Al Jazeera Yatuhumiwa Kutangaza “Habari za Upendeleo”

Makala haya ni sehemu ya Habari zetu Maalumu za  Wamisri Wamng'oa Morsi

Al Jazeera iko kwenye wakati mgumu nchini Misri kwa kile kinachoelezwa na wengi kuwa ni “upendeleo” wake katika kutangaza habari zake wakati na baada ya kuondolewa madarakani kwa rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi mnamo Julai 4. Kituo hicho cha televisheni kilichopo nchini Qatar kinatuhumiwa kuegemea upande wa wafuasi wa Muslim Brotherhood na kugeuka kuwa mdomo wa kikundi hicho.

Baada ya Morsi kuondolewa madarakani na Jehsi, matangazo ya moja kwa moja kutoka Misri ya kituo hicho cha Al Jazeera, yaitwayo Al Jazeera Mubasher, ghafla yalikatika. Kituo hicho kilitangaza:

Matangazo ya moja kwa moja ya Al Jazeera kutoka Misri yameondolewa hewani pamoja na vituo vingine vya televisheni.

Habari kutoka kwa waandishi wetu zinasema wakati matangazo ya moja kwa moja yakiendelea wanajeshi walivamia jengo na kumkamata mtangazaji, wageni waliokuwepo na watayarishaji wa kipindi hicho.

Siku mbili baadae mwendesha mashitaka wa eneo la Downtown jijini Cairo alitoa hati ya kukamatwa kwa mkurugenzi wa habari wa kituo hicho Abdel Fattah Fayed. Fayed anashitakiwa kwa “kuhatarisha amani miongoni mwa raia na usalama wa taifa kwa kutangaza habari za kichochezi.” Alishikiliwa kwa siku mbili na baadae aliachiwa kwa dhamana.

Siku ya Julai 8, wafanyakazi 22 wa kituo hicho walijiuzulu kwa kile walichodai kuwa “matangazo yalikuwa hayaonyeshi matukio halisi ya hali ya mambo nchini Misri.” Habari nyingine [ar] zinasema wafanyakazi 26 raia wa Misri wamejiuzulu, wakiwemo wanne wanaofanya kazi kwenye ofisi kuu iliyoko Doha.

Mmoja wa watangazaji, Wesam Fadhel inasemekana kuwa aliacha kazi kupitia posti yake kwenye mtandao wa Facebook [ar]. Ujumbe wake unasomeka:

Ninaacha kazi Al Jazeera leo. Kituo hiki kinadanganya mchana kweupe. Wanaonyesha picha za video zilizopigwa zamani kutoka kwenye viwanja vya Tahrir na kusema eti zimepigwa muda mfupi uliopita na kuzirudia rudia kwa masaa kadhaa hewani. Nilipomwuliza Ahmed Abu Al Mahasen sababu ya kufanya hivyo alinijibu nisiingilie mambo yasiyonihusu. Kamera za Al Jazeera ziko Tahrir sasa hivi. Nafadhaika, nimewahi kufanya kazi kwenye sehemu niliyodhani ina weledi lakini [sasa nimetambua] weledi wake unategemeana na hali ya kisiasa.

Kwenye mtandao wa Twita, Elijah Zarwan anatoa maoni yafuatayo:

@elijahzarwan: Mfanyakazi wa Al-Jazeera Misri ameacha kazi kwa sababu ya “habari za upendeleo”: Angeacha kazi tarehe 1 June angekuwa ushujaa http://tinyurl.com/mjculx8

Na Nezar AlSayyad anaongeza:


@nezar:
Kituo cha Jazeera kwa muda wa hivi karibuni kimekuwa cha Kiislamu kama ambavyo Fox News kimekuwa cha wahafidhina wa Republican nchini Marekani kwa miaka mingi.

Katika hali isiyoeleweka sawia, Rawya Rageh, mwandishi wa Al Jazeera jijini Cairo, anatwiti picha za vipeperushi vya kutishia vilivyotupwa nje ya ofisi za Al Jazeera jijini Cairo leo:

A threatening leaflet dropped outside Al Jazeera office in Cairo. Photograph shared on Twitter by @RawyaRageh

Kipeperushi cha vitisho kilichotupwa nje ya ofisi ya Al Jazeera, Cairo. Picha imewekwa kwenye mtandao wa twita na @RawyaRageh

@RawyaRageh: Threatening leaflets dropped near AlJazeera's offices in Cairo – bloodied hand & line ‘lies & other lies’ #Egypt

A lying camera kills a nation reads a flyer thrown outside Al Jazeera office in Cairo. Photograph shared by @RawyaRageh

“Kamera inayodanganya ni maafa ya taifa” ndivyo kinavyosomeka kipeperushi kilichotupwa nje ya ofisi ya Al Jazeera jijini Cairo. Picha imewekwa kwenye mtandao wa twita na @RawyaRageh

@RawyaRageh: ‘Risasi yaweza kumwua mtu, lakini kamera iliyojaa uwongo ni maafa kwa taifa’ kinasema kipeperushi kimoja karibu na ofisi za Al Jazeera #Misri

Makala haya ni sehemu ya Habari zetu Maalumu za  Wamisri Wamng'oa Morsi

2 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.