Watoto Wachanga 44,000 wa Madagaska Hupoteza Maisha kila Mwaka kwa Kukosa Matunzo. Tunawezaje Kukabiliana na Hali Hii?

Enfants Malgaches par Yves Picq - CC-BY-SA-3.0

Watoto wa Madagaska na Yves Picq – CC-BY-SA-3.0

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Shirika la Watoto Duniani, UNICEF watoto 44,000 walio chini ya umri wa miaka mitano hupoteza maisha kila mwaka nchini Madagaska. Idadi hii ni sawa na idadi ya watoto wote wa miaka mitano na chini ya miaka mitano katika eneo lote la jimbo la Alpes-de-Haute la ukanda wa Ufaransa. Pia, ni idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, zaidi ya mara 15.

Matukio ya watoto kupoteza maisha  kwa kiasi kikubwa yanaathiri familia zisizojiweza. Katika nchi ya Madagaska, suala la afya ya jamii imeonekana kuathiri zaidi makundi mawili: watoto walio na umri chini ya maika mitano na wanawake wajawazito.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, nusu ya watoto wote hudumaa, “uwiano ambao ni mkubwa kabisa miongoni mwa mataifa yote ya Afrika.” Kiwango cha vifo vya watoto unakadiriwa kufikia watoto 498 kwa kila wanawake 100,000 wanaojifungulia katika vituo vya afya. Vyanzo vya vifo hivi ni vingi, ikiwa ni pamoja na kukosa wataalamu wa kutosha wa kuwasaidia wanawake wakati wa kujifungua, matunzo hafifu katika kipindi cha kabla ya kujifungua na ukosefu wa huduma za dharura. 

Wakati hali ya utoaji wa huduma za afya inazidi kuzorota, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizokwisha kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo hili.

Huko Toliara, kusini mwa Madagaska, mradi wa chakula cha mchana mashuleni unasaidia katika kukabiliana na matatizo yaliyokithiri ya utapia mlo. Shirika la Les Enfants du Soleil (Watoto wa Jua) linawapa hifadhi na kuwasomesha watoto wa mitaani pamoja na wale wanaotokea katika familia zisizojiweza. Pia, watoto hupata chakula cha mchana katika mkahawa wa shule. Tazama picha za watoto wanaofaidika na mradi huu katika video ya You tube iliyo katika lugha ya kifaransa:  

Miradi mingine inalenga kushughulika na changamoto zenye kuhitaji ufuatiliaji wa karibu zaidi kama vile ugonjwa wa upungufu wa damu au malaria. Shirika la LCDMF (vifupisho vikiwa na maana ya Tokomeza Anemia Nchini Madagaska) linafanya kazi ya kutoa elimu kwa watu wa Madagaska kuhusiana na ugonjwa huu wa kurithi unaoathiri asilimia 2 ya watu wa Madagaska.  Video ifuatayo inawaonesha viongozi wa LCDMF wakitoa ufafanuzi wa kazi za asasi hii binafsi zilizokwishafanyika pamoja na malengo yake ya miaka mitatu ijayo. Kurahisisha upatikanaji wa viuavijasumu (antibiotics) vya ugonjwa wa anemia na kuwashauri viongozi wa Madagaska kutoa kipaumbele kwa ugonjwa wa anemia katika vipaumbele vya taifa vya huduma ya afya yajamii, ni miongoni mwa malengo mawili ya asasi hii isiyo ya kiserikali kwa miaka ijayo: 

Katika barua ya wazi aliyoandikiwa Waziri Mkuu, Malgache Kolo Roger, asasi ya LCDMF ilisisitiza umuhimu wa kukabiliana na tatizo hili na hususani katika maeneo yaliyosahaulika na yasiyo na mifumo ya kisasa ya utoaji wa huduma ya afya:

Ce problème crucial de santé publique qui affecte de manière dramatique les plus nécessiteux dans une région avec près de 20% de prévalence où un enfant sur cinq souffrant d’un syndrome drépanocytaire majeur est susceptible de ne pas survivre au-delà de l’âge de 5 ans, ne peut plus souffrir de demi-mesures. Il illustre à lui seul, parce qu’il s’agit d’une maladie transversale intéressant toute les spécialités médicales, l’exigence d’une prise en compte urgente de votre part de ces logiques de santé de proximité.

