Mtu aliyetengeneza ukurasa bandia kwa jina la mke wa rais wa zamani wa Zambia, Maureen Mwanawasa alipandishwa kizimbani hivi karibuni kujibu mashitaka ya utapeli.
Mwanawasa, mke wa rais wa tatu wa Zambia, marehemu Levy Patrick Mwanawasa, aliyetawala kwa miaka saba mpaka alipopatwa na mauti mwaka 2008, anaendesha shirika lisilo la kiserikali linaloitwa Mradi wa Jamii wa Maureen Mwanawasa (MMCI), unaosaidia watu masikini katika jamii. Shirika hilo lilikuwa imara sana enzi za utawala wa mme na lilipokea msaada kutoka katika mashirika kadhaa pamoja na watu binafsi. Tangu kifo cha mumewe shirika hilo limekuwa likipunguza shughuli zake na kubakiwa na maeneo mawili tu, Kapiri Mposhi ambapo linaendesha shule kwa ajili watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Taarifa za kina kuhusiana na kesi hiyo hazitolewa, lakini Mwanawasa, ambaye ni mwanasheria yeye mwenyewe, alipanda kizimbani na kutwiti sababu za kwenda mahakamani kujibu maswali ya watumiaji wa mtandao wa twita:
@NizaSich someone has created a face book page in my name and she collects 250$ for false scholarships she has been arrested#Zambia
— Maureen K Mwanawasa (@mwanachilembo) October 3, 2013
kuna mtu ametengeneza ukurasa wa facebook kwa jina langu na anakusanya dola za marekani 250$ kwa ajili ya kutoa udhamini bandia kwa wanafunzi ametiwa kizuizini.
Mtandao wa Zambian Watchdog uliripoti kashfa hiyo mwezi Januari 2012, lakini haiko wazi kama inahusiana na kesi iliyopo mahakamani. Akimnukuu mkosoaji Laston Nyirenda, wavuti hiyo iliripoti:
Nina urafiki [kwenye mtandao wa Facebook] na mtu huyo na walianza kunitumia jumbe wakidai kuwa Bi Mwanawasa na kuanza kuniomba niwaazime dola 2000 na kumtumia mtu aliyetajwa kuwa Florence Lucky aliyesema anaishi Madrid, Uhispania na wakanitaka niwatumie pesa hizo kwa njia ya western union. Wakanipatia namba ya simu ya Zambia ili niwapigie wakisema kwamba ni ya mke wa zamani wa rais na kama ninataka kuhakiki na nilipoipiga namba hiyo, ikapokelewa na mtu aliyekuwa [mji wa] Kitwe na hata haikuwa ya Bi Mwanawasa.
Baada ya Mwanawasa kulitangaza suala hilo kupitia mtandao wa Twita kuwa yuko mahakamani, mtumiaji mmoja alimwuliza mke huyo wa rais huyo wa zamani namna alivyojisikia kutoa ushahidi:
@mwanachilembo how did it feel to be on the other side? probably recieving end of a X examination?
— Eric (@EricKamocha) October 2, 2013
Ulijisikiaje kuwa kizimbani? Huenda ukihojiwa?
Akajibu:
@EricKamocha naturally it felt strange but it was a good experience
— Maureen K Mwanawasa (@mwanachilembo) October 3, 2013
@EricKamocha kwa kawaida mtu unajisikia vibaya lakini ulikuwa ni uzoefu mzuri
Twiti za Mwanawasa hakutoa habari za kina kuhusu kesi hizo kama jina la mtuhumiwa na wapi anakoishi.
Mke huyo wa Rais wa zamani, hata hivyo, si mtu maarufu wa kwanza nchini Zambia aliyewahi kukumbwa na matukio ya kughushiwa kwa akaunti zao mitandaoni. Hivi karibuni, ukurasa wa Facebook kwa jina la Makamu wa Rais wa nchi hiyo Dr. Guy Scott, ulitumiwa kutuma “maombi ya urafiki” kwa watu ambao kwa kawaida kutoa maoni ya kisiasa katika mitandao ya kijamii.
Ukurasa huo bandia wa Facebook uliodaiwa kuwa wa Dr. Scott ulipoonekana, wavuti ya kiraia ya Zambian Eye iliripoti habari hizo, inagwa kulikuwa na maswali mengi kuhusiana na uhalisi wake:
Inashangaza kuona Guy Scott anatuma maombi ya urafiki kwa kila mtu kwenye mtandao wa Facebook. Haihitaji kuwa na akili nyingi kugundua kuwa akaunti hiyo unaendeshwa na majenerali bandia wa PF [mashabiki wa chama tawala cha Patriotic Front wanaojiita jina hilo] kwenye mtandao wa Facebook wanaotaka kuitumia kukusanya takwimu. Amkeni jamani.
Dr Scott baadae alinukuliwa na mtandao wa Zambia Intelligence News, akisema:
Nilifungua akaunti mwaka 2011 kwa malengo ya kampeni na sijawahi kufungua akaunti nyingine tena. Sijawahi kuitumia tangu wakati huo kwa hiyo kila kinachoibukia leo ni bandia. Yote hayo ni utapeli tu. Huo ni utapeli tu.