- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Maisha ya Wakenya Yana Thamani, Wanafunzi wa Kiafrika Wasema Kwenye Ibada ya Kuwaombea Wahanga wa Garissa Jijini Beijing

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia Mashariki, Afrika Kusini, China, Kenya, Harakati za Mtandaoni, Maandamano, Uandishi wa Habari za Kiraia, Vita na Migogoro
Participants wrote messages and sealed them in envelopes for the families of the Garissa victims.

Washiriki wa ibada hiyo waliandika ujumbe na kuufunga kwenye bahasha kwa ajili ya familia za wahanga wa mauaji ya Garissa. Picha na Filip Noubel

Kikundi cha wanafunzi, wengi wao wakiwa Wakenya, walikusanyika jijini Beijing mnamo Aprili 18 kufanya ibada isiyorasmi ya kuwakumbuka watu 147 waliouawa [1] kwenye Chuo Kikuu Kishiriki cha Garissa mnamo Aprili 2 kaskazini mwa Kenya.

Wakati vyombo vya habari vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na vile vya China, vilianza kwa kuandika mno habari za Garissa, baada ya muda mfupi, hakuna kilichoendelea. Kama wengi walivyoonesha, mwitikio wa dunia kwa ujumla umekuwa mdogo [2] kwa kulinganisha na matukio ya watu wengi kupoteza maisha yao kwa wakati mmoja hivi karibuni.

Hali hii ya kukosekana kwa taarifa zilizohusiana na shambulio la Garissa liliwafanya wanafunzi wa Kiafrika wanaosoma jijini Beijing kuchukua hatua, pamoja na kuwa maelfu ya kilometa mbali na nchi walizotoka. Kwa sababu hiyo, mnamo Aprili 18 ibada ya kuwaombea marehemu iliandiliwa kwenye bustani ya Chaoyang katikati ya Beijing kuwaenzi marehemu, waathirika pamoja na familia zao.

Ibada kwenye jiji linalozuia maandamano

Beijing ni makazi ya jamii kubwa za wanafunzi wa Afrika, wengi wao wakiishi mabwenini kwenye kampasi za vyuo na huunda familia zenye udugu wa karibu unaowaunganisha raia wa nchi na lugha mbalimbali. Wazo la kufanya ibada hiyo kwa ajili ya wahanga wa Kenya lilianzishwa na tovuti ya Brand South Africa [3] inayoratibiwa na Tebogo Lefifi, kwa eneo la nchi ya China . Tovuti hiyo ilianzishwa kutangaza taswira ya nchi hiyo.

Lefifi anaiambia Global Voices kwamba alihamasishwa na watu wengi kutangaza kwenye mtandao wa WeChat [unaokaribiana na WhatsApp kwa matumizi nchini China] kulalamika kwamba dunia haijaonesha msimamo kuhusiana na shambulio hilo lililopoteza maisha ya watu 147.”

Kwa nyongeza, anasema barua pepe kutoka kwa Africa2.0 Kenya Chapter [4], taasisi kwa ajili ya miradi ya Kiafrika, ikichambua shambulio la Garissa lilimkumbusha kwamba anatokana na kizazi ambacho Afrika imekuwa ikikingoja kwa ajili ya kutekeleza mabadiliko chanya. Hajaridhishwa na kampeni ya kuelimisha watu iliyokuwa ikifanyika kwenye mtandao wa Twita iliyokuwa na jina la #147isnotjustanumber [#147sitarakimuzisizonamajina], akisema kuwataja kwa majina wahnga hakutoshi kuleta mabadiliko chanya. Anaamini ni muhimu sana kuziratibu jamii za Waafrika kupaza sauti kuwaunga mkono rafiki zao wa Kenya.

Hatimaye, ibada ya mkesha iliandaliwa na Lefifi na wanafunzi wengine watatu wa kike raia wa Kenya. Mmoja wao, Tina Kinuthia, anaeleza namna wazo lilivyozaliwa na kufanyiwa kazi:

Tunadhani maisha ya Waafrika na Wakenya yana thamani kubwa, hili haliwezi kusahaulika kiwepesi, kwa hiyo tulianzisha kundi la soga kwenye mtandao wa WeChat ambapo ndani ya muda mfupi tulifikia watu 100 tuliokuwa pia tukisambaza tangazo tulilokuwa tumelitengeneza kwa ajili ya ibada yetu ya mkesha kwa watu tuliokuwa tukiwafahamu. Wengine walitumia mtandao wa WeChat kutuma ujumbe ambao baadae ungeandikwa kwenye kadi za karatasi na kuwatumia wanafamilia wa wahanga. Lakini pia tulikuwa na watu wengi waliokuwa wakijaribu kuhujumu tukio hilo, wakisema tusijaribu kuandaa tukio ambalo halina ruhusa rasmi.

