- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Miaka 50 Baadae, wa-Zambia Wanajiuliza Nini Maana ya Uhuru

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Zambia, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Utawala
Zambia's National Freedom Day last year in Lusaka. October 24, 2013, photo by Owen Miyanza. Demotix. [1]

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Zambia mwaka jana jijini Lusaka. Oktoba 24, 2013, picha na Owen Miyanza. Demotix.

Zambia ilisherehekea  jubilee ya miaka 50 [2] juma lililopita tarehe 24 Oktoba. Maadhimisho ya siku ya uhuru kwa mwaka huu yameweka historia ya kuwa maadhimisho ya kwanza kufanyika katika miaka 50 bila kuhudhuriwa na rais aliye madarakani kufuatia Rais  Michael Sata kuwa nje ya nchi katika kile wasaidizi wake wanachokiita “uchunguzi wa afya yake [3].”

Wakati wa-Zambia duniani kote wakisherehekea siku kuu hiyo kwa vyakula, rangi rasmi za nchi hiyo na chochote walichoweza kukifanya, baadhi ya wachunguzi wa mambo waliibua maswali mazito kuhusu historia na mustakabali wa nchi hiyo.

Zambia's official golden jubilee logo. [4]

Nembo rasmi ya sherehe hizo za uhuru wa miaka 50 ya Zambia.

Ukosoaji mkubwa ulitoka upinzani: kiongozi mkuu wa chama cha United Party for National Development (UPND) Hakainde Hichilema aliyetoa wito [5] kwa watu kuvaa nguo nyeusi kuomboleza na sio kusherehekea tukio hilo:

Kipi ambacho wapigania uhuru wetu wanaweza kujivunia kwa kuwa uhuru kwa miaka 50? Leo tunasherehekea nini? Tangu chama PF kiingie madarakani kwa ahadi za uongo na udanganyifu, taifa limeshuhudia unyanyasaji, nchi imeshuhudia kukiukwa kwa haki za binadamu, uhuru na kujiamulia mambo yetu, tumeshuhudia habari zikitangazwa kwa upendeleo mkubwa, ukatili wa polisi, matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi vyote ambavyo sikuwahi kufikiri baada ya mwaka 1991 ningekuja kuyaona kwa ghasia nyingi za kisiasa kiasi hiki.

Baadhi ya wa-Zambia wanaotumia mitandao ya kijamii [6] hawakukubaliana na Hichilema, aliyetumia siku nzima ya uhuru kuwafariji wenye shida na  kugawa magunia ya [7] mahindi na mafuta ya kupikia, lakini haikuwa  Canicius Banda, mmoja wa makamu rais wawili wa chama UPND waliovutia watu wengi kwenye sherehe za miaka hamsini ya uhuru kwa swali waliloliwekwa kwenye mtandao wa Facebook. Banda aliwapa changamoto wananchi kufikiri kwa kina kuhusiana na sherehe hizi, , akihoji kama siku ya uhuru inasherehekewa kwa kupitisha muda tu, aukwa mafanikio ya nchi tangu  kupatikana kwa uhuru miaka 50 iliyopita, mwaka ambao  Rhodesia Kaskazini ilipojibadilisha kuwa  Jamhuri ya Zambia. Aliandika [8]:

