Asasi ya Kiraia Inayofuatilia Bunge Yawaunganisha Wabunge Wanawake na Wananchi wa Uganda

Uganda's parliament in session. Photo by

Bunge la Uganda likiendelea na kikao. Picha imetumiwa kwa ruhusa ya Taasisi ya Parliament Watch Uganda.

Wananchi wa Uganda wanatumia vizuri mitandao ya kijamii kuwasiliana na wabunge wao, kwa msaada wa Parliament Watch Uganda, taasisi inayofuatilia shughuli za Bunge la Uganda na kisha kutoa takwimu zinazohitajika pamoja na uchambuzi wa kitaalam.

Mnamo Februari 26, 2015, taasisi hiyo iliandaa  Mjadala ulioitwa #MPsEngage  na kufanyika kwenye mtandao wa Twita ili kuwapa fursa wabunge wanawake kuzungumzia mada iliyoitwa, “Kuwafanya Wanawake Wathaminike kwenye Mchakato wa Kibunge’. Wahudhuriaji walikuwa wa aina tatu na kwa wakati ule ule: Watu wa Gulu kaskazini mwa Uganda, wabunge wanawake wa Uganda na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uganda.

Gulu ni wilaya iliyokuwa na misuguano Kaskazini mwa Uganda. Kilikuwa ni kitovu cha mgogoro kati ya serikali ya Uganda na waasi wa  Lord’s Resistance Army (LRA). Wanawake wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni athari za vita na kupuuzwa na serikali kuu.

Wahudhuriaji kutoka Gulu waliuliza maswali kupitia vinasa sauti, na wataalamu wa mitandao ya kijamii walitwiti maswali hayo kwa wabunge.

Wakati wa majadiliano hayo, wabunge wanawake walitakiwa kuelezea mafanikio na changamoto walizokabiliana nazo wakati wote wa kipindi cha uongozi wao.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walitoa maoni, kunukuu na kuwaelekeza wafuatiaji wao kwenye alama ishara ya majadiiano hayo ambayo ilikuwa ni #MPsEngage.

Je, wanawake nchini Uganda wanapata ushiriki katika katika michakato yote ya kisiasa na kufanya maamuzi nchini Uganda?

Mwandishi wa Uganda, ambaye pia ni mwanablogu Raymond Qatahar alikuwa na haya ya kuchangia:

Ninafuatilia majadiliano ya #MPsEngage. Nina furaha kwamba hatimaye, suluhisho ya kiteknolojia limepatikana na kuwaunganisha wabunge na wananchi

Jackie Asiimwe, Mwanasheria ya Uganda, aliuliza:

Ni lini tutapata fursa ya kuwauliza wabunge wanaume namna wanavyoshughulikia masuala ya wanawake, kwa sababu na wao pia walichaguliwa na wanawawakilisha wanawake

Kollin Rukundo aliibua suala la muswada wa ndoa na talaka Muswada huo, pamoja na mambo mengine, unawalazimisha wanandoa kuwa na umiliki sawa wa mali zao, na kuwafanya wenzi wanaoishi pamoja bila ndoa kuwa na haki za kumiliki mali na pia unafanya ubakaji unaofanyika kati ya wanandoa kuwa kosa la jinai:

Kwa kurejea muswada wa Ndoa na Talaka, “Namna gani Mbunge anaweza kuchukua kipengele kimoja (talaka) na kukitumia kupinga muswada mzima?

Akimnukuu Miria Matembe, waziri wa zamani wa maadili na uadilifu, Jackie Asiimwe alisema:

Wabunge hawatumii mamlaka yao ipasavyo. Badala yake wanafanya kazi za Serikali -kujenga shule, kununua madawa – Matembe

Daniel Turitwenka, mshauri mwelekezi wa mitandao ya kijamii, aliweka picha ya mshiriki wa Gulu, kaskazini mwa Uganda, akishiriki moja kwa moja kwa njia ya simu wakati wa mjadala huo:

Wakazi wa Gulu walikuwa na majadiliano ya moja kwa moja kwa njia ya simu na Mwenyekiti wa Asasi ya UWOPA, Betty Among – maswali yalijibiwa na moja kwa moja

Alimnukuu mmoja wa washiriki:

Bw Okello anasema kutengana kwa watoto na wazazi ni suala gumu na aliwasihi @pwatchug kuendelea kuwaleta wabunge wajibu maswali

Wakazi wa Gulu walijitahidi kufanya mahitaji yao yafahamike:

Hapa Gulu kila mmoja lazima apate huduma za afya ya uzazi. Bado wanawake wengi hawana huduma hizi

Suala la huduma duni za ukunga lililalamikiwa:

Wanawake wetu wengi wanapoteza maisha mchana na usiku kwa sababu ya kukosekana kwa wakunga! Hali hii haivumiliki!

Ingawa mazungumzo hayo yalifanyika kwenye mtandao wa Twita, Denis R Tumusiime alibaini kwamba wabunge wanawake bado hawajaweza kutumia vizuri mitandao ya kijamii kufanya shughuli zao:

Bado sijaona twiti kutoka kwa mbunge mwanamke

Wakati mjadala huo ukielekea ukingoni, Jackie Asiimwe, ambaye ni mwanasheria, alishauri kwamba ushiriki huo usiishie hapo:

Muda wetu unakaribia kuisha, lakini mazungumzo yaendelee. Lazima tuwasiliane na wabunge wetu muda wote

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.