Mradi wa Video Waelezea Mapambano ya Kimaisha ya Watu wa Papua ya Magharibi

Photo from Papuan Voices, used with permission.

Picha kutoka Kwenye Video ya “Sauti za wa-Papua, imetumiwa kwa rushusa.

Sauti za wa-Papua ni mkakati wa utetezi kupitia uandaaji wa video unaowawezesha wanaharakati wa Papua ya Magharibi kutengeneza filamu fupi zinazosimulia habari zao pamoja na kuelezea harakati za maisha yao ya kila siku.

Vyombo vikuu vya habari ni nadra sana kuzungumzia lolote kuhusiana na maisha ya watu wa Papua ya Magharibi, moja ya majimbo ya Indonesia. Waandishi wa habari wanapolitupia jicho eneo hili, mara nyingi wamekuwa wakizungumzia mgogoro wa kisiasa uliopo kati ya serikali ya Indonesia na harakati za uhuru wa Papua ya Magharibi. Mradi wa Sauti za wa-Papua unawajulisha wasomaji mambo mengine yanayohusu utamaduni na historia ya watu wa Papua:

Simulizi hizi hazina uhusiano wa moja kwa moja na harakati za Papua ya Magharibi za kujitafutia uhuru; siyo habari za mgogoro ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo zimekuwa zikisambazwa. Hizi ni habari tofauti na mgogoro wa kisiasa unaoendelea: Ni kuhusu juhudi katika elimu, mazingira, usawa na utu.

Mradi wa Sauti za wa-Papua ni ushirikiano kati ya EngageMedia na Haki, Amani, na Uaminifu wa Ubunifu. Mradi huu  unafanya kazi na mashirika ya wazawa katika maeneo ya Jayapura na Merauke huko Papua ya Magharibi, ambapo wanaharakati wazawa walihudhuria warsha ya njia za upashanaji habari na kujifunza namna ya kuelezea kupitia video habari ambazo si rahisi kufikiwa. Hii imepelekea kuandaliwa kwa matoleo mawili ya video yaliyowahusisha waandaaji kadhaa wa filamu ambao ni wazawa na pia, zikiwa zimesheheni habari za kipekee za kijamii, kitamaduni, pamoja na hali ya kisiasa ya Papua ya Magharibi.

Waandaji wa mradi huu wanategemea kuwa “habari hizi zitawapa watu wengine hamasa ya kujifunza na kuchukua hatua, na hivyo kupelekea sauti za watu wa Papua Magharibi kusikika.”

Tayari kuna picha zilizopigwa kutoka katika baadhi ya video hizo katika maeneo mengine ya Indonesia. Moja ya filamu maarufu ni ile ya Mutiara Dalam Noken (Lulu ndani ya Noken), inayozungumzia habari ya daktari Mia, “Mwanamke wa Papua aliyejitolea kuwatibu wagonjwa pamoja na wale wanaoelekea kukosa haki zao za kiraia katika maeneo ya ndani sana ya Papua ya Magharibi.”

pearl_in_the_noken

Picha kutoka kwenye video ya “Sauti za wa-Papua.”

Video nyingine maarufu ni ile inayozungumzia zaidi nyumba za jadi aina ya Honai, ambazo ni kitovu cha maisha ya watu katika maeneo ya uwanda wa kati, iliyo na lengo mahususi la kuhifadhi urithi huu wa kiutamaduni.

honai

Picha kutoka kwenye video ya “Sauti za wa-Papua.”

Mtayarishaji wa Filamu,Patricio Wetipo alisaidia kuandaa video ya Sauti za wa-Papua  inayohusu madhila wanayokabiliana nayo wanawake wachuuzi. Katika kutoa maoni yake, Wetipo alilalamikia suala la ukatili dhidi ya wanawake kutokuripotiwa ipaswavyo.

Vyombo vya habari vinazungumzia tu masuala ya siasa pamoja na ukatili wa wanajeshi. Hakuna hata mmoja anayezungumzia ukatili dhidi ya wanawake.

Video ya Wetipo's inategemewa kuonesha hali ngumu ya maisha inayowakabili wanawake wa Papua:

Ninataka kuuonesha ulimwengu kuhusu maisha ya wanawake wa Papua. Wanafanya kazi kwa bidii sana na bila ya kupata usaidizi wowote kutoka kwa wanafamilia wenzao. Hata waume wao huwa hawawasaidii kubeba mizigo pindi wanapoelekea sokoni. Ni mategemeo yetu kuwa watu wataona filamu hizi na na kupata hamasa ya kuwasaidia kubadili maisha yao.

areca_nuts

Picha kutoka “Sauti za wa-Papua.”

Video nyingine inazungumzia utamaduni wa Wamena, mahususi ikilenga wanyama aina ya nguruwe na ishara yao muhimu kwa watu wa vijijini.

Jina lenyewe, Wamena linatokana na neno ‘Wam’, likiwa na maana ya nguruwe, na ‘Ena’, likiwa na maana kufuga. Kila maadhimisho ya hatua fulani ya maisha huambatana na kukabidhiwa nguruwe, na pia, utajiri wa familia hupimwa kwa wingi wa nguruwe katika familia. Nguruwe pia ni ishara ya amani miongoni mwa makabila ya watu wanaoishi maeneo ya kati ya uwanda wa juu. Hii inamaanisha kuwa, panapotokea ugonjwa unaosababisha vifo vya nguruwe wengi, ni dhahiri kuwa pia kutakuwa na anguko kubwa lamkiuchumi miongoni mwa jamii ya watu wa Wamena.

Video hii inaonesha uhusiano wa karibu kati ya nguruwe na watu pamoja na madhara kwa jamii kutokana na nguruwe wengi kufa kwa ugonjwa:

wamena

Picha kutoka kwenye video ya “Sauti za wa-Paupa.”

Sauti za wa-Paupa ni mradi unaoisadia jamii kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo watu wa Papua nchini Indonesia. Pia, ni moja ya miradi inayotukumbusha kuwa tunapaswa kujituma zaidi kwa kufuatilia na kusambaza habari kuhusiana na maisha ya wa-Papua wa kawaida mbali na kuelezea tu kwa mapana harakati za kisiasa za kutaka haki na usawa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.