Kwa hakika, hakuna yeyote ajuaye kiasi cha gesi iliyopo nchini Tanzania, hata hivyo inakisiwa kuwepo kwa takribani futi za ujazo trilioni 51 za gesi. Mategemeo katika uvunaji wa gesi nchini Tanzania yanaongezeka kwa kasi kubwa.
Katika maeneo mbalimbali ya jiji la Kibiashara la Tanzania, Dar es Salaam, kumekuwa na ongezeko la haraka la magari pamoja na majengo mapya. Mji wa Dar es Salaam umepewa hadhi na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kama jiji linalokuwa kwa kasi zaidi Afrika Mashariki ni jambo lisilohitaji ushahidi hata kidogo. Taarifa ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, “Ufuatiliaji wa Maendeleo ya Africa”, imeonesha makisio ya ongezeko la watu katika jiji hilo kutoka watu milioni 4 hadi milioni 6.2 katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa siku za usoni unadhaniwa kuongezeka kutokana na kipato kutokana na rasilimali za asili kama vile gesi katika mkoa wa Mtwara. Kwa mfano, Mategemeo ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ni kuwa uchimbaji huu wa gesi utaongeza kiasi kikubwa cha upatikanaji wa ajira.
Hata hivyo, maandamano ya Januari na Mei 2013 katika mji wa kibandari wa Mtwara yalitoa ishara ya kukosekana kwa imani kuwa matarajio ya Benki ya Maendeleo ya Afrika kutokuwezekana katika maeneo ya vijijini kama yale ya mkoa wa Mtwara. Chanzo cha maandamano hayo kilikuwa ni maamuzi yaliyofikiwa na serikali ya kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar Es Salaam badala ya kujenga kiwanda cha kuchakata gesi mkoani Mtwara. Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mafuta mkoani Mtwara ungesaidia katika kukuza maendeleo ya kiviwanda mkoani humo.
Tukio la mwanzoni mwa mwezi Julai 2014 lililohusu makubaliano ya ushirikiano katika uzalishaji (PSA) kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC) na kampuni ya Norway ya kimataifa ya Statoil, sambamba na Exxon Mobil, ilionesha hali ya mashaka kuhusiana na suala la mapato kwenye uvunaji wa gesi nchini Tanzania na suala la nani kunufaika na mkataba huo. Pamoja na kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja na vurugu zilizotokea Mtwara, uhusiano uliopo kati ya TPDC na Statoil wapelekea wananchi wengi wa Tanzania kuongeza umakini wao kwenye masuala ya mafuta na gesi, na pia kuongezeka miongoni mwao kwa kutoridhishwa na namna serikali inavyosimamia mikataba ya rasilimali za asili na namna inavyowashirikisha wananchi.
Sababu za hali hii ni kuvuja kwa kiambata cha mkataba rasmi uliofikiwa kati ya Statoil na serikali ya Tanzania kuhusu uchimbaji wa mafuta mkoani Mtwara, ulivuja, na kisha kugonga vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya Tanzania mapema mwezi Julai, 2014. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa kwenye taarifa hiyo iliyovuja, seriakali inaonekana kupoteza kaisi cha dola kimarekani bilioni 1 kwa mwaka.
Kwenye mitandao ya kijamii, watanzania wameshangazwa kwa namna ambavyo makampuni hay mawili yafanyavyo kazi katika mataifa mbalimbali yalivyoweza kuingia makataba mnono kwa kiasi hicho. Katuni iliyoandaliwa na Masoud Kipanya na kuchapishwa kwenye gazeti la Tanzania litolewalo kila siku la Mwananchi, ikimuonesha mzungu akiwa amebeba mgongoni mwake tangi la “GESI” akiendelea kuchimba gesi na wakati huo akimpa mtanzania vijisenti. Katuni nyingine ya Kipanya ikimuonesha panya akisema: “Natamani kama gesi yetu isingechimbwa hadi tutakapopevuka.”
Mradi wa Statoil wa uvunaji wa gesi nchini Tanzania ni moja ya miradi mikubwa kabisa kuwahi kutokea Kusini mwa Jangwa la Sahara. Akiandika kuhusiana na masuala ya Africa, mchambuzi na mwanablogu, Ben Taylor alitanabaisha kuwa, mapato sahihi yatokanayo na gesi asilia yanaweza kuifanya Tanzania kuacha kutegemea misaada ya kimaendeleo kwa kiasi kikubwa.