Hatukuwa na fedha, wala mfadhili na hivyo tuliamua kuandaa tukio la saa moja tu ili kukwepa matatizo na tukadhamiria.

Wakati kuandaa ibada hiyo ya wazi kulionekana kama ni wazo jepesi tu la kutekeleza, kwa mazingira ya China, ni kama hakuna uvumilivu wa aina yoyote kwa yeyote anayeonesha hisia hadharani, ikiwa ni pamoja na maombolezo, bila kulazimika kupitia mchakato mrefu na mgumu wa kupata idhini rasmi ya kiusalama. Kwa sababu hiyo, wanafunzi waliamua kuwa wabunifu na kupanga tukio abalo lingewawezesha kuonesha hisia na wasiwasi wao bila kuwaingiza matatizoni washiriki wake.

Poster for Garissa vigil in Beijing.

Bango la ibada ya kumbukumbu ya Garissa jijini Beijing. Picha na Filip Noubel

Waandaaji walisambaza ujumbe kwenye mtandao wa WeChat na kutumia majadiliano ya ana kwa ana na watu ili kujikusanya kwenye viwanja vya Chaoyang [5], moja wapo ya sehemu kubwa zaidi za kibiashara jijini Beijing. Kiutaratibu, kukusanyika watu wasiozidi 500 kwenye viwanja hivyo hakuhitaji ruhusa, wakati kuwa na ibada ya kumbukumbu hata mbele ya ubalozi wa Kenya au kwenye eneo lolote la kibiashara kunahitaji kufuata urasimu mkubwa. Moja wapo ya maelekezo yaliyotolewa kwenye kundi la mtandao wa WeChat yanasema:

Tukio lionekane kama mtoko wa kawaida wa nje kwenye bustani hiyo. Mlete mablanketi.

Mshiriki mwingine alikumbushia kwamba:

Kwa kawaida huwa kuna mkusanyiko wa watu wanaofikia 50 wanaofanya tahajudi kwenye bustani hiyo, na huwa hawalazimiki kupata ruhusa.

Tina Kinuthia anaeleza zaidi:

Tulitaka kuwa na mkusanyiko kwenye eneo la wazi, kwa sababu ibada za maombolezo kama hizi zilikuwa zinaandaliwa Garissa na Nairobi na tulitaka kuwa na matukio yanayotokea kwa wakati mmoja.

Tukio hilo lilihusisha kusomwa kwa mashairi yaliyotungwa na washiriki wenyewe, kuwasha mishumaa ya maombolezo inayoambatana na dakika moja ya kukaa kimya na pia kutengeneza kadi za pole zilizoandikwa kwa anuani za familia za wahanga 147 ambazo zingetumwa nchini Kenya baadae.

Matokeo ya Ibada Hiyo

Around 70 African students gather near an entrance of the park to join the vigil.

Wanafunzi wapatao 70 wa Kiafrika walikusanyika karibu na lango la bustani hiyo kuhudhuria ibada hiyo. Picha na Filip Noubel

Kwa bahati nzuri, hali ya hewa ilikuwa murua alasiri ya Aprili 18, wanafunzi walipoanza kujikusanya kwenye moja wapo ya malango ya kuingilia bustani ya Chaoyang ili kuwakumbuka marehemu wa shambulizi hilo la Garissa. Karibu watu 70, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutoka Afrika na China, walikaa kwenye kona ya mbali ya viwanja hivyo mbele ya picha maalum ya maombolezo wakiwa na mishumaa yao. Kisha, wanafunzi wa Kenya walianza kutoa hotuba zao fupi kuonesha masikitiko yao lakini pia wasiwasi wao kuhusu mustakabali wa jamii ya Wakenya. Wasemaji kadhaa walisisitiza kwamba Kenya lazima ishinde tofauti zilizopo na ijifunze kuishi pamoja bila kujali tofauti za utamaduni, makabila na dini.

