Wabunge wa Ukraine Wataka Utoaji Mimba Upigwe Marufuku Kisheria

Mapema mwezi Aprili, wabunge watatu toka katika kambi ya Upinzani iitwayo “Svoboda” [“Uhuru”] waliandikisha mswada utakaozuia utoaji mimba nchini Ukraine. Mambo pekee ambayo hayakujumuishwa kabisa katika mswada huu ni pamoja na mazingira ambayo mimba inahatarisha maisha ya mama mjamzito, ugonjwa uliothibitishwa kuwa mtoto hatapona na ujauzito uliothibitika kuwa ulitokana na kubakwa. Hatua hii inakuja mwaka mmoja tu tangu Bunge la Ukraine lilipojaribu na kushindwa kuzuia utoaji mimba.

Katika taarifa ya kufafanua mswada huo, watunzi wa mswada huo walitetea ulazima wa kupitishwa sheria hiyo kwa hoja zifuatazo [uk]:

Pamoja na kupungua kwa tabia hii, kiwango cha utoaji mimba nchini Ukraine bado kinaendelea kuwa kikubwa kabisa miongoni mwa nchi za Ulaya kwani mimba zilizotolewa zilifikia 21.1 kwa kila wanawake 1000 waliofikia umri wa kuweza kuzaa, mimba zilizotolewa ni 45.8 kati ya mimba 100 au mimba zilizotolewa 84 kati ya watoto 100 waliozaliwa.

Ifahamike kwamba [wakati ambao utaratibu uliotangulia wa kuzuia utoaji mimba ulipoanza kutumiwa] uhalisia ufuatao haukutiliwa maanani: kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kitabibu, mimba inapotolewa, mtoto huwa anapata maumivu sawasawa na ya mtoto aliyezaliwa kawaida na akakuzwa halafu akateswa hadi kufa. Zaidi, utoaji mimba una madhara ya afya ya kisaikolojia na kimwili kwa wote waliohusika.

Kwa maeneo mengi ya Ukraine, idadi ya vifo vya watu ni karibu mara tatu ya idadi ya watu wanaozaliwa. Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, sensa ya watu nchini Ukraine ilionyesha kupungua kwa watu milioni tano (kutoka watu milioni 52 hadi milioni 47). Kama kutakuwa na mabadiliko ya kitakwimu ya aina hii, kwa miaka michache ijayo, wahamiaji, hususani kutoka bara la Asia, wataongezeka kwa kiwango kikubwa kabisa katika nchi ya Ukraine.

Moja ya sababu kuu ya uwepo wa hali hii ya takwimu isiyoridhisha ni kuhalalishwa kwa vitendo vya utoaji mimba.

Wabunge hao pia walitilia mkazo mtazamo hasi dhidi ya utoaji mimba unaofanana [ru] kwa makanisa yote ya Kikristo nchini Ukraine

Mswada huu umeleta mkanganyiko mkubwa kiasi cha kuibua mijadala mikali katika mitandao ya intaneti na uraiani.

Watoa maoni wengi, kwa haraka walijadili suala la kuthibitisha mahakamani kuwa mwanamke kabakwa au la. Wanahabari wa kituo kikuu cha televisheni cha Ukraine, TSN, walitanabaisha kuwa, asilimia 10 tu ya makosa ya ubakaji yanafunguliwa mashitaka mahakamani na walimuuliza ndugu Olexandr Sych ambaye ni miongoni mwa waandishi wa mswada huu kuwa, mwanamke angefanyeje kama alipata ujauzito lakini akashindwa kuthibitisha kuwa alibakwa? Mbunge huyo alijibu [uk]:

Sifanyi kazi katika vyombo vya kusimamia sheria na sifahamu kile anachoweza au asichoweza kukithibitisha… lakini kabla ya yote, mwanamke ni lazima ajiepushe na aina ya maisha itakayompelekea kubakwa. Kiuhalisia, mwanamke hapaswi kunywa pombe iliyotengenezwa na makampuni yasiyoeleweka.

Maelezo haya yalisambazwa mtandaoni kwa kiwango kikubwa na kujadiliwa na watumiaji wakuu wa mtandao katika mtandao wa facebook, wakiwemo Wanahabari na wanaharakati.

Mtumiaji wa Facebook Serhiy Masliuchenko aliandika [uk]:

Sheria hii ni jaribio jingine tena la serikali na ni ukiritimba wa kuingilia maisha ya mtu….. wanapokosa maarifa ya kufanya jambo fulani linalohusu uchumi, sayansi, elimu, elimu ya uhusiamo wa viumbe, ndipo wanapoanzisha sheria kama hizi. […]

Mtumiaji wa Facebook Vasyl Martyuk alikuwa na mawazo tofauti [uk]:

Sichukulii Upinzani kuwa kinga kwa wote, lakini ninauunga mkono mswada huu. Nchi ya Ukraine ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya matukio ya utoaji mimba- hali inasikitisha!