“Ishara nyingine kuhusiana na mgawanyo huu,” aliandika Taylor, “ni kuwa, kwa kuwa serikali ya Norway ndiye mmiliki mkubwa wa Statoil, mapato ya ziada inayopata serikali ya Norway katika mradi huu yanaweza kuwa ni mara mbili zaidi ya misaada yote iliyowahi kutolewa na serikali ya Norway kwa Tanzania tangu Tanzania kupata uhuru.”
Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge na pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, alifafanua baadhi ya mambo ya msingi yaliyomo kwenye waraka uliovuja katika blogu yake, na kuchambua kwa kina kuhusiana na hoja ya kuwa hati ya makubaliano kutokuwekwa bayana. Kwenye makala ya Julai 6 katika gazeti la Daily News TPDC ilimjibu Kabwe, kwa kusema kuwa, hoja ya kwamba nchi imejiweka katika hatari ya kupoteza kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1 kwa mwaka ni hoja isiyo na msingi wowote. Kabwe na watu wengine walijibu hoja za TPDC katika Twita. Kabwe aliitaka TPDC kutolea ufafanuzi wa makubaliano yaliyofikiwa.
Kwa mujibu wa makala ya Julai 19 katika gazeti la The Citizen, TPDC ilitoa msimamo wake katika mkutano na waandishi wa habari mnamo Julai 16: “Mkurugenzi aliyeko madarakani wa TPDC, Yona Killagane alipinga vikali kabisa kuwa nchi itapoteza dola bilioni 1 za kimarekani kila mwaka iwapo mkataba huu utatumika kama makubaliano yalivyofikiwa. Kinyume chake, alisisitiza kuwa nchi ingaliweza kunufaika zaidi kifedha na hii ineipa nchi nafsi kubwa ya kunufaika katika mkataba huu.”
Watanzania kimsingi hawaridhishwi na suala la uwazi wa mikataba inayohusu rasilimali zao, tukio la kuvuja kwa hati ya makubaliano limechochea zaidi watanzania kutokuiamini serikali yao. Vile vile, haikusaidia, hata pale Patrick Rutabanzibwa, mwenyekiti wa PanAfrican Energy, kampuni inayoendesha mradi wa gesi ya Songo Songo pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme wa Ubungo uliopo jijini Dar es Salaam (na pia ndiye aliyekuwa katibu wa Wizara ya Nishati na Madini), kulimaliza suala hili kimya kimya.
“Tunashindwa kuingia mikataba inayohusu rasilimali kama ilivyokuwa kwenye uchimbaji madini na sasa katika mafuta na gesi kwa kuwa uwezo wetu bado ni mdogo,” alisema Rutabanzibwa. “Lakini kama watanzania watawezeshwa, mikataba itakuwa katika hali ya usawa. . . . Tunapaswa kusahau yaliyopita na tuanze kuingia mikataba ya uwekezaji ya gesi asilia kwa uwazi na kwa kufuata taratibu; Ni dhahiri kuwa, itafikia wakati ambao mikataba yote ya uwekezaji itakuwa bayana.”
Kwa washikadau walio na mipango ya kufanya biashara na uwekezaji nchini Tanzania, ukosoaji unaifanya sekta kama ya gesi iliyo na changamoto nyingi kuwa ngumu zaidi, na wengine wanaona kuwa, matokeo yake ni kuwa, maeneo yaliyotelekezwa hayatafaidika ipasavyo. Wengine wanaweza kusema kuwa, mbali na mgawanyo wa mapato baina ya Tanzania na makampuni yaliyowekeza, bado kutakuwa na faida ya upatikanaji wa ajira pamoja na ukuaji kiuchumi kwa mkoa wa Mtwara.
Mchambuzi Ben Taylor hakuwa na imani na maelezo hayo. “Moja ya hatari kubwa ya kisiasa katika uvunaji wa mafuta na gesi,” aliandika Taylor, “ni kuwa,jambo hili linaweza kuchukuliwa na wanasiasa na viongozi waandamizi kuwa ni fedha za “bure” ambazo huwa hazipatikani kirahisi kwa walipa kodi wanaofuatilia kwa makini kabla ya kulipa kodi zao pamoja na matakwa ya watoa misaada kabla ya kutoa misaada.
“Bila ya mtu– vyombo vya habari, wanasiasa, watetezi wa haki za raia – wasipoingilia kati na kutatua tatizo, viongozi wa serikali wataendelea kuwa huru kufanya maamuzi wanayoona wao yanafaaa, na yasiyo na tija yoyote kwa jamii. Makubaliano ya Ushirika katika uzalishaji ya Statoil yanaweza kuigharimu Tanzania mabilioni ya dola, lakini yaonekana bado hakuna yeyote anayejaribu kuwawajibisha wale wanaohusika.”