Soma pia: Namna Shambulizi la Westgate Lilivyodalidiliwa kwenye Mitandao ya Kijamii na Mwandishi wa Global Voices Awakumbuka Marafki Waliouawa kwenye Shambulio la Westgate.
Mnamo Septemba 21, 2013, kikundi cha watu wenye silaha wanaodhaniwa kuwa al-Shabab walivamia jengo la Westgate jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, wakiua watu wasiopungua 61, wanausalama sita na kujeruhi mamia ya watu wasio na hatia wakiwamo watoto.
Kufuatia shambulizi hilo la kusikitisha, Ushahidi wamekuja na zana mbili mahsusi kwa dharura . Ushahidi kampuni ya teknolojia isiyoendeshwa kibiashara iliyobobea katika kutengeneza zana huru za bure kwa ajili ya kukusanya na kutazama habari pamoja na utengenezaji shirikishi wa michoro.
“Ushahidi”, neno linalotokana na maana yake halisi ya kiswhaili, ilikuwa tovuti ambayo ilitengenezwa awali kwa ajili ya kutengeneza michoro inayotokana na taarifa za ghasia zilizokuwa zinapokelewa nchini Kenya baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi mwanzoni mwa mwaka 2008.
The Ping ni zana tumizi yenye sehemu mbili, chaneli kadhaa za kuingia na kumtafuta mtu inayoweza kutumiwa na watu kadhaa kwa pamoja. Zana hii inatawasaidia wanafamailia, marafiki na makampuni yanayotaka kutafutana kwa haraka:
Kuna tatizo sugu katika kila janga linapotokea, si tu nchini Kenya, lakini mahali kokote. Vikundi vidogo, wanafamilia na makampuni yanahitaji kutafutana. Wanahitaji “kupigiana alamu” kuhakikisha kuwa wako salama. Ili hilo liwezekane, inabidi zana hiyo iwe rahisi sana, isiyohitaji kufikiri sana. Watu wamekuwa wakitumia njia zinazofanana na hili tunalolisema tangu siku za nyuma, kwa mfano watu wanaotumia simu za kisasa (smartphone) wanaweza kutumiana ujumbe wa “niko salama”, lakini inabidi hilo liwezekane hata kwa simu za kawaida sana. Lengo letu ni kuifanya zana hii ipatikane kwa ajili ya matumizi ya kila mmoja duniani.
Hivi ndivyo Ping inavyofanya kazi:
Unatengeneza orodha ya watu wako (wanafamilia, taasisi), na kila mmoja anamworodhesha kila mmoja aliye kwenye orodha (mwenzi, mshiriki wa chumba, rafiki wa kike/kiume, nk). Janga linapotokea, unatuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kila mmoja kujua hali zao. Mtu anayedhibiti orodha hiyo hutuma ujumbe wenye herufi 120 ambao huwa na maneno “uko salama?” mwishoni.
Ujumbe huo huenda kwa mfumo wa kawaida wa Ujumbe mfupi wa simu (SMS) na barua pepe (chaneli nyingine zitaongezwa baadae).
Ujumbe huenda mara tatu, mara moja kwa kila dakika tano. Kama hapatakuwa na majibu, basi mtu huyo aliyetumiwa atachukuliwa kuwa yuko salama. Ikiwa hapatakuwa na majibu, ujumbe huo hutumwa kwa wengine walio kwenye orodha.
Kila jibu linakuwa katika mojawapo ya maeneo matatu: alijibu (imethibitishwa), hajajibu, hayuko salama.
Kila ujumbe unaorudi kutoka kwa mtu aliye kwneye orodha hiyo hutunzwa katika kapu kubwa la ujumbe, na mtu anayedhibiti orodha hiyo huweza kuongeza ujumbe ikihitajika.
Zana nyingine ni Kujitolea Damu Kenya, ambayo ni ramani ya vituo vyote vya kupokelea damu. Ramani hiyo huoanisha vituo vya kupokelea damu na watu wanaohitaji kujitolea damu, vifaa vya kitabibu au wafanyakazi wa afya.
Erik Hersmann anaeleza mantiki ya ramani:
Mmoja wapo wa jamaa mahodari sana nchini Kenya katika kila wakati wa dharura ni Philip Ogola wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya. Huwa wa kwanza kwenda kwenye eneo la tukio akiwa na habari za wakati husika, lakini kwa kweli haiwezekani mtu mmoja kufanya zaidi. Sasa, Msalaba Mwekundu Kenya wenyewe wamekuwa wakifanya kazi kubwa, lakini wana tatizo kwamba wafanyakazi wao wengi bado wanategemea sana kalamu na karatasi (na kuna kikundi cha watu wengine, wakiongozwa na Nivi wa eLimu, wanaojaribu kutengeneza mfumo wa “database” utakaokuwa wa humu humu nchini ili kufanya kazi hii iwe ya kidijitali bila kulazimika kuweka majina halisi ya watu mtandaoni). Tatizo jingine wanalokumbana nalo ni kwamba hospitali zinaishiwa damu, na zinazidiwa, hata wanapokuja watu kwa ari kubwa kuja kujitolea damu.
Namna gani hili linaweza kudhibitiwa vizuri zaidi, ili watu wasikumbane na usumbufu wa kuondoka katika vituo fulani [kwa sababu wameambiwa damu yao haiendani na inayohitajika sehemu hiyo] ili basi wajue wanatakiwa kwenda wapi kutoa damu ya aina yao?
Tumetengeneza ramani ya kuonyesha maeneo ya kutolea damu, kama sehemu ya juhudi za kuyaoanisha maeneo haya na wale wanaojisikia kusaidia BloodDonationKenya.Crowdmap.com, ama kwa kutoa damu, vifaa vya kitabibu au watu wenye ujuzi wa mambo ya afya.
Soma pia: Namna Shambulizi la Westgate Lilivyodalidiliwa kwenye Mitandao ya Kijamii na Mwandishi wa Global Voices Awakumbuka Marafki Waliouawa kwenye Shambulio la Westgate.