Mwanablogu wa Kibahraini Takrooz Akamatwa

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain imetangaza kumkamata mtumiaji mwingine tena wa mtandao, anayedaiwa kutakiwa kujibu mashitaka ya “kuchochea chuki dhidi ya utawala.”

Mwanablogu huyo mwenye mtindo wa kutumia utani katika kuwasilisha ujumbe wake, mwenye jina la utani Takrooz, alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bahrain, wakati akirtudi kutoka Thailand, ilisema taarifa ya Wizara hiyo iliyotolewa Juni 18, 2014, bila kuanika jina lake halisi.

Siku moja kabla, Wabahrain wengi walikuwa na hasira kwenye mtandao wa twita, wakisema kuwa kukamatwa kwake kumefanyika bila sababu na hapakuwa na kingine isipokuwa kuonyesha rangi halisi za serikali dhidi ya sauti kuu za upinzani katika mtandao wa intaneti. Watumiaji kadhaa wa mtandao wameshakamatwa na utawala huo tangu maandamano ya kupinga serikali yaanze nchini Bahrain mnamo Februari 14, 2011. Miongoni mwao ni Mahmood Al-Yousif, Mohamed Almaskati na mwandishi wa Global Voices Mohamed Hassan.

Bahrain inaonekana kuwa adui wa Mtandao wa Intaneti kwa mujibu wa Taarifa ya 2014 ya shirika la Reporters without Borders [waandishi wasio na mipaka] na imeshikilia nafasi ya pili kwa idadi ya waandishi wa habari waliokamatwa nchini humo kwa mwaka 2012 kwa mujibu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari.

Karibu ya wafuatialiaji wa mtandao wa twita 18,000 na twiti zenye jina la Takrooz zipatazo 100,000  zimekuwa sauti hai zinazoilaani serikali kwa kupambana na wanaharakati. Asasi ya Bahrain Watch, inayojihusisha na utafiti na uwazi, ilisema kuwa anuani ya twita ya Takrooz inasemekana  kuwa shabaha ya kufuatiliwa na serikali ya Bahraini. Kwenye twiti zake, kwa lugha ya Kiarabu, zinajikita kwenye uvunjifu wa sheria unaofanywa na watu, kupambana na vitendo vya ufisadi na masuala ya kila siku ya raia wa kawaida wa Bahraini.

Siku iliyofuata mtumiaji wa twita aitwaye @M_Alshaikh alichapisha picha ya habari za Gazeti moja la kila siku la Kiarabu kuhusu kukamatwa kwa Takrooz:

Gazeti la serikali limechapisha makala kuhusu kukamatwa kwa Takrooz kwenye ukarasa wake wa kwanza #Bahrain @Takrooz

Mwanasheria Hanan Alaradi ‏@hananalaradi alitwiti akihoji kinachoendelea baada ya kukamatwa na Takrooz:

Je, mtumiaji wa anuani hii @Takrooz ataachiwa kwa dhamana lama watumiaji wengine wa twita wanaoishabikia serikali @mnarfezhom

Hapo awali, Bahrain ilimkamata mtumiaji wa mtandao wa twita anayeishabikia serikali, Mnarfezhom, ambaye aliachiwa kwa dhamanaon, akisubiri mashitaka. Mnarfezhom anatuhumiwa kutumia majina manne tofauti kuwatukana na kuwadhalilisha watu, akiwavunia heshima na hadhi yao na kudhalilisha familia za Wabahraini kwa kutumia maneno ya kuudhi kupitia mitandao ya kijamii ya Twita na Instagram kwa kutumia majina manne tofauti Al Raqeeb, Ahfad Al Waleed, Ahfad Omar na Mnarfezhom.

Watumiaji wengi wa mtandao wa twita waliokuwa na hasira walihamasihwa kutwiti baada ya kukamatwa kwa Takrooz wakisema kuwa vitendo vya ukamataji havina sababu ya msingi. @Lair_Vulnerable alibainisha:

#Bahrain unapokamata…muasi, mtumiaji wa twita, mpiga picha nk…unamtengenezea alama ya ushujaa nyie wajinga na atakuwa imara zaidi. Mimi ni Takrooz anayefuata

Vyanzo rasmi vinasema Takrooz amekiri kutumia anuani hiyo na kwamba atafunguliwa mashitaka kwa kuchochea chuki dhidi ya utawala.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.