Magazeti mawili yenye umaarufu mkubwa leo katika kurasa za mbele yalihanikizwa kwa habari za kushindwa kwa Saudi Arabia. Habari zili zimetokana na tangazo la Saudi Arabia la kusitisha mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen mapema Jumanne hii. Kayhan, gazeti lililo na uhusiano na kiongozi mkuu wa Kidini, Ayatollah Khamenei, katika ukurasa wake wa mbele lilichapisha picha ya kijana wa Yemen wa Kihouthi akiwa amekalia kitu ambacho kilionekana kama mabaki ya roketi yaliyotokana na mashambuli ya anga ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya wapiganaji wa Houthi. Kichwa cha habari kinasomeka, “Wapiganaji wa Yemen wa Ansar Hezbollah waidhalilisha Israel na Marekani.” Nchini Iran, Wahouthi wa Yemen kwa kawaida hujulikana kwa jina la Ansar Hezbollah”.
Vatan Emrooz, gazeti jingine lenye msimamo mkali lilikisimamia kidete chama cha ‘Peydari Front,’ ambacho ni chama cha kisiasa kilicho na uhusiano na walinzi wa kiuanamapinduzi na majeshi ya Basij katika ukurasa wake wa mbele lilichapisha picha ya kutengenezwa iliyokuwa inamuonesha Mfalme wa Saudi Arabia akiwa ameanguka kwenye kifusi cha jengo lililoharibiwa na ikiwa na maneno, “Pumzi ya Saudi imekufa!”. Unaposema pumzi ya mtu imekufa, huu ni msemo maarufu wa kiajemi unaoonesha kushindwa kwa mtu. Maelezo ya chini yanasema, “Kampeni ya ‘Kimbunga Yakinifu’ yamalizika mara baada ya siku 27 za uhalifu na mauaji ya vichanga na bila ya kufikia hata moja ya matazamio yake”
Fuatilia habari za Yemen katika Global Voice hapa.
Angalizo Kutoka kwa Mwandishi: Huu siyo uchambuzi kamili wa vyombo vya habari vya nchini Iran. Kuvitazama vyanzo vya habari vilivyo na msimamo mkali kama vile Kayhan au Vatan Emrooz kunafanana na kufuatilia Fox News nchini Marekani.