Rafiki Yangu Anateswa kwa Ku-blogu

HABARI MPYA [Octoba 2, 2013]: Mapema leo, Mohammed Hassan aliachiwa huru kutoka gerezani kwa dhamana. Taarifa za marafiki zake wa karibu zinasema yu salama na tayari ameungana na familia yake nyumbani. Tunawashukuru rafiki na ndugu zetu kwa msaada na kutuunga mkono katika utetezi wa kuachiliwa.

Tangu kushikiliwa kwake mwishoni mwa Julai, imekuwa vigumu kwangu na wanablogu wengine kutangaza suala la Mohammed Hassa (anayejulikana pia kama Safy) mwanablogu wa Bahrain alikamatwa na serikali kwa shughuli zake za mtandaoni. Katika nchi kama Bahrain, imekuwa ni kawaida kwa utawala huo wa kikatili kuwafanyia unayama na wakati mwingine kuwanyamazisha wale wote wanajihusisha na mapambano ya kisiasa kudai uhuru na usawa. Madaktari, waandishi, watetezi wa haki za binadamu, walimu, wanariadha, na waandamanaji wamekuwa walengwa ya uovu huo nchini Bahrain wakifanyiwa vituko mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo, kufuatiliwa nyendo zao, kuhojiwa na hata kutiwa nguvuni. Wengine wamekuwa wakiteswa. Wengine wamekuwa wakiuawa. Matendo ya kutisha yaliyofanywa tangu wakati wa mapinduzi ya Februari 14 (na miaka iliyopita) ni mengi kuyataja na suala la Safy ni moja wapo ya mengi.

Illustration by Jafar al-Alawy

Picha imechorwa na Jafar al-Alawy

Wengi wenu huenda hamfahamu Safy; ni mmoja wapo wa kizazi cha watu wazima cha wanablogu anayependa kufahamika ingawa amekuwa mstari wa mbele, akikabiliwa na uwezekano wa kukamatwa, kuteswa na huenda hata kusahaulika. Safy ni mtu wa aliyewahi kufanya kazi kama Afisa wa Teknohama mpaka aliposhuhudia rafiki yake akipigwa risasi na polisi wa kutuliza ghasia wakati wa wiki ya kwanza ya mapinduzi. Hakuweza kubaki kuwa ‘mtu wa kawaida’ baada ya tukio hilo. Baada ya miezi kadhaa ya ku-blogu kwa siri, Safy aliamua kutumia jina lake halisi na picha yake. Aliwasaidia waandishi wenzake kusafiri, aliwachukua kwenda vijijini ambako watu walivuta moshi wa mabomu ya machozi kuliko hewa ya oksijeni, ana alizungumza kwa lugha kali mbele ya kamera. Aliamua kujiunga na Global Voices pamoja na hatari zinazowakabili wanablogu wa Bahrain wanapochangia habari kwenye majukwaa ya kimataifa.

Safy hayupo pekeyake katika mapambano haya: Wapiga picha Hussain Hubail na Qassim Zainaldeen walikamatwa wiki hiyo hiyo, wakifuatiwa na kukamatwa kwa mwanasgeria binafsi wa Safy aitwaye Abdulaziz Mousa aliyetuhumiwa kutoa siri ya mahojiano bila ruhusa ya kisheria. Mousa alisema kabla ya kukamatwa kwamba Safy alipigwa wakati wa kuhojiwa na kushitakiwa “kwa kuwa mwanachama wa Mtandao wa Vyombo vya Habari vya Februari 14, akialika na kushiriki maandamano ya umma, akichochea chuki dhidi ya serikali na kuwa na mawasiliano na wanachama wa Upinzani wa Bahraini waliokimbia nchi.

Safy hakuruhusiwa kulala kwa siku nne. Walimpiga makofi, walimpiga ngumi usoni, walimpiga mateke tumboni, mabegani, miguuni na mgongoni. Katika siku hizo nne, alikuwa amefungwa pingu na hakuruhusiwa kukaa kitako. Haya yote yalitokea katika chumba chenye baridi kali mithili ya jehanamu ya barafu. Kama ilivyo kwa watesaji wa Bahrain, walimtukana muda wote, wakimwita msaliti wa Washia kibaraka wa Iran na mtu asiye na heshima. Walitishia kumbaka yeye na dada zake. Safy alipoachiwa huru, tutahitaji kujua habari zaidi za jinamizi aliloishi nalo akiwa gerezani.

Mwaka uliopita, Safy alionekana kwenye taarifa ya Dan Rather kuhusu Bahrain. Alipoulizwa ikiwa anahofia mateso kwa kusema wazi wazi akiipinga serikali, Safy alijibu, “Sijali tena. Rafiki zangu wamefungwa. Baadhi bado wanatumikia vifungo. Wengine wako mafichoni na wengine wamepoteza maisha…mwisho wa siku kama haupati heshima unayostahili, mambo mengi wala hutayajali tena.” Kwa mwanablogu huyu, mateso ni matokeo yanayotarajiwa kwa hiari yake ya kuamua kupingana na ukatili unaofanywa na utawala wa kidikteta. Utayari wake wa kukubali matokeo wapaswa kutufanya tupige kelele zaidi kumtetea. Katika nchi kama Bahrain, uhuru wa maoni ni kosa kubwa la jinai kwa watawala; udikteta huu unatishiwa na jitihada zinazolaaini matendo yote ya utawala huo wa kimla na kikatili.

Wanablogu wengi tayari wameonyesha kushirikiana na Safy lakini wengine wengi wanahitajika kumpigania rafiki yetu huyu aliyewekwa kifungoni. Hatutaki kumwacha Safy akiwa mkiwa, hatutaki kuona matukio ya vifo na utesaji yakionekana kama mambo ya kawaida, hatutaki kuacha taswira mbaya iendelee kuwa wananchi wa Bahrain hawana lolote la maana, au kwamba miili yao na roho zao hazina thamani. Kumfikiria Safy akiwa gerezani huku akipigwa na kuteswa ni sababu tosha ya kutufanya tujisikie kutokutulia.

 

Kampeni ya #SafyAachiweHuru

Tunawasihi wasomaji wetu kusambaza habari hii kwa watu wengi. Tumia alamahabari #FreeSafy [SafyAachiweHuru na tafadhali twiti viungo vya Taarifa kwa Umma au taarifa za hivi karibuni za Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain. Tumia picha ya kampeni hii inayoonekana hapo juu ili kuweka msisitizo wa kesi yake na soma zaidi kumhusu Safy na kamepni yake hapa chini

Mwandishi wa zamani wa shirika la CBS News Dan Rather alimhoji Safy mwaka 2012. Tazama kipande hiki cha video hapa kutoka kwenye kipindi hicho cha habari hapa:

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.