Solana Larsen Aachia Ngazi kama Mhariri Mtendaji, Sahar Habib Ghazi Apokea Kijiti

Outgoing Managing Editor, Solana Larsen (L) will be succeeded by Sahar Habib Ghazi (R)

Mhariri Mtendaji anayemaliza muda wake, Solana Larsen (kushoto) nafasi yake inachukuliwa na Sahar Habib Ghazi (kulia)

Mwishoni mwa mwezi Mei tulimuaga rasmi Mhariri wetu Mtendaji wa muda mrefu, Solana Larsen, na kumkaribisha rasmi kubadili majukumu yake kuwa, sasa, mchangiaji wetu mpya kabisa wa kujitolea, akiitwa Solana Larsen.

Solana anaachia ngazi kutoka nafasi ya Mhariri Mtendaji, aliyoishikilia kwa miaka saba kuongoza bodi ya uhariri ya Global Voices. Watu wengi wanapong'atuka hutumia “sababu binafsi” kama maelezo rahisi ya kufunika sababu halisi, lakini Solana kwa hakika ameamua kuachia ngazi ili apate nafasi ya kutosha kutunza familia yake, hususani binti yake wa miaka miwili. “Ni jambo jema kwangu binafsi na familia ya Global Voices,” aliandika kwenye waraka ulioelekezwa kwa familia ya Global Voices, “kuachia ngazi sasa na kuruhusu mambo mapya yatokee.”

Ujuzi wa Solana umemsaidia kumudu vyema majukumu ya uhariri wa Global Voices katika kipindi ambacho uandishi wa habari ulishuhudia blogu na mitandao ya kijamii vikigeuka kuwa majukwaa muhimu kuwawezesha wananchi wa kawaida kusema mawazo yao. Tunafurahi kwamba ataendelea si tu kama mchangiaji wa kujitolea, lakini pia atafanya kazi nasi kwenye shughuli maalumu na kutuwakilisha kwenye mikutano.

Solana anaiacha bodi ya uhariri ya Global Voices kwenye mikono mahiri ya Sahar Habib Ghazi, aliyeungana nasi kama Naibu Mhariri mwezi Juni 2012.

Sahar, ambaye ni mwandishi wa habari, mwanablogu na mwanaharakati anayegawa muda wake kati ya Marekani na Pakistani, alisaidia kuanzisha DawnNews TV na ameandikia jarida maarufu la New York Times. Akiwa sehemu ya Shule ya Uandishi wa Habari ya John S. Knight katika chuo kikuu cha Stanford, alianzisha Hosh Media, jukwaa la mtandaoni la uandishi wa habari kwa vijana.

Sahar amekuwa mhimili katika kutengeneza mwongozo wa kimaudhui wa Global Voices, kuratibu shughuli nyingi za uhariri na kujenga timu imara ya uhariri. Lililo kubwa zaidi, ni mjuzi aliyebobea na mwanachama anayejitolea vya kutosha kwa familia ya Global Voices, ambaye tunaamini ataipeleka mbele timu ya uhariri, kwenda inakotakiwa kwenda.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.