- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Simu za Bure Kwa Wakulima wa Nigeria?

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Naijeria, Chakula, Maendeleo, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, Mustakabali wa TEKNOHAMA na Maendeleo

Mwisho wa mwaka wa 2012, Wizara ya Kilimo ya Nigeria ilitangaza mipango yake ya kutoa Simu za Mkono bure kwa wakulima vijijini. Kulingana na ripoti hii [1]:

Idusote Ibukun, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo katika serikali ya Shirikisho la Nigeria, aliripotiwa akisema kuwa Wizara hiyo lingetafuta fedha za kununua simu za Mkono zipatazo milioni kumi zenye thamani ya N60 bilioni, kutoka China na Marekani kwa ajili ya kuzisambaza bure kwa wakulima vijijini nchini kote.

Mpango huo uliibua gumzo katika ulimwengu wa blogu za Nigeria. Kikiowo Ileowo [2] anauliza mahali ambapo serikali ilitoa takwimu – kwamba Simu za Mkono milioni 10 zilihitajika kwa wakulima milioni 10:

swali ni … wakulima milioni 10 wako wapi hasa? Je, wao ni wale kutoka jeshi la Wanijeria 16, 074, 295 wasiokuwa na ajira au kutoka kwa 51, 181, 884 walioajiriwa. Kama jibu ni wale wasiokuwa na ajira, ni nini hasa wanazalisha ambacho hakijaiifanya Nigeria kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula?
Sasa, elewa kwamba sehemu kubwa ya uzalishaji wa chakula nchini Nigeria hufanyika kwa njia ya kilimo kinachotumia mashine inayotumia idadi ndogo ya wafanya kazi. ‘Wakulima’ ambao Mheshimiwa Rais anataka kutoa simu za Mkono kwao ni wakulima ambao huzalisha chakula kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya chakula majumbani mwao. Nina bustani nyuma ya nyumba yangu; je hiyo inanifanya nikidhi vigego vya kupokea ‘Simu za Jonathani'? Sioni sababu kwa nini rais kwa kushirikiana na waziri wake wa Kilimo wangeweza kutusi akili za Wanigeria wote kwa kufanyia maigizo wazo zuri kama hili ambalo limebadilisha nchi kama Uganda, Kenya na India.

Kumekuwa na marekebisho [3] juu ya gharama halisi ya simu:

… Waziri wa Kilimo, Dk Akinwunmi Adesina, amesahihisha maelezo ya ripoti ya Katibu Mkuu wa Wizara, Bi Ibukun Odusote, iliyosema kuwa simu za Mkono zingeweza kununuliwa na serikali kwa gharama ya N60 bilioni, maelezo yake ni kwamba Simu za Mkono zitatolewa kwa wakulima kupitia ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi …

[4]

Dr. Akinwumi Adesina, Waziri wa Kilimo wa Nigeria

Dk Adesina, Waziri wa Kilimo aliutetea mradi huo. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema [5]:

Wakati mimi nilifika kwenye bodi ya Kilimo kama waziri wa kilimo mnamo Julai 2011, serikali ilikuwa inatumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye manunuzi ya moja kwa moja na usambazaji wa mbolea ya ruzuku, lakini chini ya 11% ya wakulima waliipata hiyo mbolea. Kiasi fulani cha mbolea iliyolipiwa na serikali haikuwa ikifikishwa katika maghala. Kiasi fulani cha mbolea hiyo kilikuwa na mchanga mwingi kuliko mbolea wakati sehemu kubwa ya mbolea hiyo ya ruzuku ya serikali ilivushwa nje ya mipaka yetu na kupelekwa katika nchi jirani ambapo iliuuzwa kwa bei halisi ya soko.

Suluhisho hili la kiteknolojia, yeye anadai [5] lilimaliza tatizo la rushwa kwenye usambazaji mbolea:

Tulimaliza ufisadi uliodumu kwa miongo minne katika sekta ya mbolea ndani ya siku 90 baada ya kuingia ofisini kama waziri. Tulifanikiwaje? Tuliweza kufanya mbolea na mbegu za ruzuku zenye viwango vya juu zipatikane kwa wakulima wetu wa vijijini na kuanzisha GES (Msaada wa Uwezeshaji wa Kuimarisha) mwezi Aprili ya 2012. Mpango wa GES huwezesha kupatikana kwa mbolea na mbegu kwa wakulima moja kwa moja kwa kutumia simu za Mkono za wakulima. Tumetengeneza jukwaa la kielektroniki (mkoba-pepe) ambako tuliwasajili wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo wanaomiliki maduka yanayouza pembejeo za kilimo kote nchini. Hadi sasa tumeweza kuwasajili wakulima milioni 4.2 na pia wafanyabiashara wa mazao ya kilimo 900.

