Kwa mtazamo wa tetesi zilizoenea sana kuhusu afya ya rais wa Zambia, Michael Sata, Gershom Ndhlovu ana hoja kwamba katiba inalipa Baraza la Mawaziri mamlaka ya kuchunguza afya yake:
Mara ya mwisho rais wa Zambia Michael Sata kuonekana hadharani ilikuwa takribani Juni 20 ambapo alikuwa mwenyeji wa ujumbe wa serikali ya China ukiongozwa na Makamu wa Rais Li Yuanchao katika ikulu ya nchi hiyo. Wakati huo, mwenekano wa Sata ulikuwa ule wa mtu aliyedhoofishwa na ugonjwa, hali inayothibitisha madai ya kuonekana mkondefu mno alipojitokeza kwenye Mahakama Kuu majuma kadhaa yaliyopita.
Picha za Sata anayedaiwa kuwa mgonjwa ziliposambaa mtandaoni, tovuti moja ya habari mtandaoni, Zambian Watchdog, iliripoti kwamba Rais amepelekwa Israel kwa ajili ya matibabu.
Ni wazi, habari hizo za siri hazikufunua vyema yanayoendelea kuhusu afya ya rais huku maafisa waandamizi wa serikli kuanzia makamu wa Rais na mawaziri wakitoa matamko ya aina aina kuanzia madai kwamba rais yuko kwenye likizo yake ya malipo hadi madai ya kwamba alikuwa anatafuta fursa za kiuwekezaji na kukutana na Rais wa nchi hiyo Shimon Perez.
Aliporudi Lusaka, ikulu ilijaribu kumwonyesha akiendelea na majukumu yake ya kazi kama kawaida na hata kuchapisha picha zake akiongoza kikao cha baraza la Mawaziri. Watu hawakushawishika hata hivyo, na kuona kuwa hiyo ilikuwa ni hatua ya kuwapumbaza, wengine wakisema picha hizo zilikuwa zimetengenezwa.
Hata hivyo, jaribio la hatari zaidi lililofanywa na idara ya mahusiano ya umma ya rais ni picha ya rais Sata akimwapisha mkuu wa masuala ya kisheria wa serikali Musa Mwenye ambaye alithibitishwa na bunge kwa nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali lakini hajaapishwa majuma kadhaa. Kumekuwepo wasiwasi kuwa Mwenye hataweza kutekeleza majukumu yake asipokula kiapo.
Picha iliyokuwa imechapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Ikulu ya Rais, ikisemekana kuwa na lengo la kuonesha kwamba Mwenye alikuwa ameapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilikuwa na sura ya mtu aliyefariki na mwingine aliyekuwa ameteuliwa kuwa mwanadiplomasia miaka miwili iliyopita.
2 maoni