Hili ni tatizo kubwa sana katika afya ya jamii lililo na madhara makubwa kwa watu wanaohitaji msaaada wa haraka katika eneo lililo na kiwango cha ongezeko la ugonjwa huu kwa asilimia 20 na ambapo kwa kila mtoto mmoja kati ya watoto watano walio na anemia huwa katika hatari ya kupoteza maisha baada ya kufikisha miaka mitano. Tatizo hili haliwezi tena kumalizwa kwa kulipa msisitizo hafifu. Kwa kuwa, ugonjwa wa anemia unamuhusisha kila mmoja na kuwajumuisha wataalamu wote wa afya, ugonjwa huu unaonesha ni kwa jinsi gani unavyopaswa kupewa msisitizo wa haraka kwa kutoa huduma za afya zinazopaswa.

Bado kuna mambo mengi yanayotakiwa kutekelezwa

Sehemu nyingine yenye kuhitaji msisitizo wa haraka na kufanyiwa kazi ni afya ya uzazi, hii inatokana na ongezeko la haraka la idadi ya watu nchini Madagaska. Kwa mfano, kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Takwimu ya Madagaska (INSAT) pamoja na Mfuko wa Takwimu ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA), mmoja kati ya wanawake watano walioolewa wanaopenda kupangilia uzazi au kuzuia mimba hawana elimu ya uzazi wa mpango (asilimia 19), na kiwango cha utoaji mimba kinakadiriwa kufikia mwanamke mmoja kati ya kila wanawake 10 wanaojifungulia katika vituo vya afya. 

Pamoja na juhudi zote hizi, Madagaska inakabiliwa na mapungufu kadhaa yanayokwamisha uboreshaji wa mambo muhimu katika utoaji wa huduma ya afya. Huduma hafifu inachangiwa na utofauti wa vipato katika familia pamoja na namna ya kuzipata huduma za afya. Kutokana na changamoto hizi, takribani mtu mmoja kati ya watu wanne (sawa na asilimia 23) wanaosumbuliwa na maradhi hawakuweza kupata huduma ya matibabu kwa kuwa hawakuwa na fedha za kulipia.

Upatikanaji wa dawa pia ni tatizo kubwa kwa kuwa kuna tatizo la kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa dawa na taarifa za upatikanaji wa dawa pamoja na taratibu za usambazaji zinazokwamisha mgawanyo sahihi. Matokeo yake ni kuwa, watu matajiri hufaidi huduma za afya mara nne zaidi ya watu masikini: kwa mujibu wa Benki ya Dunia, asilimia 40.9 ya matumizi yote ya sekta ya afya yalichangiwa na kundi la watu matajiri, wakati asilimia 10.1 ilichangiwa na kundi la watu masikini. 

Wataalamu wanakubaliana kuwa, kuchukuliwa kwa hatua za haraka ni jambo la msingi. Shirika laUNICEF ladokeza kuwa  chanjo pamoja na usimamizi wa lishe bora kwa watoto wachanga ni mambo ya muhimu ya kuzingatia ili kupunguza vifo ya watoto wachanga. Ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya ya jamii kwa ujumla, mambo yanayopaswa kupewa  kipau mbele ni:

  •     Kuboresha miradi ya lishe kwa kuangalia zaidi makundi yanayoathirika zaidi na namna bora ya upatikanaji wa lishe ya kutosha;
  •     Kuboresha ufanisi wa matumizi ya bajeti ya afya;
  •     Kuboresha usimamizi wa rasilimali watu katika utoaji wa huduma za afya;
  •     Uwepo wa vifaa kwa ajili ya kutolea huduma za dharura za afya;
  •     Kuwarudisha madaktari katika vituo vya afya vya vijijini.

Hali ni tete, pamoja na kuwa haijafikia kiwango cha kukatisha tamaa. Sera zilizopendekezwa zinaweza kutekelezwa vizuri kama zitapewa kipau mbele na serikali. Watoto wa Malagasi wamesubiri kwa miaka 50 ili kupata mustakabali wa afya yao katika vipau mbele muhimu vya Taifa. Ni muda muafaka wa kuikumbusha serikali kuwa hakuna nchi inayoheshimika ingaliweza kuvumilia kuona vizazi vijavyo vikiteketea katika hali kama hii, vifo 44,000 kwa mwaka.  

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.