- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Uwakilishi wa Kisiasa: Mapambano ya Raia wenye Asili ya Afrika Waishio Colombia

Mada za Habari: Amerika Kusini, Colombia, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Ubaguzi wa Rangi

Ikiwa na idadi ya watu milioni 5, au asilimia 10.6 ya idadi ya watu wote wa nchi hiyo, Colombia ina idadi kubwa zaidi ya watu wenye asili ya Afrika katika bara la Amerika Kusini, nyuma tu ya Brazili kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2005. Hata hivyo, kuna changamoto kubwa ya kuutafsiri weusi wa mtu, kutokana na mchanganyiko mkubwa wa rangi kwa wa-Columbia wengi. Unyanyapaa wanaofanyiwa watu wenye asili ya Afrika katika sehemu kubwa ya nchini hiyo husababisha machotara wengi kutotaka kujulikana kuwa wana asili ya Afrika, wakati takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika wanafikia asilimia 25 ya watu wote.

Maren Soendergaard kwenye tovuti ya Colombia Reports [1] anaandika kuhusu kutengwa kisiasa kwa raia wenye asili ya Afrika nchini humo, akisema kwamba “kukosekana kwa uwakilishi wa kisiasa katika mfumo wa kisiasa wa Columbia ni moja ya malengo ya mapambano ya kijamii, ksiasa na kiuchumi yanayoendelea miongoni mwa jamii ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika.”