Tanzania iko tayari sasa kufanya mabadiliko ya historia kwa kuachana na lugha ya Kiingereza na kuanza kutumia rasmi Kiswahili kama lugha ya kujifunzia na kufundishia katika shule za nchi hiyo.
Sera mpya ya elimu iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mnamo Februari 13, 2015, inayokwenda sambamba na Mpango wa Taifa Kuelekea 2025 inarefusha elimu za msingi kutoka miaka saba ya sasa mpaka miaka 11, na kuifanya elimu hiyo kuwa bure ikiwa ni pamoja na kuondoa mtihani wa taifa kwa wahitimu wa elimu ya msingi kuingia sekondari.
Hatua hii inaonekana kuwa mojawapo ya maamuzi ya kwanza kwamba nchi ya Afrika inaamua kufundisha wanafunzi wake kwa ngazi zote kwa kutumia lugha ya ki-Afrika badala ya lugha za kigeni.
Akitoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya lugha, Atetaulwa Ngatara, naibu mkurugenzi wa sera katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alisema Kiingereza kitaendelea kufundishwa kama lugha, na kwamba wanafunzi kujifunza Kiingereza haitamaanisha kuwa ni lazima masomo yote yafundishwe kwa lugha hiyo.
Makala kuhusu mabadiliko hayo ya sera iliyowekwa kwenye mtandao wa Facebook naOliver Stegen, ambaye ni mzungumzaji wa Kiswahili mwenye asili ya Ujerumani na mshauri wa lugha wa shirika lisilo la kibiashara linaloshughulika na ukuzaji wa lugha SIL International, iliibua hisia mchanganyiko.
Nancy Petruzzi Maurer alitania kwa salamu ya Kiingereza iliyokosewa:
“Goood mauning teacha!” Hakuna zaidi
Paul A Kijuu alitoa maoni kwa Kiswahili akisema kwamba Kiingereza kimegeuza tabaka la wasomi kuwa maroboti:
Kwa upande wangu, Oliver Stegen mimi naona hii ni hatua nzuri sana. Shida yetu ni kulalamika. Elimu inapaswa itolewe kwa lugha inayoeleweka kwa mtumiaji. Kiingereza hakitusaidii zaidi ya kutufanya maroboti. Wasomi wetu hawafikiri kwa kujitegemea kwa sababu hakuna walichojifunza wanachokielewa.
Vera Wilhelmsen alibainisha kwamba ingawa si kila mtu anahitaji kufika Chuo Kikuu lakini kila mmoja anastahili elimu bora ya msingi:
Ninadhani ni muhimu kutafakari aina gani ya elimu ya msingi itawanufaisha watu wengi. Ni bayana kwamba mpaka leo hii si watu wengi wanafanikiwa kufika sekondari, na ni wachache sana wanahitimu elimu hiyo. Kuna tatizo pale ambapo si wanafunzi wala walimu wameandaliwa kubadilika kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza katika shule ya Sekondari. Ni kweli, tunapaswa kutazama athari zake, lakini ninaamini hii ni hatua nzuri ya mafanikio. Si lazima kila mmoja afike Chuo Kikuu, lakini raia wote wanastahili elimu bora ya msingi!
Hata hivyo, si kila mmoja aliafiki mfumo huo mpya wa elimu. Steve Nicolle alibainisha uwezekano wa athari ya sera hiyo mpya ya elimu:
Ninahisi athari ya sera hii itakuwa kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika shule binafsi ambazo zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Chunguzeni sana mtaona wanasiasa wakifungua shule mpya zinazofundisha kwa Kiingereza katika siku za hivi karibuni!
Elly Gudo alikubaliana na Steve Nicole, akidhani kwamba wanasiasa watakuwa wanufaika wakuu wa sera hii:
Ninakubaliana na wewe kabisa Steve Nicolle. Kwa kuishi hapa Tanzania, ninaweza kukuambia kwa hakika kwamba wanasiasa watakuwa ndio wanufaika wakuu wa sera hii ya elimu. Wengi wa wa-Tanzania wa tabaka la kati na la juu ambao wanahusudu utandawazi watafanya kila wanaloweza kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinazofundisha Kiingereza. Mtoto wa masikini ndiye atakayekuwa mwathirika mkuu utakapokuja wakati wa kujiunga na Chuo Kikuu na hata pale anapoanza kutafuta kazi. Baada ya miongo miwili, nchi [hii] itakuwa na matabaka yaliyo wazi. Tanzania inahitaji mapinduzi kama yale ya Ufaransa katika sura nyingi.
