Msiyalaumu Mataifa ya Magharibi kwa Matatizo ya Afrika

Gershom Ndhlovu anasema kuwa viongozi wa Afrika wanafanya kosa kuzilaumu nchi za Magharibi kwa matatizo ya Afrika:

Kwenye mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya ulifanyika nchini Ubeligiji, rais wa Zambia Michael Chilufya Sata alijibu mapigo kwa kile kile ambacho viongozi wengine wa Afrika walikisema huko nyuma kuhusu Nchi za Magharibi kuchangia vita barani humu kupitia biashara ya sialaha na vifaa vingine vya kivita. Akinukuliwa na Eil D’Afrique, Sata aliuambia mkutano huo kuwa Afrika haikuwa na kiwanda cha silaha zinazochochea migogoro na kwamba Ulaya inahusika moja kwa moja na migogoro inayotokea barani humu kwa sababu silaha zinazotumika kwenye migogoro zimezalishwa kwenye viwanda vilivyoko kwenye nchi za Magharibi. “Askari wengi watoto na masikini wanaohusika na migogoro hii barani Afrika wanabeba silaha zilizozalishwa Ulaya zenye kugarimu maelfu ya dola. Watoto hawa masikini hawawezi kuwa na fedha za kununulia silaha hizi,” alisema Sata.
Katika kipindi cha baada ya uhuru, Afrika imekuwa na mchango wake wa kutosha kwenye mapinduzi na visasi vya kupindua waliopindua pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ni kweli, kuwa mapinduzi mengi yalipangwa kwenye vyumba vya faragha ambapo wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walikutana na maafisa wa kijeshi huku wakigida mvinyo na pombe ghali, wakiwafanya si tu wawe na tamaa ya kudhibiti raslimali za taifa kama watang’oa viongozi wenye misimamo mikali dhidi ya nchi za Magharibi lakini pia kuwafadhili mtaji. Hivi ndivyo madikteta kama Mobutu Sese Seko walivyoweza kupanda na kung’ang’ania madarakani.
Lakini kuzilaumu nchi za Magharibi na viwanda vya silaha barani Ulaya kwa migogoro yote au mingi ya migogoro hiyo ya hivi karibuni ni kutokuwa wakweli na kwa hakika ni sawa na kuficha vichwa mchangani, kama afanyavyo mbuni. Ni aibu kuwa leo bado nchi za Afrika zinawalaumu mabwana zao wakoloni wa zamani kwa uchumi uliozorota ambao kwa hakika kabisa kunasababishwa na ufisadi, udhibiti mbovu wa raslimali na kukosa uwezo.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.