Waziri anadhani [5] kwamba ingawa wakulima wengi Nigeria hawajui kusoma na kuandika lakini wana uwezo wa kutumia simu ya mkononi:

Baadhi ya watu wanadhani kwamba wakulima wetu hawana elimu na hovyo hawawezi kutumia simu za mkononi. Ushahidi haukubaliani na madai hayo. Chini ya mpango wa GES, tuliwezesha wakulima kufanya miamala ya kibiashara kwa kutumia lugha zao za kiasili kwa kutumia simu za mkononi. Kutokana takwimu tulizozikusanya kwa kuangalia namna wakulima wanavyotumia simu za mkononi kupata mbolea na mbegu kwa mwaka jana, tuligundua kwamba idadi ya miamala iliyofanywa kwa njia ya simu katika mpango wa GES ilifikia 4,900,000. Kati ya hizi, milioni 1.2 ilikuwa katika Kiingereza, 620,000 ilikuwa katika ki-Pidgin, milioni 2.2 ilikuwa katika Kihausa, na 854,000 ilikuwa katika ki-Yoruba na 344 ilikuwa katika ki-Igbo. Kutokana na takwimu hizi, hatuna shaka kwamba wakulima wetu wanao uwezo wa kutumia simu za mkononi.

Teknolojia, kwa mujibu wa Dk Adesina [5], imesaidia ubashiri wake kwamba hakutakuwa na ukosefu wa chakula hata baada ya mafuriko kukumba baadhi ya maeneo ya nchi:

Wakati mafuriko yalipotokea, kulikuwa na taharuki katika nchi … mimi sikubabaika kabisa. Tulitumia teknolojia ya kisasa kuongoza uamuzi wetu. Kwa kutumia teknolojia ya kujua maeneo na matumizi ya picha za satelaiti, tulichora picha za kiwango cha mafuriko na kufahamu kuwa si zaidi ya asilimia 1.17 ya eneo lililolimwa lilikuwa limeathirika na mafuriko. Wapinzani wetu walitaka dunia kuamini kinyume, kwamba ukosefu wa chakula usingekwepeka. Walikuwa wamekosa. Leo hii, miezi mitano baada ya mafuriko, hatuna ukosefu wa chakula.

Hata hivyo, baadhi wana-mtandao bado wana maswali yasiyojibiwa. Olusola Adegbeti anauliza [6]:

Mtu anaweza kuuliza, ingawa ni swali lisilohitaji jibu, kama ununuzi na usambazaji wa Simu za Mkono za GSM kwa mamia ya wakulima walioenea katika urefu na upana wa nchi hiyo kubwa, ni muhimu zaidi kuliko changamoto ya masuala yanayoikumba sekta ya kilimo ya Nigeria wakati huu? Hisia zako kuhusiana na suala hili ni nzuri kama langu. Nikirejelea swala hili, ni rahisi kusema kwamba mtu hana haja ya hekima ya Solomoni au ufahamu unabii wa Isaya kwa kuongozwa katika mwelekeo kuwa kunayo masuala mengi ambayo tangu kitambo yameikumba sekta ya kilimo. Masuala kama vile kama ukosefu wa upatikanaji rahisi wa ardhi ya kilimo, ukosefu wa taasisi za kuaminika na zisizo na mianya ya rushwa ili kuwawezesha wakulima kupata mashine za kisasa zinazohitajika kwa ajili ya kilimo cha kibiashara ambacho kwa kawaida huwa ndio uti wa mgongo wa kila taifa, ukosefu wa upatikanaji rahisi wa teknolojia zinazohitajika katika kilimo na mfumo wa kuwezesha kupatikana kwa dawa za kilimo kwa ajili ya kilimo endelevu kwa mwaka mzima pamoja na ufugaji ….

Jarida la Sun [3] linauliza kama kweli wakulima wanahitaji Simu mpya za Mkono, wakati tayari wana namna moja au nyingine ya vyanzo vya habari?

Ni wazi pia kuwa Simu ya Mkono si njia bora ya kufikia wakulima ambao wengi wao wanaishi katika maeneo ya vijijini. Vituo vya habari vya vijiji na redio ni njia bora zaidi. Kuna njia ambazo serikali inaweza kukuza uzalishaji wa kilimo katika nchi, kuliko utoaji wa simu. Muhimu zaidi, serikali haina haja ya kununua simu kwa ajili ya wakulima kwa sababu wale kati yao ambao wanaweza kutumia simu hizo, tayari wanazo.

Kwa vile Simu za Mkono huuzwa kwa bei ya chini kama kati ya N2000 na N3000 nchini Nigeria, mkulima yeyote anaitwa mkulima anaweza kumudu simu, na zaidi huenda anayo tayari. Kama hawana, kitu ambacho serikali inahitaji kufanya ni kuwapa uwezo wa kuweza kujimudu ili waweze kununua chombo hicho cha msingi.

Disu Kimor [7] anadhani kwamba mradi huu una harufu ya ujanja ujanja:

Miradi ya ujanja ujanja kama hii itaimarisha mtazamo wa uliosambaa duniani kote kuwa wa-Nigeria ni vichekesho tufundoshao kipofu lugha ya ishara. Nchi yoyote inayoendelea kama Naijeria inayotaka kuendeleza sekta ya kilimo, italenga kuifanya serikali iingilie kati kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha utafiti na maendeleo, maji, kuhakikisha gharama ya chini ya mafuta na kazi, ( bila rushwa) pia ruzuku kwa kilimo vifaa na miundombinu ya msingi.

Disu anahitimisha [7]:

Siku moja, vizazi vijavyo vitahukumu vigogo na wanasiasa wa nchi hii ambao kazi kubwa ni kuitafuna nchi au kutumia vibaya fedha za umma zinazohitajika sana.