This is Uganda (ThisIs256) ni jukwaa la waandishi waliobobea kutoka Uganda walio na utayari wa kuandika habari makini za kuihusu nchi yao, wakilenga kutokomeza uanahabari uchwara, njaa, Ebola, ukabila, pamoja na mambo mengine. Wanachojaribu kukifanya ni kuanzisha aina ya utafiti kuihusu Uganda ambao ni halisi, makini, wa kweli na usio wa kiupendeleo ambao kamwe usingalikuwa rahisi kuuona kwenye vyombo vikuu vya habari vya magharibi.
Habari yao ya hivi karibuni ni ya kumhusu Victor Ochen,aliyekuwa mmoja wa wakimbizi wa ndani, aliyependekezwa na American Friends Service Committee (AFSC), ambayo ni taasisi ya utetezi wa haki za kiraia, kushindania Tuzo ya Amani ya Nobeli.
Kwa kipindi cha nyuma, AFSC iliwapendekeza akina Desmond Tutu, Martin Luther King Jr., na Rais wa Marekani, Jimmy Carter, ambao wote walifanikiwa kushinda tuzo hii. Taasisi hii mara kadhaa ilimpendekeza Mahatma Gandhi, ambaye hata mara moja hakufanikiwa kutangazwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobeli, pamoja na kupendekezwa kuigombea mara tano kati ya miaka ya 1937 na 1948.
Ochen, mwenye umri wa miaka 33, alianzisha taasisi ya African Youth Initiative Network, mnamo mwaka 2005 iliyo na mskani yake huko Lira, Uganda, taasisi iliyo na jukumu la kuwasaidia watu kurudia katika hali yao ya awali wakiwemo wale walioungua kwa moto, ukeketaji wa namna mbalimbali, ubakaji, pamoja na unyanyasaji wa kisaikolojia ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha vijana katika masuala ya uongozi. Hadi sasa taasisi hii imeshapanuka kiasi cha kuwa mtandao wa kimataifa wa wataalamu wa tiba ambao jukumu lao ni kuwasaidia wahanga kujenga upya makazi yao na maisha yao. Kwa mujibu wa This is Uganda:
Kwa kile Victor alichokifanya kwa moyo wake wa dhati wa kujitolea, ndicho kilichomfanya kuwa mmoja wa watu waliopendekezwa kuwania tuzo hii iliyo ya heshima ya hali yajuu. Akiwa kijana mdogo katika kambi ya Abia iliyokuwa na watu zaidi ya 40,000, kambini hapo, aliweza kuanzisha kikundi cha amani akiwa na wenzake. Mkakati huu uliwakasirisha wazee kiasi cha kumuuliza “Kwa nini unaongelea amani ambayo hujawahi kuiona?” Alijitolea; alihatarisha maisha yake kwa kuchoma mkaa ili apate ada ya shule. Baadae alijiunga na elimu ya sekondari ambapo ni mara chache sana alipata muda wa kufanya biashara yake ya mkaa, hivyo alilazimika kuwa fundi viatu, alikuwa akirekebisha viatu vya watoto shuleni. Wakati fulani Victor alijipatia kazi nzuri ya kufanya maboresho ya viatu vya timu ya shule ya mpira wa miguu, kwa bahati mbaya fedha aliyoipata iliibwa. Kusoma kwake kwa bidii na kupendwa kwake na walimu kulimuwezesha kusoma elimu ya upili.
Victor alionesha uzalendo wa kweli kwa nchi yake hata pale alipokuwa akifanya kazi na taasisi ya straight talk foundation ya Kampala, alipokuwa akikutana na watu katika shughuli zake aligundua kuwa watu wa Kaskazini mwa Uganda kuna mengine zaidi walistahili na walihitaji mbali na vipeperushi. Na hili ndilo lililomfanya akaacha kazi yake na kuanzisha Mradi wa Mtandao wa Vijana wa Kiafrika (African youth initiative Network). Mradi huu unazikutanisha jamii na hususani vijana ili waweze kudumisha amani pamoja na kulinda haki za binadamu na kuleta maridhiano. Wanatoa msaada wa saikolojia ya inayohusiana na matatizo ya kijamii, wanatoa msaaada kwa wahanga wa migogoro iliyotokea kipindi cha nyuma, wengi wao wakiwa ni wale walio na maumivu makali ya kihisia na wanaohangaika kupata msamaha, pia wameshasaidia zaidi ya watu 5000 waliokuwa wanahitaji upasuaji wa kurekebisha sehemu za mwili hususani kwa wanawake ambao midomo yao ilikatwa. Mradi huu ambao pia unawawezesha vijana katika shughuli mbalimbali za kuwapatia kipato, umesaidia pia kuaanzishwa kwa klabu 100 amani kaitka mashule na kwenye vyuo vikuu Kaskazini mwa Uganda na zaidi ya vijana 6000 wameshahudhuria mafunzo ya kuimarisha amani na upatikanaji wa waki.