- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Siku 100 Gerezani Bila Mashitaka: Simulizi la Alaa Abd El Fattah

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Misri, Harakati za Mtandaoni, Maandamano, Sheria, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza

Mwanablogu maarufu nchini Misri Alaa Abd El Fattah alimalizia siku yake ya 100 katika gereza bila ya kufunguliwa mashitaka leo. Abd El Fattah alipigwa kikatili na kukamatwa kutoka nyumbani kwake Cairo Novemba 26, 2013 na kutuhumiwa kwa “kuandaa maandamano ya Tunapinga Mashitaka ya kijeshi kwa raia” siku mbili kabla ya kukamatwa kwake.

Kwa mujibu wa Rasha Abdulla, mwandishi wa Kitengo la Utetezi cha GV [1] ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Abd El Fattah:

Amekuwa kizuizini tangu Novemba 28, baada ya kutuhumiwa kuandaa maandamano mbele ya Baraza la Shura (Bunge Kuu nchini Misri) bila kupata ruhusa kisheria. Siku mbili kabla ya maandamano, wabunge walipitisha sheria inayohitaji waandaaji maandamano yoyote kuwasilisha taarifa kuhusu kusudio la kuandamana kwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
[…]

Maandamano hayo yaliandaliwa na kikundi kinachopinga kuendeshwa kwa mashitaka ya kijeshi kwa raia, kampeni iliyoanzishwa na Mona Seif lakini ambayo hata hivyo kaka yake Alaa hakuwa mwanachama. Kikundi hicho kimetoa taarifa kwa vyombo vya habari kudai kuhusika na maandamano hayo. Wanachama wa kikundi hicho pia waliwasilisha ripoti kwa mwendesha mashitaka ya umma kudai uwajibikaji kwa tukio hilo. Maandamano, ambayo yalifanyika Novemba 26, yakitoa wito kwa ajili ya kusitishwa kwa uendeshaji wa mashitaka ya kijeshi kwa raia wa kawaida katika katiba mpya ambayo wananchi wa Misri wataipigia kura baadaye mwezi huu [Januari].

Maandamano yalitawanywa kwa ukatili na polisi takribani nusu saa baada ya kuanza. Polisi waliwaweka kizuizini wanawake 11, wengi wao wanachama wa kundi hilo la kupinga mashitaka ya kijeshi kwa raia, na wanaume 24. Wanawake, ambao wote walipigwa na ambao baadhi yao walibakwa wangali kizuizini, walishikiliwa kwa masaa kadhaa. Baada ya hapo walilazimishwa kusafiri kwa gari la polisi na kutelekezwa jangwani baada ya usiku wa manane. Wanaume waliwekwa kizuizini kwa juma zima na sasa wote wameachiliwa huru (isipokuwa mmoja, Ahmed Abdel Rahman ) akisubiri uchunguzi wa kipolisi. Alaa alitiwa kizuizini baada ya polisi kuvamia nyumba yake siku mbili baadaye na kutuhumiwa kuandaa maandamano. Madai hayo yalitokea licha ya Alaa kusubiri nje ya kituo cha polisi ambapo dada yake alikuwa kizuizini Novemba 26 jioni yote mpaka yeye alipochukuliwa na marafiki baada ya polisi kumrusha yeye na wenzake jangwani na kutelekezwa. Ingawa wote Alaa na Ahmed Abdel Rahman wamekuwa kizuizini kwa zaidi ya mwezi wakisubiri uchunguzi, hakuna tarehe iliyopangwa na mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi.

Hali bado ni sawa leo. Tarehe ya mahakama bado haijawekwa – siku 100 baada ya kukamatwa kwake. Blogu ya Kumbukumbu za Tahrir Diaries iliweka video hii kwenye mtandao wa YouTube kuadhimisha siku 100 ya kukamatwa kwa Abd El Fattah.

Inamwelezea Manal Hassan, anayeelezea kile kilichotokea kwa mumewe Abd El Fattah, na Nazly Hassan mwanachama wa Kikundi cha kupinga Mashitaka ya kijeshi kwa raia, ambaye anaonyesha matatizo aliyokabiliana nayo Ahmed Abdul Rahman, mpita njia ambaye aliyewauliza polisi kwa upole akiwa kwenye maandamano kwa nini walikuwa wakiwapiga na kuwabaka wanawake washiriki.

Picha iliyotumiwa kwenye makala haya inaonyesha maneno yanayosomeka “Uhuru wa Alaa Abd El Fattah” yaliyoandikwa ardhi nje ya jengo la Mashitaka ya Kijeshi mjini Cairo. Picha ilichukuliwa na Nazly Hussein na kuwekwa kwenye mtandao wa Twita..