Akipinga sera hiyo, Muddyb Mwanaharakati alisema yafuatayo kwa Kiswahili:
Oliver Stegen usichekelee. Wametia siasa ndani yake. Watoto zao wanasoma international schools [shule za Kimataifa]. Sisi akina kajamba nani tutasoma zilezile S.t vichochoroni ili tubaki na Kiingereza chetu cha ya, ya, yes no yes no. Wakati watoto wao wanamwaga ngeli ya maana. Sijaifurahia hatua hii. Kwetu bado sana Oliver hata matangazo na sehemu nyingi ya masuala ya serikali yapo Kiingereza.
Josephat Rugemalira alibaini kwamba sera mpya haina mabadiliko makubwa kinyume na watu wanavyofikiri:
Unahitaji kusoma kwa makini sera inavyosema: Inasema Kiswahili kitafundishwa katika ngazi zote na PIA inasema Kiingereza kitaendelea kutumika katika ngazi zote (maana yake ni pamoja na shule ya msingi). Kwa hiyo tafsiri yangu ni kwamba jambo pekee jipya linalowezekana kupitia kauli kama hizi ni kuwepo kwa uwezekano kwamba sasa baadhi ya watu wanaweza kuanzisha Shule za Sekondari zinazofundisha kwa Kiswahili, na kwamba sasa ni rasmi mamlaka za serikali za mitaa zinaweza kugeuza shule za msingi zilizopo kuwa za Kiingereza.
Akijibu makala hiyo hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa Trending Kenya, Margaret Njeru alieleza kwamba mfumo huo mpya wa elimu haipigi teke lugha za kigeni bali kuziweka katika nafasi sahihi katika mafunzo:
Kwa hakika, hatua hii ni ya kijasiri na ni mwelekeo sahihi. Elimu ni maendeleo, na maendeleo yanaweza kuja tu kupitia lugha inayoeleweka vizuri kwa watu. Duniani kote, hakuna nchi zinazosemekana kuwa zimeendelea zinazotumia lugha za kigeni. Matumizi ya lugha za wakoloni waliotawala nchi nyingi za Afrika yamechangia kubaguliwa kwa wananchi wengi katika mchakato wa maendeleo. Kama tunapaswa kutafsiri njia ya maendeleo ‘yetu’, basi uchaguzi wa lugha lazima uende sambamba na njia hiyo. Na hii haimaanishi kwa vyovyote kuzipiga teke lugha za kigeni (au zile tunzojifunza ukubwani), badala yake ni kuziweka katika nafasi inayozifaa katika ufundishaji na ujifunzaji.
Kwame Aboagye alisema ni wakati sasa wa-Afrika watumie lugha zao wenyewe:
Wakati umewadia nchi zetu za ki-Afrika ziongee lugha zetu wenyewe kama vile ki-Twi, ki-Yoruba, ki-Swahili na ki-Mandingo. Kiingereza hakikuwa lugha yetu ya asili na tunahitaji kuamka na kurejea misingi yetu wenyewe kwa fahari.
Mabadiliko hayo ni ya kihistoria lakini yanakuja na changamoto kadhaa, kama alivyobainisha Christina Higgins:
Habari njema kabisa. Sasa jaribio kubwa litakuwa namna ya kutafsiri kwa Kiswahili vitabu, mitihani na zaidi. Pamoja na changamoto zake, mabadiliko haya ni ya kihistoria.
1 maoni
kuna sentensi moja ninayotaka kuiachia hapa:
During this period (1885-1919) Kiswahili was the medium of instruction throughout the school system in the colony (Rubagumya 1989/1990:6).
nataka kusema pia baada ya kupata uhuru ni fahari kubwa kwa Tanzania, pia kwa wananchi wote wa Tanzania kwani
tanzania ndiyo nchi ya kwanza katika bara afrika kuchukua lugha ya kiafrika kuwa mojawapo ya lugha zitumikazo kama lugha ya shule yaani “language of instruction”