Wanawake wa Kiislam na Kikristo Nchini Nigeria Walivyoungana Kupambana na Misimamo Mikali ya Kidini

Nigerian pastor Esther Ibanga joined with Muslim leaders in the city of Jos to call for the return of Chibok girls who were kidnapped by the extremist group Boko Haram. Credit: Women Without Walls Initiative (Willie Abok). Published with PRI's permission

Mchungaji wa ki-Naijeria Esther Ibanga akiwa na viongozi wa Kiislam mjini Jos kutoa mwito wa kurudishwa kwa wasichana wa Chibok waliokuwa wametekwa na kikundi cha kigaidi kiitwacho Boko Haram. Picha: Women Without Walls Initiative (Willie Abok). Imechapishwa kwa ruhusa ya PRI

Makala haya na taarifa ya redio ya  Joyce Hackel wa Kipindi cha The World yalichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa PRI.org mnamo Januari 14, 2015 na yamechapishw atena kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana maudhui.

Wakati macho yote yakiwa yameelekezwa Ufaransa juma lililopita, shambulio la kigaidi lililofanywa na magaidi wa kidini na kukatisha maisha ya watu wengi katika mji wa kaskazini mashariki mwa Naijeria uitwao Baga halikupata kutangazwa na vyombo vingi vya habari duniani.

Kukosekana kwa habari kwa makusudi namna hiyo hakukubaliki kwa wa-Naijeria. 

Esther Ibanga, mchungaji wa mji wa Jos na mwanzilishi wa kikundi kiitwacho  Wanawake Wasio na Mipaka, anasema alitegemea dunia ingetazama kwa uzito ugaidi unaofanywa na kikundi cha Boko Haram kinachochukua mamia, na pengine maelfu ya maisha ya wa-Naijeria.

“Nilikasirika sana moyoni mwangu. Lakini hasira yangu ilikuwa dhidi ya serikali yangu,” anasema Ibanga, mchungaji wa kanisa la Jos Christian Missions. “Kwa sabbau serikali yangu na watawala wake wanapaswa kuthamini watu wao wenyewe. Kama huthamini watu wako mwenyewe kwanza, kwa nini utarajie mtu mwingine awathamini?”

Jos ni mjini kuu wa Jimbo la Plateau kwenye ukanda wa kati wa Naijeria. Uko mamia ya maili kusini mwa ngome ya Boko Haram kwenye Jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Naijeria. Misuguano ya kidini katika uakdna wa kati imeanza siku nyingi kabla ya kufahamika kwa Boko Haram katika miaka ya 1990.

“Ni bahati mbaya sana, lakini kwa miaka kadhaa sasa ni kama tumeanza kuzoea, kwamba wa-Kristo na wa-Islam hawapatani,” anasema Ibanga. 

Hata baada ya misuguano hiyo kuzoeleka, kiwango cha mauaji ya mwaka 2010 kwenye mji wa Dogo-Nahawa kulimfanya Ibanga na wanawake wengine wa sehemu hiyo kuwa wanaharakati wanaopaza sauti.  

“Vita imeenea mpaka kwenye vyumba vya kulala,” anasema. “Kijiji kilichoshambuliwa, washambuliaji walienda mpaka vyumbani walikolala watu usiku na kuanza kuwaua.”

Matokeo yake, Ibgana aliwaratibu wanawake 100,000, wengi wao wakiwa wa-Kristo, kuandamana katika mji wa Jos. Wazo, anakumbuka, lilikuwa “kuifanya serikali ijue kwamba wanawake kwenye Jimbo hilo hawakuwa tayari kuendelea kunyamazia vitendo hivyo” 

Lakini katika majuma yaliyofuata, Ibanga na wengine waligundua kwamba ghasia hizo za kigaidi katika eneo la Dogo-Nahawa zilikuwa kwa hakika mashambulio ya kulipiza kusasi -kujibu shambulio la awali lililofanywa na wanamgambo wa ki-Kristo. 

“Wanawake wa ki-Islam waliitikia na kusema, ‘Jamani, subiri kidogo, mbona watu wetu wenyewe wanauawa pia,'” anakumbuka. Kw ahiyo wanawake wa Kiislam mjini Jos waliamua kufanya mkutano wao wenyewe. 

Lakini hata baada ya maandamano ya wa-Kristo na wa-Islam, mapigano yameendelea. Hali ilipofikia hapo, Ibanga aliamua kukutana na kingozi wa dini ya ki-Islam wa eneo hilo, Khadija Hawaja. 

“Hapo ndipo nilipotambua kwmaba suala halikuwa dini, bali siasa. Lakini dini ilitumiwa kama silaha yenye nguvu,” anasema. “Nilimfuata na kusema, ‘Hebu sikia, unajua sisi hatuwezi kuwa tatizo la mwenzake. Wala suala sio wewe kuwa Muislamu au mimi kuwa Mkristo. Hawa wanasiasa wanatugonganisha vichwa vyetu. Na nia yao ni kuendelea kubaki madarakani.'” 

Kwa sababu Jos ilikuwa imeathirika sana kisiasa, wanawake hao walikutana katika ‘eneo lisilo na upande’ — hotelini. 

“Angeuawa,” Ibanga anasema. “Na ningeuawa pia, kwa kwenda tu kwenye jamii ya ki-Islam.”   

Baada ya miezi ya kushirikiana, Ibanga na Hawaja walianzisha Mradi wa Wanawake Wasio na Mipaka. 

“Tunataka kuachana na mipaka inayotutenga na kutugawanya, iwe ni mipaka ya matabaka ya kijamii au mipaka ya kidini,” alisema. “Hatuwezi kuungana na wanasiasa kwenye vita hii. Sisi ni akina mama. Sisi tunatengeneza uhai na tunatafuta majibu. Na tunadhani kwmaba lazima tuje na majibu ya matatizo, badala ya kuishi kwenye matatizo.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.