- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Mvua ya Moto Inanyesha Gaza: Israeli Yaanza Shambulio la Ardhini

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Israel, Palestina, Habari za Hivi Punde, Uandishi wa Habari za Kiraia, Vita na Migogoro

Wa-Palestina wanasema mvua ya moto inanyesha Gaza, baada ya Israeli kuanza operesheni ya ardhini [1] ndani ya eneo inalolizunguka, Gaza. Gaza, inayoelezwa kama gereza la wazi, ndiko wanakoishi wa-Palestina milioni 2, ambao hawana pa kukimbilia. Israeli inapakana na Gaza upande mmoj, na Misri inaifungia kwenye upande mwingine.

Kwenye mtandao wa Twita, Jehan Alfarra, mwenye wafuasi 8,000 anasema:

Gaza usiku huu inakabiliana na uvaizi wa ardhini unaofanywa na Israeli!

Mtumiaji mwingine aitwaye Gaza Writes Back, mwenye wafuasi 36,400 kwenye mtandao wa Twita, anasema kuanza kwa uvamizi wa ardhini na milipuko mizito ya mabomu imeifanya “Gaza yote kuwa mithili ya mpira wa moto”:

Israeli imeanza uvamizi wa ardhini na kuugeuza ukanda wote wa Gaza kuwa mithili ya mpira wa moto

Na iFalasteen, vile vile akitokea Gaza, alitwiti kwa wafuasi wake 26,800:

Mvua ya mabomu inanyesha kwenye ukanda wa Gaza sasa hivi kutoka baharini, ardhini na hewani…Israeli inapiga mabomu pande zote

Pia mtumiaji mwingine akiwa Gaza, Palestine, anatuma picha hii ya milipuko ya mabomu ukanda wa Gaza usiku huu kwa wafuasi wake 10,000 kwenye mtandao wa Twita:

Ni shambulio zito linaendelea sasa!!

Kwenye picha nyingine, anasema:

Hata mwezi umekuwa mwekundu hapa Gaza usiku wa leo

Mpiga picha Jehad Saftawi anatuma picha kutoka kwenye mpaka wa Gaza, ikionyesha kuanza kwa operesheni hiyo:

Shambulio la ardhini linalofanywa na Israeli limeanza kwenye ukanda wa Gaza, hapa kwenye mpaka wa Gaza

Wakati Lara Abu Ramadan, mwandishi wa habari wa ki-Palestina, mfasiri na mpiga picha wa kujitegemea anayeishi Gaza, anaeleza:

Hali inatisha. Naweza kuona moto mkubwa kutoka kwenye matanki ya Israeli magharibi mwa ukanda wa Gaza

Na mwanablogu wa ki-Palestina Haitham Sabbah, anatoa kiungo hiki cha habari a moja kwa moja kutoka Gaza:

Habari za moja kwa moja kuhusu shambulio linaloendelea Gaza #GazaUnderAttack [6] http://t.co/jg2PZQbXXK [18] — Haitham Sabbah (@sabbah)

Wakati huo huo, mwandishi wa habari Richard Hall, anayeishi Paris, anawakumbusha wafuasi wake 6,000:

Mara ya mwisho Israeli kuivamia Gaza, wa-Palestina 1,387 waliuawa. 773 walikuwa wananchi wasio wanajeshi, wakiwemo watoto 320 na wanawake 109 (Chanzo: B'Tselem)

Leo ni siku ya 11 tangu kuanza kwa “Operesheni ya Kujilinda”, ambayo imepoteza maisha ya wa-Palestina 230, wakiwemo wanawake na watoto, na zaidi ya watu 1,500 wakijeruhiwa.

Kutoka Gaza, Hamas, ambayo imeutawala ukanda huo tangu mwaka 2007, ililipua makombora [21] kwenda Israeli. Roketi nyingi zinazoingia Israeli hazijasababisha madhara makubwa, kwa sababu, kwa kiasi fulani, ya mfumo wa anga wa ulinzi unaofadhiliwa na Marekani, ambao umezuia makombora yapatayo 70 mpaka sasa, [22] kwa mujibu wa gazeti la the Guardian.

Kwa operesheni hii ya kimakundi, madhara yanaweza kuongezeka zaidi.