Pengine hatukuweza kuonekana kutokea angani, kama ilivyo kwa Ukuta Mkubwa wa China. Lakini kwa bahati nzuri kifaa mithili ya eropleni kilichofungwa kamera kiliweza kutuchukua picha za video tukiwa mbele ya Jengo la Provincial Capital la Mamlaka ya Jiji la Cebu majira ya mchana wa Januari 25, 2015, kikiwa umbali wa mamia kadhaa ya futi tokea ardhini, tukiwa ni sehemu tu ya wanajamii wa Global Voices tuliokuwa tumekusanyika katika muonekano wa kipekee kabisa-na ikizingatiwa namna tulivyokusanyika hivyo kwa haraka-mpangilio wa mstari mmoja na mduara uliowakilisha miaka 10 ya kuwepo kwetu.
Tulifikisha miaka 10 mwezi Disemba, kwa hiyo Mkutano Wa Dunia wa Uanahabari wa Kiraia wa sita uliofanyika mwezi Januari huko katika jiji la Cebu, nchini Ufilipino, ulikuwa ni fursa nyingine ya kusherehekea, hata hivyo, ni masikitiko yetu kuwa hatukuweza kuadhimisha siku hii tukiwa na wanajamii wote hai zaidi ya 800 waliopo hadi sasa.
Ikiwa ndio wakati pekee wa jamii yetu hai kukutana ana kwa ana, Mikutano yetu ifanyikayo kila baada ya miaka miwili ni ya muhimu sana kwa maendeleo ya jumuia yetu. Mkutano wa mwaka 2015 ulihusisha siku nne za mikutano ya ndani, na ulihitimishwa kwa kongamano la wazi lililofanyika katika jengo la Provincial Capitol la Mamlaka ya Jiji la Cebu lililojadili dhana kuu ya Uhuru wa Mtandao wa intaneti. Uhuru wa Kujieleza, Haki ya kila Mmoja. Kongamano lilifunguliwa kwa namna mahsusi iliyowagusa watu kwa wanajamii wa Global Voices kusoma tamko la kushinikiza kuachiwa huru kwa wanahabari wa mtandaoni na wanaharakati waliofungwa jela. Pia, katika kongamano hilo, walitangazwa washindi wa shindano la kuandika insha lililofadhiliwa na Google.
Tuna wengi wa kuwashukuru kwa kufanya mkutano wetu wa mwaka 2015 kuwa wa mafanikio:
Wawasilishaji mada wetu, kwa kutushirikisha ujuzi wenu bila hiana katika mafunzo wakati wa mkutano (fuatilia taarifa na video kwenye tovuti ya Mkutano).
Shukrani za dhati kwa Wawakilishi, ambao walikuja kutoka katika maeneo ya karibu na ya mbali katika nchi ya Ufilipino, na pia wote waliokuja kutoka katika maeneo mengine Duniani kwa lengo la kushiriki mkutano huu.
Shukrani za dhati kwa Wafadhili wetu wa kimataifa: Ford Foundation, MacArthur Foundation, Google, Open Society Foundations, Knight Foundation, Yahoo! na Automattic.
Na pia, mkutano wetu usingeweza kufikia mafanikio haya bila ya ushirikiano wa kipekee tulioupata kutoka kwa wenyeji wa tulipofanyia mkutano. Shukrani zetu za dhati kabisa ziwaendee wafadhili wetu wa masuala ya habari SunStar Publishing, pamoja na wafadhili wetu wa mawasiliano Globe Telecom na Smart Communications. Pia, shukrani zetu za dhati ziiendee Mamlaka ya Jiji la Cebu kwa kuturuhusu kutumia jengo lao tukufu la Provincial Capitol kwa muda wa siku mbili. Pia, tunatoa shukrani za kipekee kwa Idara ya Utalii ya Ufilipino kwa ukaribisho mwanana wa maadhi ya Kifilipino na kwa sherehe iliyofana ya kuhitimisha mkutano, iliyofanyika Museo Sugbo. Shukrani za kipekee pia ziwaendee Doris Isubal-Mongaya na timu yake ya PRWorks kwa kutumia maarifa na ujuzi wao wa hali ya juu uliofanya maisha yetu ya Cebu, kwa namna kadha wa kadha, kuwa ya kipekee sana-pia tunashukuru sana kwa zawadi ya video iliyochukuliwa kutokea angani.
Na tunasonga Mbele na Juu Zaidi kwa Mafanikio.