Je, Tunaweza Kuwasaidia Wazee kwa Kuwakumbatia? Kampeni hii ya India Yasema ‘Ndio!’

A HUG Campaign Poster. Image courtesy HelpAge India

Bango la Kampeni ya KUKUMBATIA. Picha kwa hisani ya HelpAge India

Kwa miongo kadhaa, utamaduni wa familia kuishi pamoja nchini India ulimaanisha kuwa vizazi kadhaa kuanzia babu mpaka wajukuu viliishi kwenye nyumba moja. Lakini shauri ya mageuzi ya haraka ya kimaendeleo nchini India, miingiliano ya kijamii nchini humo inabadilika. Wahindi wengi zaidi sasa wanaishi kwenye familia ndogo, na vijana wanahama kutafuta fursa bora zaidi za kimaisha.

Hali hii imesababisha kuongezeka kwa wazee wengi wanaolazimika kuishi maisha ya upweke. Wengi wao wanakabiliana madhila ya kutengwa, kupuuzwa na upweke. 

Kampeni moja inayosisimua inajaribu kusaidia kubadili hali ya mambo. Kampeni inayoratibiwa na HelpAge India  KUKUMBATIA- Kunasaidia kuunganisha vizazi inawahamasisha vijana wa Kihindi kufanya urafiki na wazee na kutuma picha zao zinazoonyesha wakiwakumbatia wazee kwa lengo la kujenga “muunganiko wa vizazi na vizazi na kuongeza uelewa wa vijana kwa hali wanazokabiliana nazo wazee”. 

HelpAge India, shirika lisilo la kiserikali ambalo hufanya kazi ya kuwasaidia na kuwajali wazee, linaeleza   katika ukurasa wao utetezi namna vijana wanavyoweza kuleta tofauti:

Wakati wowote unapomwona mzee amekaa mwenyewe, mtazame kwa mara ya pili!! Anaweza kuwa anatoka kwenye familia yako au jirani yako au mtu uliyewahi kumwona mara nyingi akiwa peke yake. Mzee huyo analo hitaji moja tu ambalo kwa hakika unaweza kulitimiza. Kwa neno moja, tabasamu moja, KUMBATIO moja! Wape wazee wa namna hii muda wako mdogo. Ishara hizi ndizo wazee wanazozitaka lakini kwa bahati mbaya hawazipati. Kampeni ya KUKUMBATIA inawahamasisha vijana kuwapigia simu, kusikiliza uzoefu wa wazee na kuwauliza siku yao imeendaje na shiriki masimulizi yako na rafiki yako mzee.

Kampeni hii imeweka video inayoweza kukutoa machozi kuonyesha kile ambacho kinaweza kusababishwa na kukumbatia mzee:

Wahindi wanaishi maisha marefu, na idadi ya wazee vikongwe inaongezeka…Kwa mujibu wa taarifa [pdf] ya mwaka 2011 iliyoandaliwa na Serikali ya India, “idadi ya wazee wa Kihindi wenye mvi” (inayoweza kutafsiriwa kama umri wa miaka 60 na kuendelea) inawezekana kuendelea kuongezeka miongoni mwa raia wa nchi hiyo kutoka asilimia 7.4 mwaka 2001 kufikia asilimia 10 mwaka 2026. Kwa maana ya tarakimu, ni ongezeko kubwa —kutoka wastani wa milioni 77 mwaka 2001 mpaka milioni 140 kufikia mwaka 2026.

Manjira Khurana (@KhuranaManjira), Mkuu wa kitaifa, utetezi na Mawasiliano katika shirika la HelpAge India, anaamini kwamba jitihada kama hizi zinaweza kuwasaidia vijana kuelewa mahitaji ya wazee. Katika mahojiano ya barua pepe na Global Voices, alizungumzia matarajio yake kwa kampeni ya KUKUMBATIA:

Nyakati chache za kupata kahawa mahali, kutoka mara moja kunyoosha miguu mtaani na basi tu kupiga simu, hubadilisha maisha. Mzee huwa na furaha na kijana hugundua kuwa Mzee anaweza kuwa mtu wa muhimu kuzungumza nae pia! Hiyo inaweza labda kumfanya kijana huyu aelewe na kuwa mkarimu kwa wazee katika maisha yake ya baadae.

Kampeni ya KUKUMBATIA inawaomba vijana vilevile kututumia uzoefu wao katika kampeni hii na picha hali kadhalika. Shreya Misra, anayefanya kazi katika shirika la Teach for India, anatuma picha kwenye ukurasa wa Facebook wa HelpAge India, inayomwonyesha akimkumbatia babu yake.

"I am sharing a hug with my grandfather. Its such a wonderful feeling to see him smile." Image from HelpAge India's Facebook page

“Ninamkumbatia bau yangu. Ni hisia nzuri sana kumwona akitabasamu.” Shreya Misra, mfanyakazi wa Teach for India. Picha kutoka ukurasa wa Facebook wa HelpAge India

Kuna msemo kuwa hakuna mtu aishiye kisiwani. Kwa hakika, wazee hawastahili kutelekezwa kwenye kisiwa cha upweke na ukiwa katika miaka yao ya uzeeni. Kampeni ya KUKUMBATIA imepuliza kipenga kwa vijana wa Kihindi –katika maisha yako yenye harakati nyingi, katika kuwahi kwako kwenda mahali au kwenda mbele, usiwasahau wazee. Simama kwa muda na wafanye wawe sehemu ya maisha yako –wape tabasamu, wasimulie, wakumbatie.

Leo, asilimia 50  ya idadi ya watu nchini India wana umri wa chini ya miaka 25. Je, kundi hili la vijana linasikia kampeni hii? Na lililo muhimu zaidi, je litachukua hatua sasa ili wazee wajisikie kujaliwa, kupendwa na hata kujisikia kuhitajika katika kipindi ambacho kwao ni kama jua linazama? Mimi, mmoja wapo, nadhani kwa dhati itakuwa hivyo.

Usiwe na wasiwasi na idadi ya miaka. Msaidie mtu mmoja kwa wakati mmoja, na siku zote anzia na mtu aliye karibu zaidi na wewe.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.