Afrika Kusini Imejitenga na Waafrika Wengine?

A screenshot of a YouTube video posted by Ren TV showing an attack on an Ethiopian national.

Picha ya video ya You tube iliyowekwa na A Ren TV ikionesha kushambuliwa kwa raia wa Ethiopia.

Mashambulizi ya hivi karibuni huko Kwa-Zulu Natal na Durban yanahusishwa na kauli iliyotolewa na mfalme wa Zulu Goodwill Zwelithini. Inasemekana kuwa aliwataka wahamiaji warudi makwao. Mashambulizi hayo yalihusisha watu kupigwa, kuuawa, kuchomwa moto, wizi madukani pamoja na wizi wa mali za wahamiaji. Watu watano wameshauawa, miongoni mwao akiwamo mvulana wa miaka 14 aliyeuawa siku ya jumatatu. Zaidi ya wahamiaji 1,000 wameyakimbia makazi yao.

Baadhi ya watu wa Afrika Kusini wanawatuhumu wahamiaji kuwachukulia nafasi zao za kazi, biashara, pamoja na kujihusisha na uhalifu.

Kati ya mwaka 2000 na 2008, takribani watu 67 walipoteza maishakwenye shambulio dhidi ya wahamiaji. Mnamo Mei 2008, mfululizo wa machafuko ulisababisha watu 60 kupoteza maisha. Mapema mwezi wa Januari mwaka huu, watu wanne walipoteza maisha huko Johannesburg kutokana na matukio ya aina hii.

Kwa kutumia viungo habari#XenophobicSA na #AfrophobicSA raia wa Afrika Kusini na wale wasio wa Afrika Kusini kwa haraka kupitia mtandao wa Twitter walionesha kuchukizwa na kushtushwa na ukatili uliofanywa na raia wa Afrika Kusini pamoja na Serikali ya Afrika Kusini kushindwa kuchukua hatua kufuatia tukio hili.

Nakaka Ronald, mshauri wa masuala ya Kitekinolojia kutoka Tanzania aliandika:
Falsafa ya kujitolea ya

( Utambuzi wa Mwafrika ni harakati za kisiasa na kifalsafa zilizolenga kumkomboa mwafrika kifikra, harakati zilizoanzishwa na shujaa aliyepinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Steve Biko.)

Oyinlola, mshairi na mwandishi aishiye Ireland, alikuwa na swali kwa watu wa Afrika Kusini:

Enyi watu wa Afrika Kusini, mnafahamu kweli kuwa wapo raia wenu wanaoishi katika nchi nyingine za Afrika?

Ghadafi Ghadafi kutoka Kenya naye aliuliza:

Ninyi mna tofauti gani na wakoloni waliowanyonga hadi kuwaua waafrika au wale wakoloni waliokuwa wakiwabagua waafrika kwa sababu ya rangi yao?

Mtumiaji mwingine wa Twitter, Nyawira Njoroge, aliandika:

Nimekuwa nikifikiri kuwa ninaweza kuishi sehemu yoyote ya Afrika bila tatizo lolote. Ni dhahiri kuwa nilikuwa najidanganya

Akijibu madai kuwa wahamiaji wanachukua nafasi za kazi za wazawa, Abi Mwachi, daktari wa magonjwa ya binadamu huko Mombasa, Kenya, alitoa mapendekezo:

Njia rahisi kabisa ya kupata kazi ifanywayo na mhamiaji ni kwenda shule na siyo kuchukua silaha

Joan Mumbua alihitimisha kuwa Afrika litabaki kuwa bara la ulimwengu wa tatu:

Wakati Kenya ikitumia muda wao mwingi kupambana na ugaidi, XenophobicSA wao wanatumia muda wao mwingi kuwakatili waafrika wenzao. Tutaendelea kuwa bara la ulimwengu wa tatu! Nkt

Kwa upande mwingine, James Chikonamombe, raia wa Zimbabwe anayeishi Amerika, anayaona mashambulizi haya kama ushuhuda wa kushindwa kwa dhana ya umajumui wa Afrika (falsafa ya kisiasa inayosisitiza mshikamano miongoni mwa Wafrikaa):

Umajumui wa Afrika (kwa tafsiri yoyote iwayo) ni jambo gumu kueleweka kwa Waafrika wanaobaguana(kwa tafsiri yoyote iwayo)

Akirejelea tukio la hivi karibuni la kuondolewa kwa sanamu ya kikoloni ya Cecil Rhodes katika Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika ya Kusini, Ashley Mendelowitz alitwiti:

Matokeo ya kuondoa sanamu za kikoloni kumefuatiwa na watu wa Afrika Kusini kuwaondosha waafrika wenzao

Mwandishi wa habari wa Afrika Kusini, Nomsa Maseko aliwaandikia watu wa Afrika Kusini na viongozi wa Kisiasa wa nchi hiyo:

Viongozi wa kisiasa wa Afrika Kusini wapo wapi?, viongozi wa dini na viongozi wa vijana? hamasa ya maadili ipo wapi? kuna mikakati yoyote?

Mtumiaji mwingine wa Twitter aliwafananisha washambuliaji na wanamgambo wa vikundi vya Al Shabaab na Boko Haram:

Hakuna tofauti kati ya Al-Shabaab, Boko Haram na watu waliowachoma moto watoto wakiwa hai

Mshairi wa Zimbabwe, Larry Kwirirayi aliwatahadharisha watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kusambaza taarifa zisizo sahihi:

Wakati kinachotokea Afrika ya Kusini kinasikitisha, kuwa mwangalifu katika kusambaza picha za zamani za machafuko nchini Afrika Kusini& wakizifanya kama vile ni za hivi karibuni

Afrika Kusini ni kama ilivyo Misri, James Chikonamombe aliandika:

Kama ilivyo kwa Misri, Afrika ya Kusini “ipo” Afrika lakini “imejitenga” na Afrika.Huu ni ukweli unaouma, asante kwa miaka 300 ya utumwa wa kifikra.

Akitwiti tokea Afrika ya Kusini, mfuasi wa Afrika isiyo na mipaka aliweka bayana:

Mashambulizi dhidi ya wahamiaji hayahusiani na watu wanaovuka mpaka wa nchi kinyume na utaratibu, kinachotkea ni kulazimishwa kuwachukia Waafrika wenzetu

Mukula na Caroline Kere walijadili namna waafrika walivyojitolea kuhakikisha Afrika ya Kusini inajipatia uhuru wake:

Tulipokuwa elimu ya upili, tulijitolea, tulichanga sh 50, hii ni zaidi ya XenophobicSA,wanawachukia Waafrika wenzao …

Akijazia kilichotangulia kusemwa, AKA alisema:

Wakati vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, walikuwa ni hawahawa wahamiaji waliowahifadhi wapigania uhuru wetu…

Baadhi ya watumiaji wa Twita walikumbushia ukweli kuwa biashara za wahamiaji wazungu hazikushambuliwa.

Tatenande wa kutoka Namibia aliuliza:

Ni maduka mangapi yanayomilikiwa na wageni wa kizungu yameshaporwa?

Hata hivyo, Wadzanai Thembani alihoji:

Wapendwa, mambo yanapaswa kubadilika

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.