Watu 147 Waliouawa Garissa Ni Zaidi ya Takwimu

Photos of Garissa shooting victims being shared under the 147notjustanumber hashtag on Twitter.

Picha ya gazeti huru la Daily Nation (@DailyNation) ikiwa na picha za wahanga wa shambulio la Garissa, iliyosambaa kwenye mtandao wa Twita.

Habari zilizochukua nafasi ya mbele kwenye vyombo vya habari vya kimataifa na vile vya ndani ya nchi kuhusiana na shambulio la kigaidi lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab kwenye Chuo Kikuu cha Garissa, lililosababisha vifo vya watu 147, zimepata ukosoaji mkali. Wakati majina ya washambuliaji yakichapishwa sana, wahanga wa tukio hilo wamekuwa wakitajwa kwa tarakimu pekee: 147.

Katika kujaribu kufanya tofauti, wananchi wa Kenya mtandaoni wamefanya jitihada kubwa za kutangaza majina na sura za marehemu waliopoteza maisha yao kufuatia shambulio hilo.

Akiblogu kwenye blogu iitwayo Afrika ni Nchi, mwandishi wa Kenya Binyavanga Wainaina alisema Kenya “haitakuwa taifa kama hatutaweza kupeana heshima zinazostahili kwa raia wanaopoteza maisha yao”:

Ninataka kuona majina na umri na picha za wale wote waliopoteza maisha yao kwenye shambulizi la Mpeketoni. Wle waliouawa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi. Nataka habari zilizokamilika. Kusahau si jambo jema. Ni kupitia matendo haya, ubinadamu wetu unahuishwa. Siasa za kusema hatuko tayari kuwajitazama, uchungu mkubwa, ni siasa zinazoturuhusu kupuuza pale m-Kenya anapoharibu taasisi aliyoipewa kuiongoza, na kuiharibu vibaya, kisha kurudi tena, akiwa mithili ya roboti, aina mpya ya roboti kutawala sehemu nyingine tena.

Aliendelea:

Ninataka kuona wakazi milioni tatu wa Nairobi wakiingia mtaani kulia, kuimba na hata kukumbatiana kwa sababu watoto wetu wameuawa. Ninataka kuacha kujisikia kwamba tunaishi kwa uhuru wa ndani ya nafsi zetu. Nataka kuacha kusikia neno kujiwezesha kwa mara nyingine.

Kwenye mtandao wa Twita, Ory Okolloh Mwangi alieleza kwa nini ni muhimu katika utamaduni wa Kiafrika kuwataja kwa majina wahanga:

Kumtaja marehemu kwa jina lake ni jambo kubwa kwenye utamaduni wa Afrika. Ni kitendo cha kuyapa maisha maana inayostahili iwe kabla, hivi sasa na kwa siku zijazo. Na tutawaja kwa majina mmoja baada ya mwingine.

Ili kuweza kuwafanya wahanga kupata hadhi ya ubinadamu, baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Twita wame-twiti alama habari ya  #147notjustanumber yenye maana ya #147sitarakimutu ili kujaribu kuwataja marehemu kwa majina yao pamoja na picha:

Apumzike kwa amani Elizabeth Nyangarora. Alihitimu mwaka 2012 Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mt. Andrew

Huyu ni Tobias, aliuawa kwenye shambulio la Garissa; kwetu yeye si tarakimu, ni mwana, kaka, rafiki

Apumzike kwa amani Ivy Betty Wanjiku (Shiko) mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyeuawa kwenye shambulio la Garissa

Angela ‘Ka/Jojo’ Kimata Githakwa. Alimaliza Shule ya Sekondari ya Wasichana Karima mwaka 2011

Tutaendelea kuwakumbuka mioyoni mwetu daima. Tafadhali endelea kutuma wasifu na picha zao

Magaidi wanapoandikwa sana na majina yao yakionekana kuendelea kuwa hai, wahanga wa ugaidi wao wanasahaulika kama tarakimu tu

@Reclvse aliandika kwamba hatua hii inahusiana na na uhai wa binadamu na sio tarakimu:

Ninapenda namna wa-Kenya wanavyotaja majina na kusimulia wasifu wa wahanga wa shambulio la Garissa kuhakikisha kwamba hawabaki kuwa tarakimu pekee. Marehemu hawa ni binadamu, sio takwimu tu

@lunarnomad alizungumzia kuhusu lengo la kampeni hiyo:

Nimechoka kuona picha za marehemu wakitapakaa damu kufuatia shambulio la Garissa. Angalia alama habari ya #147sitarakimutu ili kuona binadamu walioathirika na risasi hizo

Mary Njeri Mburu alitwiti:

Ninaamini magazeti yataruhusu matangazo ya bure ya vifo kwa wahanga wa shambulio la Garissa kama walivyofanya baada ya lile la Westgate

Eunice aliweka mithali ya ki-Kenya, kwa kutumia alama habari tofauti— #KenyanLivesMatter [Maisha ya wa-Kenya yana thamani], sawa sawa na kampeni ya #BlackLivesMatter nchini Marekani:

Mtu atumiaye nguvu anaogopa kutumia akili. ~Methali ya ki-Kenya. Tuko pamoja katika kipindi hiki kigumu

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.