Juma lililopita Chuo Kikuu maarufu cha binafsi nchini Pakistani kililazimika kuahirisha mjadala wa kitaaluma kuhusu haki za binadamu kwenye jimbo la kusini magharibi la Balochistan “kwa sababu ya kuingiliwa na serikali“.
Balochistani, jimbo kubwa zaidi nchini Pakistani, lenye idadi ndogo zaidi ya watu na lenye umasikini mkubwa linashuhudia vuguvugu la tano la kujitenga tangu mwaka 1947. Majadiliano kuhusu vita vinavyoendelea Balochistani ni nadra. Watetezi wa utaifa wa nchi hiyo wanadhani kwamba kimya kwa hali ya mambo jimboni Balochistani ni wajibu wao, wengine wanajihadhari kwa hofu ya nguvu kubwa ya kijeshi iliyopo Pakistani.
Lakini wachache wanaelewa kile kinachoendelea kwenye jimbo hilo, kwa sababu habari zinazoandikwa kutoka kwenye jimbo hilo ni chache mno.
Katika toleo hili la GV Face, tunavunja ukimya kuhusu jimbo la Balochistani kwa kuzungumza na wanaharakati na wanandishi wa Kipakistani na Kibalochi wanaothubutu kuzungumza na kuripoti kuhusu uvunjifu wa haki la binadamu kwenye jimbo hilo. Wanaharakati hawa na waandishi hawa wanafanya kazi kwenye mazingira yenye hatari. Mir Mohammad Ali Talpur (@mmtalpur), mwanaharakati mkongwe wa haki za binadamu alikuwa sehemu ya mjadala wa kitaaluma uliofutwa ataungana nasi. Tutakuwa na Fahad Desmukh (@desmukh), anayeongoza PakVoices, tovuti ya habari inayoripoti kuhusu jamii zinazoishi kwenye maeneo ya pwani ya jimbo la Balochistani, Adnan Amir (@iadnanamir), anayeongoza chapisho la mtandaoni liitwalo Balochistan Point, na Ali Arqam (@aliarqam), mwanaharakati na mwandishi wa gazeti la Newsline
Historia ya hali ya mambo
Habari za kweli kuhusu mgogoro wa Balochistani ni ngumu kuthibitika. Kile tusichokijua ni kwamba wananchi wanaodai uhuru wa Balochistani kutoka Pakistani, na shughuli za kiintelejensia za kijeshi nchini humo zinajaribu kupunguza harakati hizi, wakati mwingine kupitia “kupotea kwa watu” kwa njia zilizo nje ya taratibu za kisheria. Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Pakistani, tangu mwaka 2010, miili ya mamia ya Wabalochistani “waliopotea” wanasemekana kupoteza maisha wakiwa na majeraha ya kuteswa. Mwaka 2013 pekee, miili 116 ilipatikana kwenye jimbo hilo, kati ya hiyo 87 ilitambuliwa na familia zilizotuhumu vyombo vya usalama nchini Pakistani kwa kuwaua wapendwa wao.
Serikali inasema kwamba watu wanaotaka kujitenga wanalipwa na “vikosi vya nje ya nchi hiyo”.
Wanamgambo mbalimbali wa kidini na Kiislamu pia wanatumia eneo hilo kwa kuendesha mafunzo kwa ajili ya kuandaa wapiganaji wa vita nchini Irani na Afghanistani, nchi zote zikiwa kwenye mpaka wa Balochistan. Makundi haya pia yameanzisha mashambulizi ndani ya Pakistani.
Wakati mwingine vikundi hivi vinaunganisha nguvu katika jitihada za kutafuta fedha na raslimali nyingine. Matokeo yake ni watu wanaoishi Balochistani kujilinda wenyewe dhidi ya itikadi mbalimbali za hatari.
Tangu mwaka 2001, maelfu ya kabila la Shia Hazara, ambalo ni kubwa katika makabila madogo yanayopatikana kwenye jimbo la Balochistani, wameuawa na vikundi vya wanamgambo. Wengi zaidi wamelazimisha kulihama jimbo hilo ambalo kwa vizazi vingi limekuwa ndiyo makazi yao.
Baadhi ya makundi ya Wabalochi yanayopigania taifa lao yanajaribu kuwafukuza raia wasio Wabalochi pamoja na vikosi vya kijeshi vya Pakistani nje ya jimbo. Yapo matukio ya wanajeshi wanapigwa mabomu. Familia za Punjabi zinazoishi kwenye jimbo la Balochistani kwa miongo mingi kwa sasa wamepachikwa majina ya vikundi vingine kama “walowezi” wasiohitajika, mamia wakiwa wameshauawa kwenye mashambulio na maelfu wakiwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa sababu ya ghasia.