KUHUSU JUBILEE YA MIAKA 50 YA ZAMBIA [Tukio la kufurahia kupita kwa miaka na SIO mafanikio/Ratiba ya vyama]: Vernon Mwaanga, mmoja wa wapigania uhuru wa Zambia na mwanasiasa mwandamizi, katika kitabu chake, The Long Sunset [Machweo marefu] anasema kama ifuatavyo: ‘wakoloni walituacha miaka 40 iliyopita na kama ilivyo kawaida ya nchi za ki-Afrika hatuwezi kuendelea kuwalaumu wakoloni kwa matatizo yetu. Utumwa ni historia iliyopita. Sasa lazima tugeuze nchi zetu ili zipige hatua za kimaendeleo, huku tukisaisha makosa yetu, twapaswa kusonga mbele…’ Makamu wa Rais wa Jamhuri Dr Guy Scott, miaka hamsini baada ya uhuru, juma moja tu lililopita alipokuwa akizungumzia bajeti ya serikali ya mwaka 2015 alisema: ‘Vipaumbele vyetu vya taifa vimepinda. Badala ya kupambana na ukosefu wa ajira sisi tunapambana na mfumuko wa bei ubaki kuwa tarakimu moja; wakati huo huo wananchi wanaoishi kwenye mabwawa ya Lukanga wanaishi kwa [kula] nge. Hili si sahihi.’ Bw Alexander Chikwanda, Waziri wa Fedha, majuma machache yaliyopita alitamka maneno yafuatayo: ‘Tumeshindwa kuendelea nchi hii kwa sababu ya uongozi ulioshindwa.’ Bw Chikwanda yuko sahihi na ameelewa tatizo letu. Wakati tunaanza miaka mingine 50, tunahitaji kizazi kipya cha vijana, chenye uzalendo, uelewa, busara na chenye kumcha Mungu. Haya ndiyo maombi yetu. Bwana tusikie! Na tuna uhakika kwamba utajibu maombi yetu. Hizi nyakati za undanganyifu na ulangai lazima zifikie mwisho!

Michael Chishala, akichangia kwenye tovuti ya habari mtandaoni iitwayo Zambian Watchdog, aliandika [9]:

Baada ya miaka 50 ya kujitawala, ni aibu kuwa takwimu za uchumi wetu zinafanana na zile za nchi zenye machafuko vya vita, na nyingine zinafanya vizuri kuliko sisi katika maeneo mengi. Kila serikali mpya ya Zambia huja na lawama kwa jambo fulani badala ya kujikagua yenyewe pale iliposhindwa na kutuingiza kwenye matatizo. Wanachaguliwa kuleta mabadiliko lakini wanashindwa, wakati sisi raia tunawashinikiza. Ni wakati wa kizazi kipya kuleta mabadiliko.

Chishala aliandika kile alichofikiri ni suluhisho la kwenda mbele [9] kwa taifa la Zambia:

Ninaamini kwamba kumekuwepo mabadiliko ya mawazo na mtazamo. Wazambia lazima kwanza waelewe kwamba ni lazima kuona umuhimu wa kura zao na wasidanganywe na maneno ya ulaghai wa wanasiasa. Lazima wajenge hali ya kutokuwaamini kirahisi wanasiasa na wawaulize maswali mazito wanapogombea nafasi za uongozi….vyama vya kiraia, makanisa, vyama vya kisiasa na sisi sote lazima tushinikize kupunguzwa kwa madaraka ya watalawa, ambalo kwa hakika ndilo tatizo kubwa linalotukabili.

Katika barua ya pamoja ya kichungaji kwenye mkesha wa siku ya Uhuru, makanisa makuu matatu ya Zambia—Mkutano Mkuu wa Maaskofu Zambia, Baraza la Wakristo Zambia, na Umoja wa Kiinjili wa Zambia—yalisisitiza [10] juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za kupunguza umasikini kama kipaumbele cha taifa:

Changamoto iliyopo ni Zambia kutekeleza sera bora za usawa ili masikini waliowengi na wale walio kwenye mazingira hatarishi katika jamii yetu wasiachwe nyuma na kubaki kuwa waangaliaji tu wa shughuli za uchumi. Kwa maneno mengine, ukuaji wa uchumi utakuwa na maana kama utaweza kupunguza umasikini wa watu wa Zambia na kuruhusu ushiriki wa raia walio wengi. Bahati mbaya, kile tunaona tunafanikiwa ni kukuza pengo kati ya matajiri na masikini na kutengwa kwa maeneo ya vijijini kwa maana ya maendeleo ya miundombinu na shughuli za uchumi.