Wanablogu na waandishi tisa, wanne wakiwa wanachama wa Global Voices, wamefunguliwa mashitaka ya ugaidi na shughuli zinazohusiana na ugaidi mbele ya Mahakama Kuu ya Lideta nchini Ethiopia hapo jana. Wakiwa wamekamatwa na kuwekwa ndani jijini Addis Ababa tarehe 25 na 26 Aprili, wamekuwa mahabusu kwa tuhuma zisizo rasmi za “kufanya kazi na mashirika ya kigeni yanayodai kuendesha harakati za haki za binadamu na …kupokea fedha kwa ajili ya kuchochea ghasia kwa kutumia mitandao ya kijamii.”
Wanasheria na ndugu wa washitakiwa hao hawakupewa taarifa ya kusomewa mashitaka yao, na hivyo hakupata msaada wa kusheria wakati mashitaka yao yanasomwa..
Blogu ya Kufuatilia Shauri la Zone9, inayoendeshwa na watu walio karibu na washitakiwa hao, iliripoti kwamba mashitaka yao ni pamoja na kufanya kazi na mashirika yaliyopewa jina la ‘magaidi’ na serikali ya Ethiopia; kushiriki kwenye mafunzo ya kuandika barua pepe kwa lugha ya siril na “kuwa na mipango ya siri.”
Mwanasheria wa wanablogu hao aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mashitaka hayo “hayana maaana yoyote.” Watu wanaowaunga mkono duniani kote walionyesha hasira yao dhidi ya mashitaka hayo kwenye mtandao wa Twita, kwa kutumia alama habari ya #FreeZone9Bloggers. Yoseph Mulugeta, mwakilishi wa zamani wa shirika la Kutetea Haki za Binadamu [Human Rights Watch] nchini Ethiopia ana anayefuatilia kwa karibu kesi hiyo, alitwiti:
19page fabricated charges but no mention of Zone9 by name.Not even once.The brand surely terrifies enemies of free speech #FreeZone9Bloggers
— Yoseph Mulugeta (@YosephMulugeta) July 18, 2014
Mashitaka hayo ya kutunga yaliyoorodheshwa kwenye kurasa 19 hayajataja jina la Zone9 kwa jina. Hata mara moja. Jina hilo kwa hakika linawaogofya sana maadui wa uhuru wa habari
Ikiwa imetungwa mwaka 2009, sheria tata ya kupinga ugaidi nchini Ethiopia kwa bahati mbaya haifahamiki sana kwa waandishi wa habari za kisiasa nchini humo. Waandishi Eskinder Nega na Reeyot Alemu walikabiliwa na mashitaka yanayofanana na hayo na wamekuwa wakishikiliwa kwenye mahabusu ya Kalaity jijini Addis Ababa tangu mwaka 2011. Waendesha mashitaka wanasemekana kuandaa mashitaka hayo kufuatia tuhuma kwamba wanablogu hayo wamekuwa wakipokea mafunzo na misaada ya kifedha kutoka kwenye vikundi viwili vya kisiasa vyenye asili ya vilivyoko Ulaya na Marekani. Blogu ya kufuatilia shauri hilo inabainisha kwamba vikundi hivyo vinafanana kiitikadi..
Kwa mujibu wa taarifa mpya za habari, wanablogu na waandishi hao wanatuhumiwa kujiunga kinyume na sheria kama muungano wa wanablogu wa Zone9, shitaka la ajabu, kwa kuzingatia mwonekano wa wazi wa blogu ya Zone9 na shughuli zinazoendeshwa na kikundi hicho.
Kesi ya kundi hilo itasikilizwa tena Agosti 8. Tembelea Blogu ya Kufuatilia Mwenendo wa Mashitaka hayog kwa taarifa zinazojitokeza kuhusu kesi hiyo na kuona namna unavyoweza kuwaunga mkono wanablogu hao wa Zone9.