kupokonywa uhuru wake.

Katika maisha yake ya kawaida, Atnaf ni mtaalamu wa masuala ya TEHAMA anayefanya kazi na mamlaka ya Jiji la Addis Ababa katika mji wa Bole. Blogu ya trailtracker, ambayo marafiki wa wanablogu na waandishi hawa wamekuwa wakiitumia kuweka mara kwa mara taarifa za maendeleo ya kesi yao pamoja na hali yao, wanamwelezea Atnaf kama Mhabeshi ambaye “anafahamika kwa umahiri wake wa kutumia twita kusambaza kwa haraka habari motomoto za nchi yake”. Pia, Atnaf anamiliki blogu yake na pia ni mtaalamu wa masuala ya usalama wa kidigitali.

Ukweli unaoumiza wa ndoto izimwayo ya kijana mdogo kama Atnaf unafafanuliwa vizuri kwenye makala hii:

Hii ni “Shirikisho la Jamhuri ya Ethiopia” au ni “Jamhuri ya Daistopia” (Taifa la polisi)?

Je, Ethiopia imevuka mipaka, kwa kiwango cha tano?…

Ethiopia ya leo inaweza pia kuitwa “Jamhuri ya Daistopia”. Vijana wadogo wa miaka 20 wanakamatwa na kufungwa gerezani kwa “ugaidi” kwa kisa tu cha kuelimisha watu kupitia mtandao wa Facebook pamoja na kutoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii.

Atnaf, pamoja na wanablogu wengine walioko gerezani wanapaswa kupongezwa na siyo kifungo gerezani. Siyo tu mustakabali wa Atnaf unaowekwa rehani, bali pia ni kwa kila kijana mwenye ari na aliyenuia kuiwajibisha serikali kandamizi kwenye uhuru wa kujieleza.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.