Mtumiaji wa facebook, Andrey Anthony aliandika [ru]:

Kabla ya kupendekeza sheria kama hizi, ni lazima kwanza uhakikishe nchi ipo katika hali ya utulivu. Inawezekanaje kupendekeza hatua kama hiyo katika nchi ambayo haina barabara yoyote, hakuna utawala wa sheria, na rushwa isiyo na kikomo? […]

Mtumiaji mwingine wa facebook, Elena Bondarenko aliandika [ru]:

Hii ni nafasi nyingine kwa wataalamu wa magonjwa ya uzazi kwa wanawake kuneemeka kupitia utoaji mimba wa kificho. Je, ni idadi ndogo sana ya watoto wachanga wanaokutwa majalalani? WAPUMBAVU!! Andaa mazingira mazuri ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya malezi na siyo kukataza!!!

Mtumiaji wa Facebook Marianna Goncharova alitoa maoni yake [ru]:

Hili ni miongoni mwa matukio ambayo umakini wa usawa wa kijinsia lazima uzingatiwe. Kwa nini jambo hili linaibuliwa na kushadadiwa na wanaume? […]

Mtumiaji mwingine, Vitaliy Diachenko aliudhihaki mswada huu[uk]:

Kambi ya Upinzani yapaswa kupitisha sheria nyingine ya kuwazuia wanachama wake kufanya mapenzi, hadi hapo watakapopewa hati ya maandishi ya kuthibitisha kuwa nia ya dhati ya tendo la kujamiana ni kwa ajili ya kuzaa watoto tu.

Yevgeniy Ikhelzon alishangazwa na [ru] mwitikio mdogo wa watu kufuatilia mswada huu:

Hiki ni kitendawili. Watu ambao ziku za hivi karibuni walisababisha wanawake wa kiislam kuanza kuvaa hijabu, kwa upole kabisa wanapokea hatua ya wabunge ya kutaka kupiga marufuku utoaji mimba.[…].

Mwandishi wa habari, Iryna Slavinska aliukosoa mswada huu [uk]:

[…] Kukabiliana na idadi kubwa ya mimba zisizo tarajiwa na elimu ya maswala ya uzazi haina budi kuanzishwa mashuleni na ni lazima kuwe na maeneo maalum ambayo kondomu pamoja na dawa za uzazi wa mpango zitakuwa zinatolewa bila malipo badala ya kukataza utoaji wa mimba.

Watumiaji wengi wa mtandao walizungumzia utoaji wa mimba wakihusisha na kanuni na taratibu za kimaadili. Kulikuwepo na mjadala wa aina hii katika ukurasa wa facebook wa Mwanafizikia na Mwanaharakati ajulikanaye kwa jin la Evgeny Komarovsky.

Mtumiaji wa mtandao wa Facebook, Yulia Zheleznova aliandika [ru]:

Hao wanaotoa maoni yao hapa, kwa bahati mbaya, hawajaweza kubadilisha mtizamo wangu, bali wameendelea kuimarisha msimamo wangu niliokuwa nao toka awali. Kwa kukiri, kwa kizazi cha sasa, wapo wanawake wengi ambao sio tu kuwa hawazingatii mambo ya kimaadili, bali pia hawazingatii mambo muhimu ya msingi kuhusiana na afya zao. Hakuna maelezo yoyote ya kuthibitisha mauaji. Hakuna la zaidi.

Akiongezea katika mjadala huo huo, Olga Shandra aliandika [ru]:

Ninafikiri kuwa, kutoa mimba ni chaguo la kila mwanamke kwa kuzingatia kanuni na taratibu zake za kimaadili, na kwa hakika kabisa, siyo swala la wabunge, wanasaikolojia, walimu wa maadili na wengineo.

Mtumiaji wa mtandao, Enela Adonieva aliandika [ru]:

Ninapinga kabisa utoaji wa mimba. Lakini mwanamke lazima awe na maamuzi ambayo hayataingiliwa na wanasiasa.

Kwa hivi sasa, utoaji mimba nchini Ukraine unaruhusiwa kwa mimba iliyo na hadi juma la 12 (na hata juma la 22 katika mazingira ya dharura). Nchi hii ni miongoni mwa nchi za ulaya zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya utoaji mimba kwa mwaka, pamoja na kuwa kuna dalili dhahiri za kupungua kwa matukio ya utoaji mimba. Pamekuwepo na aina mpya ya utalii unaoitwa “utalii wa kutoa mimba” kutoka katika nchi jirani ambapo sheria za kuzuia utoaji mimba zimekuwa kali zaidi sana, kama vile Poland, na zimeandikwa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.