Sehemu hiyo ilifuatiwa na kusomwa kwa tenzi kadhaa zilizokuwa zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza mahususi kwa ajili ya ibada hiyo. Utenzi mmoja uliotungwa na Amina Jarso, mwanafunzi wa Kenya anayeishi Beijing, unasomeka kama ifuatavyo:

Roho yake ilitaka kuzungumza,
Kuulizia makosa anayotuhumiwa nayo,
Alitaka kujadiliana naye,
Ikiwa tu angempa muda zaidi.

Macho yake [gaidi] yalikodoa kwa hasira,
Macho yake [mhanga] yalibubujikwa na machozi,
[Gaidi] anapambana kunyamazisha nafsi yake,
[Mhanga] anahangaika afanyeje machozi yasitiririke.

Walitulia kimya kuvuta pumzi pamoja,
Mapigo ya moyo yakienda pamoja,
Risasi kati yao haikutulia,
Imeingilia mkutano wao wa kwanza.

Hebu na tusikilize zaidi kwa ukaribu,
Kwa yale ambayo maneno hayakuyasema,
Na tuwape wale 147 majina yao,
Ili kumbukumbu zao zisipotee kirahisi.

Utenzi mwingine ulisema:

Ninasimama nikiinama chini,
Machozi yakidondoka kwa nguvu kwenye ardhi isiyo na silaha,
Tarakimu ya 147 ikiizonga fikra yangu,
Nikikumbuka hatutawaona tena

Baada ya sehemu hiyo yenye hisia, washiriki waliombwa kuandika ujumbe na kuufunga kwenye bahasha ili ziweze kutumwa kwa njia ya posta kwenda kwa familia za wahanga ili kubeba ujumbe wa matumaini na kuonesha kwamba dunia —hata Beijing—haijawasahau.

Katika hatua hii ya ibada, afisa mmoja wa usalama pale bustanini alifika na kutangaza kwamba mishumaa yote izimwe na watu wote watawanyike kuondoka kwenye sehemu hiyo. Mwanafunzi mmoja alijaribu kujadiliana naye kumwomba asubiri kwa muda mfupi ili wamalize ibada, lakini mlinzi huyo alishikilia msimamo wake na kumjulisha mkuu wake huku akiwaamuru watu wote kutawanyika.

Mtazamo wa Wachima kuhusu shambulio la Garissa na ibada hiyo ya kumbukumbu

Kulikuwa na washiriki 10 wa Kichina kwenye ibada hiyo, mchanganyiko wa wanafunzi, ma-Profesa na marafiki wa Kenya. Tina Kinuthia anaeleza namna walivyopata taarifa na kuamua kushiriki:

Tulipata msaada mkubwa. Mtu anayeendesha kampuni ya usafiri aliona bango kwenye eneo la Jinru Feizhou, akajitolea kulitafsiri na kulisambaza kwenye jamii yake, hivyo ndivyo tulivyowapata baadhi ya washiriki wenzetu wa Kichina.

Mshiriki mmoja alikuwa mwanafunzi jijini Nairobi na anakumbuka maneno kadhaa ya Kiswahili na akasema alikuja kwa sababu alijisikia kuwa:

Nairobi ni sehemu ya nyumbani kwetu, na ninaijali sana Kenya.

Mshiriki mwingine wa Kichina alieleza kwamba:

Watu wengi wanaonizunguka walishangaa, na tulikuwa na mjadala darasani kwetu namna gani tunaweza kuzuia matukio kama haya, na serikali, vyuo vikuu na wanafunzi kila mmoja kwa nafasi yake afanye nini?

Muandaaji mmoja wa Kiafrika alibainisha:

Wachina wanaonekana kujua kinachoendelea, lakini bila jukwaa la kuomboleza wala kuiunga mkono Afrika, hakuna namna wanayoweza kuitumia kujieleza.

Wakati kikundi cha soga kwenye mtandao wa WeChat bado kipp, tukio hilo linafanyika wakati mwingine nje ya mtandao. Ofisi za Africa 2.0 Kenya office zitasambaza kadi kwa familia za wahanga na zimeomba picha iliyotumika kwenye ibada hiyo iwekwe kwenye ofisi za Nairobi kama alama ya mshikamo wa kidunia.