Mwanablogu wa Mirsi Nadia El Awady anaandika posti ya blogu yake ambapo anahoji kama wanawake wanaovaa Hijabu wanabaduliwa kwenye nchi za magharibi ama la. Nadia, kama Mmisri alikulia Marekani na ameishi kwa kipindi kirefu Ulaya, anaelezea uzoefu wake kuhusu mwitikio alioupata kwenye nchi za Mashariki na Magharibi linapokuja suala la kuvaa Hijab au hata kuivua.
Anaandika:
Kwa miaka yote hiyo, nimekuwa sivai Hijab, nikivaa hijab, nikivaa hijab ndefu sana (inayoitwa khimar), nikivaa kitambaa cha kufunika uso (kinachoitwa niqab), baadae nikaanza kuvaa hijab fupi na hivi sasa, sivai kabisa. Nimeyafanya yote hayo. Nimeona mwitikio. Namna nilivyovaa kwa miaka yote hiyo imekuwa ikikubaliwa na baadhi ya marafiki wangu wa karibu na kukosolewa na wengine; hii ni kweli. Namna mwanamke anavyovaa ni mada yenye mjadala mkali bila kujali uko wapi duniani humu. Nilipoacha kuvaa kitambaa cha kufunika uso, baba yangu mzazi alikuwa kinyume. Niliachana na Hijab, nilimpoteza angalau rafiki yangu mmoja wa karibu na wengi walinishangaa. Hii ni miitikio ya kawaida na inatarajiwa. Siwezi kuiweka kwenye kundi la unyanyasaji. Marafiki na familia wanajua wanachokitarajia kwa maisha yangu. Wanaamini wanajua kile kilicho bora kwangu.